Mwanzoni Utafanya Kwa Tabu Na Maumivu Mengi, Usipokata Tamaa Mwisho Wake Ni Furaha Ya Ushindi.
Jina la Yesu Kristo aliye hai lisifiwe na kila mwenye pumzi ya uhai, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuiona siku hii mhimu sana kwetu. Nafasi nzuri ya kwenda kumzalia Bwana matunda yaliyo mema, hatuendi kuzaa mapooza tunaenda kuzaa kilicho chema machoni pake.
Mwanzo ni mwanzo tu, haijalishi unaanza vipi hilo jambo ila itabaki mwanzo ni mwanzo tu. Tunaweza kuanza jambo kwa tabu nyingi na maumivu mengi sana, lakini tukiwa wavumilivu na kuendelea kufanya kwa bidii bila kuchoka, mwisho wake huwa mzuri sana wa hilo jambo.
Matokeo ya jambo unapolianza mwanzoni linaweza lisionekane la mhimu sana machoni pa watu wengi, au kwako linaweza lisiwe jambo zuri sana kutokana na changamoto mbalimbali unazokutana nazo. Ila utakapovumilia na kuweka bidii katika hilo jema unalofanya, matunda yake ni mazuri sana kuliko maumivu uliyopata huko nyuma.
Tunaweza tusielewe sana na kuona ni mateso yenye adhabu kubwa kujenga uvumilivu wa jambo ambalo wakati mwingine wengi wanaona haliwezekani. Tunapokutana na hali kama zile wengi huwa tunaona bora tuachane nalo, tufanye jambo lingine, sio kana kwamba kuacha kwetu hilo jambo kutaondoa umhimu wa hilo jambo la hasha!.
Tunajua kwa kila mmoja wetu aliyewahi kufanya mazoezi ya mwili/viungo, mwanzoni wakati unaanza bila shaka ulipata maumivu makali sana. Ambapo ilikubidi uendelee kufanya pamoja na maumivu yale, jinsi ulivyozidi kufanya hukusikia tena maumivu, na mwisho wake ulifurahia uamzi ule wa kufanya mazoezi kuimarisha misuli na afya yako, wakati huo unafurahia huna tena yale maumivu makali ya mwanzo.
Unaweza kuona ni mateso kujenga nidhamu ya kutunza ujana wako wakati bado hujaoa/hujaolewa, ila usipochoka njiani ukakatisha uchochoroni, ukamua kutulia mpaka siku yako ifike ya kuoa/kuolewa. Nakuhakikishie hutajuta kushinda ujana badala yake utafurahi sana na kujivunia uvimilivu wako, na kuona ule uvumilivu wako ulikuwa ni bora sana kwako.
Unaweza kuona ni kiasi gani kila jambo lililo na manufaa kwako linaweza kukupa usumbufu mwingi mwanzoni, ila ukiwa na subira kwa unachofanya amini kuvuna kilicho bora zaidi. Hakuna jambo zuri lilitokea kwa bahati mbaya, kuna gharama yake mtu aliitoa ndipo hilo jambo likaonekana ni zuri.
Kwanini nakueleza haya yote, huenda unasoma Neno la Mungu kwa maumivu makali sana na wakati mwingine unaona kama vile hakuna kitu kizuri sana unachokipata. Nikuhakikishie kwamba, kama kweli una safari ya kwenda mbinguni hili jambo utalifurahia siku ukishakolea vizuri kwenye NENO. Wakati ambao utamshukuru sana MUNGU kujua umhimu wa kulisoma Neno lake, waliofikia kiwango hichi watakuwa wananielewa vizuri ninachosema hapa.
Pamoja na changamoto mbalimbali za maisha usikubali kuacha kusoma Neno la Mungu, shikilia msimamo wako mpaka uhakikishe kuna kitu kimejengeka kwako. Ambacho kitu hicho kitakuwa tabia yako ya kila siku bila kujisikia maumivu yeyote. Hakikisha kila siku unayosoma Neno la Mungu, umetoka na kitu cha kukusaidia katika maisha yako ya kiroho na kimwili.
Hakuna kujuta katika hili ndugu yangu, tangu nianze kusikia shuhuda ya waliofanikiwa kusoma Neno la Mungu. Hakuna aliyesema najuta kutoa muda wangu kusoma Neno la Mungu, badala yake wamekuwa wakimshukuru Mungu na kuona zipo siri kubwa sana ndani ya Neno la Mungu.
Unaweza usinielewa sana sasa hivi, kutokana na jinsi ulivyojiwekea utaratibu wa kutojisomea Neno, nakushauri uanze sasa. Kama ulianza lakini unasoma kizembe na huoni matokeo mazuri, ongeza juhudi Zaidi, endelea kuvumilia huku ukimwomba Mungu akusaidie. Mwisho wake utaona ulikuwa wapi siku zote hukujua umhimu wa hili jambo, na utakuwa msaada mkubwa sana kwa wengine.
Acha kusikiliza sauti za uvivu, jiwekee nidhamu binafsi ya kufikia malengo yako ya mwaka huu, uliyopanga usome Neno la Mungu. Acha kuyumbishwa na watu wasio na mpango wa kujifunza Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako, nikutakie siku njema iliyojaa baraka za Mungu.
Endelea kupata masomo mazuri kupitia mtandao wetu,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
www.chapeotz.com