Muda Upi Ni Sahihi Kwako Kujifunza.

Nakusalimu Ndugu yangu katika Kristo, siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali kingine cha kuiona leo. Hatuwezi kunyamaza kimya kwa sababu jana tulilala kwa maumivu makali ya kuumizwa na jambo fulani, sifa na utukufu lazima tumrudishie Bwana wa mabwana.

Nashindwa kuelewa kabisa, hivi tuna shida gani inayotufanya tushindwe kumpa Mungu wetu muda wa kulisoma Neno lake. Mtu anasema sina kabisa muda wa kusoma Neno la Mungu, wakati huohuo unamwona anazunguka mitandaoni bila kazi yeyote ya msingi anayofanya.

Mtu anakueleza kwa umakini mkubwa, lengo ni kuja kusimamia kujipa sababu ya kutokusoma Neno la Mungu. Wakati anatoka kazini muda mzuri kabisa ambao unatosha yeye kutulia mbele za Mungu kujifunza Neno lake, wakati huo muda anaotoka shuleni ni mzuri kabisa wa kufanya shughuli za nyumbani kisha kupata nafasi ya kushika biblia yake.

Hebu tujiulize tuna matatizo gani ambayo yanatufanya kiasi kwamba, kuanzia asubuhi yote, mchana yote, jioni yote, usiku wote. Kila siku inayoingia na kutoka, hatuwezi kabisa kabisa kusoma Neno la Mungu au tunaona ni jambo la ziada tu.

Kutokujua kwako Neno la Mungu hakutakupa ofa ya kuepuka hukumu ya Mungu, huwezi kusema sikujua alafu ukaambiwa na Yesu Kristo ingia kwenye furaha ya milele kwa sababu ulifanya uovu bila kujua. Huko ni kujidanganya, kila mmoja anapaswa kutenga muda wa kusoma NENO na kulitafakari yale aliyojifunza.

Mwenye Neno la Mungu la kutosha ndani ya moyo wake, hawezi kumtenda Mungu dhambi ovyo ovyo. Maana ndani yake imo hofu ya Mungu, ndani yake kuna alarm inayomsaidia kupiga kelele pale anapotaka kwenda kinyume na utaratibu wa kiMungu.

Kujifariji huna muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu wakati mnashinda sehemu za starehe na marafiki zako, mkidai mnabadilishana mawazo. Huko ni kujaribu kukwepa jambo la mhimu kwa kufuatisha mwili unavyotaka wenyewe, maana nia ya mwili si wewe utende Jambo la KiMungu. Ndio maana upo wakati unataka kuomba mwili unakuzuia kwa kusema umechoka, kuna wakati utamani kutenda mema ila mwili wako unakusuma kutenda mabaya.

Tujiulize tutakuwa watu wa kushika biblia siku za jpili mpaka lini, tutabadilisha lini matumizi ya biblia kama urembo ambao unakuwa nao siku za ibada. Ila ndani hujui kabisa thamani inayopatikana, zaidi ya kukariri mistari michache ya kudokoadokoa.

Chukia sana kujipa sababu za kujaribu kukwepa kusoma Neno la Mungu, moyo wako ukushuhudie kweli leo umeshindwa kusoma Neno la Mungu kwa sababu ambayo hata wewe mwenyewe husikii dhamiri ikikushitaki. Siku ina masaa 24 ushindwe kupata lisaa limoja kwa ajili ya kusoma hata sura moja, kisha utulie kwa dakika chache kutafakari, kweli ukose!

Binafsi nakataa kabisa, wengi hatuna uzito kabisa na hili la kusoma Neno la Mungu, tumeona ni kazi ya wachungaji kutusomea NENO siku za ibada. Cha kusikitisha siku zenyewe za kukutana ibadani zinakuwa zimejaa mambo mengi, na muda mchache sana kwa kusomewa maandiko.

Mtu yupo ndani ya wokovu mwaka wa 20 sasa lakini bado mchanga kiroho kiasi kwamba aliyeokoka mwaka jana alafu akawa na bidii, na mambo ya Mungu. Ana afadhali kubwa kuliko huyu ambaye anajivuna ameokoka siku nyingi, lakini ukimtazama matendo yake yanakataa kabisa huo muda anaosema yupo ndani ya wokovu.

Nimeshakuambia kusoma Neno la Mungu ni suala la lazima kwa mkristo Mwenye safari ya kwenda mbinguni. Hichi ni chakula kabisa usipokula unakufa, sema tofauti yake hichi ni chakula cha kiroho. Uhai wetu wa kiroho unategemea sana bidii yetu ya kuwa karibu na Mungu wetu.

Tunapojibidiisha katika mambo yake, tunafanyika watoto wake wema, utazaa matunda mema kwa kupanda mbegu bora. Mbegu ni Neno la Mungu unayoipanda ndani yako kila siku, maarifa yote yanapatikana ndani ya Neno la Mungu yanakusaidia wewe.

Hebu kuanzia leo fukuza kukaukiwa kiu ya kumjua Mungu, kataa uvivu wa kutokusoma Neno la Mungu, kataa kabisa visababu vya kukufanya kuendelea kubaki vilevile. Hivi hujiulizi utatoaje huduma ya kiroho usipokuwa na Neno la kutosha ndani yako, hivi hujiulizi utamshuhudiaje mtu habari za Yesu Kristo ikiwa ndani yako huna uhakika na unayemshuhudia.

Wengi ni mafundi wa kutumia nguvu nyingi kubishana ila ndani yao kabisa wamejaa uchanga wa kiroho, kwa sababu vitu anavyoshikilia kubishana havipo kabisa. Tutakuwa na hali hizi mpaka lini, tunapaswa kuzikataa kwa kuweka matendo ya kusoma Neno la Mungu.

Ikiwa wewe ni mwimbaji na husomi Neno la Mungu, muda sio mrefu utaanza kutuimbia yasiyofaa, ikiwa wewe ni mwombaji na husomi neno la Mungu utaanza kuomba hata vile ambavyo umepewa. Lakini unakuwa hujui kama umepewa kwa kutojua kwako Neno la Mungu.

Acha sababu zako, shika biblia yako, utaona ahadi zako, utafunguliwa ufahamu wako, na utaacha tabia za kitoto. Fanya zoezi hili la kusoma Neno la Mungu kila siku, iwe masika au kiangazi wewe soma NENO, huo ndio mwongozo wako.

Mwenye ufahamu na afahamu, na Mwenye sikio na asikie, mimi nimefanya iliyo sehemu yangu. Usije sema hukujua, nimekueleza umhimu wa kusoma Neno la Mungu vya kutosha. Nina ujasiri wa kusema ni uvivu wako unaokufanya usiwe na muda wa kusoma Neno la Mungu.

Nikushukuru kwa muda wako, uwe na siku njema.
Kupata masomo mengine mazuri zaidi, endelea kufuatilia mtandao wetu.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com