Juhudi Za Mtu Kwa Jambo Lolote Sahihi Huzaa Matunda Mema.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tunamrudishia yeye maana ndiye atupaye uzima wake.

Hatujafanya vitu mpaka kufikia kiwango cha kusema imetosha kufanya, kama tumefanya basi ni kwa kiasi kidogo sana ambacho kinahitaji bidii zaidi ya kufanya vizuri zaidi.

Hatujafanya kazi kiasi kwamba tukafika hatua ya kusema tumepata mafanikio ya kutosha, kwa hiyo hatuhitaji tena kuendelea kupata mafanikio. Kila mmoja anaendelea kupambana kadri awezavyo kufikia hatua kubwa zaidi kimafanikio.

Tunapoweka bidii katika jambo lolote jema, tunapata matokeo mengi sana katika utendaji wetu. Unaweza kufanya jambo kwa bidii lakini mwisho wake ukavuna hakuna, kutokana na changamoto iliyosababisha kupatwa na hasara hiyo. Kuanguka kwako kunaweza kuwa darasa zuri sana la kufanya vizuri zaidi awamu nyingine.

Kama uliweka bidii katika kulima, lakini ikatokea mvua ikaja kukatika njiani mazao yako yakaharibika, msimu mwingine utajitahidi kuwahi kupanda mazao yako. Ili uweze kuendana na msimu wa mvua, unaona ni jinsi gani kuanguka kwa mwenye bidii hakumpotezi bali panamfundisha kitu.

Ndivyo ilivyo kwa mambo ya Mungu, unavyoweka bidii katika mambo ya Mungu kuna baraka nyingi unapata. Pamoja na zipo changamoto nyingi katika bidii yako ya kumtafuta Mungu, changamoto hizo zinaweza kuwa darasa kwako la kuweza kufikia viwango vya juu zaidi.

Penye juhudi na nia ya kweli ndipo pana changamoto mbalimbali za kukuzuia usiweze kufikia lengo lako. Lakini unapojua unachofanya sio kikwazo kwako kuacha kile ulichoanza nacho kufanya, kwa ajili ya kumtukuza Mungu.

Juhudi yako inaambatana kwa ukaribu sana na maono yako, pasipo bidii yako, hata kama una kitu kizuri cha kuubadilisha ulimwengu huu. Hakitatimia mpaka utakapoamua kuanza kukifanya kwa mkono wenye nguvu na usio mlegevu.

Tumekuwa tunahimizana sana umhimu wa kusoma Neno la Mungu, wachache sana wameanza kuona matunda ya hili jambo. Na wengi bado wanaona kama hadithi fulani ya kusadikika, isiyo na ukweli wala mwelekeo wowote.

Unapolipuza jambo huwezi kujitoa kwa asilimia zote kulifanya kwa bidii na ustadi mzuri, kama utafanikiwa kulifanya, utalifanya kwa ulegevu sana. Maana hujui kwa nini unafanya, unakuwa unaenda tu kama mtu asiyejua anaelekea sehemu gani na kutafuta nini.

Anayetafuta dhahabu chini ya udongo, hawezi kukatishwa tamaaa na wingi wa udongo na urefu wa shimo. Akiwa ana uhakika na anachokifanya, uhakika wake wa kuwa na dhahabu chini ndio unaomsukuma yeye kuchimba zaidi. Kuelewa unachokitaka/unachokitafuta, ni mhimu sana kwa mpambanaji yeyote yule.

Mtu aliyeokoka anapaswa kujua umhimu wa Neno la Mungu, anapaswa kujua kwanini iwe kulijua Neno la Mungu na si kitu kingine. Ukishakaa chini ukaelewana na mgongano wa mawazo yako, utaweza kufanya kitu kikubwa sana cha kumpa Mungu muda wako katika kulijua Neno lake.

Hatupaswi kuishia kwenye mbwembwe za maneno mdomoni, tunapaswa kuweka matendo kwa tunayojua yana faida kwetu. Kubaki kusema Neno la Mungu lina faida kwetu alafu huchukui hatua zozote za kulisoma, huko ni maneno bila matendo, na tunaelewa imani pasipo matendo imekufa.

Uwezekano upo wa kuamua kuanzia leo kuweka juhudi katika hili la kusoma Neno la Mungu, hakuna namna utasingizia hili. Ikiwa ndani yako una huduma ambayo Mungu amekupa, unapaswa kulijua Neno La Mungu vizuri ili uwe na ufanisi katika kuwahudumia wengine.

Huwezi kuwahudumia wengine kwa kutoa tu mawazo yako kichwani kila siku bila kutumia Neno la Mungu, Neno la Mungu ni mwongozo kwako kuweza kutoa huduma iliyo kamilika.

Tabia ya Neno la Mungu ni nzuri sana, Neno linaanza kukufundisha wewe kwanza kabla ya mwingine, kama ni kukuonya litaanzia kwako, kama ni kukukemea litaanzia kwako, kama ni kukurejesha kwenye mstari litaanzia kwako. Mpaka kumfikia mwingine utakuwa mwenyewe binafsi limekufanya upya ndani yako.

Juhudi zako za kusoma Neno la Mungu, halikusaidii tu kutoa huduma nzuri, linakusaidia hata wewe uweze kusimama kuhubiri/kuimba ujumbe uliokamilika. Pia unaweza kuhubiri kwa matendo yako bila kusema na mtu, watu wakampokea Yesu Kristo kupitia tabia yako njema.

Watu wanaweza kumpokea Yesu Kristo kupitia ufanisi wa utendaji wako wa kazi zako ofisini, ufanisi usio na michanganyo ya miungu mingine. Watu wanaweza kumpenda Mungu kupitia juhudi zako za kuutafuta uso wa Mungu, maana wanaona mpo bize wote ila wewe unapenyeza kumpa Mungu muda wako.

Watu wanakuona badala ya kukaa kijiweni kupiga tu majungu na umbea, wanakuona umetulia ndani kwako ukisoma Neno la Mungu. Juhudi za mtu zinaonekana siku zote, sio kana kwamba mtu yule anajionyesha/kujitangaza la hasha.

Weka juhudi/bidii ya kusoma neno la Mungu, matunda utakayoovuna ni mengi kiasi kwamba hutojuta kwanini uliamua kutoa muda wako kwa ajili ya kujifunza Neno la Mungu. Usisubiri kuwa na muda mwingi sana, anza na huo huo muda mdogo unaoupata, unaweza kuamua kupunguza na kuondoa kila kitu kinachokula muda wako.

Unaweza kuamua kujiondoa kabisa kwenye magroup ya wasap yasiyo kuongezea kitu, mfano yale ya kuchati kutwa nzima mpaka wakati mwingine unashindwa kufanya kazi zako. Unaweza kupunguza kuzurura facebook ukabakisha kufuatilia mambo ya msingi tu, na ukaweka muda wako kusoma Neno la Mungu.

Unaweza kupunguza muda wako wa kukaa sana na marafiki zako mkipiga stori mbalimbali, ukampa Mungu muda wa kusoma Neno lake. Ukishafikia hatua hii, bidii yako itaanza kuonekana kwa matokeo mazuri utakayoanza kuonekana nayo.

Vipo vitu usipovifanya au usipovishiriki haviwezi kukuondelea kitu chochote, ila vipo vitu usipovifanya vinapunguza kiwango kikubwa sana cha wewe kuwa na uelewa mdogo wa yule unayemwabudu na kumtumikia, Yesu Kristo.

Kwa maneno haya machache utakuwa umepata kitu kimoja cha kukusaidia katika safari yako ya wokovu. Nami nimshukuru Mungu kwa ajili yako kutoa muda wako, kusoma ujumbe huu, nasema Mungu akubariki sana.

Usiache kufuatilia masomo mbalimbali mazuri kupitia mtandao wetu,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com