Lenga Kile Unachokifanya Hata Kwa Hatua Ndogo Utafikia Lengo Kubwa.

Haleluya mwana wa Mungu, siku nyingine tena Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona leo, bila shaka kila mmoja anapaswa kuweka alama njema ya kumtukuza Bwana. Pia leo inaweza ikawa ni siku yako njema ya kufurahi na familia yako. Kukaa nao Karibu kuwasikiliza changamoto wanaopitia watoto wako. Kukaa na mke/mume wako kupanga mipango yenu kwa uhuru zaidi, kukaa na wazazi wako kuwasikiliza mahitaji yao ambayo wanategemea kutoka kwako uwatendee.

Karibu sana tujifunze pamoja namna gani tunaweza kufikia lengo letu la kusoma Neno la Mungu, unaweza ukawa na hoja nyingi ndani yako. Lakini ukisimama vizuri na Mungu wako, utashinda hili na utafurahia usomaji wako wa Neno la Mungu.

Juhudi zako ndogo unazoweka kila siku, matokeo yake yanaweza yasiwe makubwa sana siku za mwanzo. Ila kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo zile juhudi zako ndogo zinazidi kuzaa matunda na kuonekana unafanya kitu kikubwa.

Huwezi kufanana na mtu ambaye anasubiri aje anze na hatua kubwa, watu wa kusubiri waje waanze na hatua kubwa mara nyingi huwa hawafanikiwi. Huwa wanaishia kwenye maneno ya mdomoni pasipo kuweka vitendo vyovyote.

Mtu aliyejitoa kusoma sura moja ya biblia tangu tunaanza mwaka huu, mtu huyu atakuwa na hatua kubwa sana kuliko yule anayeimba kila siku nitaanza kesho kwa kusoma sura tano kwa siku. Cha kushangaza mpaka leo hajaanza, na kama ameanza alifanya hilo zoezi kwa mwezi mmoja tu akaishia hapo. Lakini huyu wa sura moja tangu anze kusoma bado anaendelea, na hatua yake ni kubwa mno.

Unaweza kumdharau mtu anayepanda mbegu kila siku mashimo kumi shambani mwake, kwa hesabu za siku sita za wiki atakuwa na mashimo 60. Ambapo unaweza kuona ni tofauti na mtu anayesubiri kuanza na mashimo 60 kwa pamoja wakati hana hizo nguvu.

Kusoma Neno la Mungu kunahitaji uvumilivu wako, hatua unazozipiga usizidharau hata kidogo, uelewa wako mdogo usiudharau kabisa. Hatua zako ndogo ndogo zinazoonekana za kipuuzi kwa wengine, zisikukatishe tamaa ukaacha kuwa Karibu na Mungu wako.

Jifunze kuepuka kelele za watu wanaongea sana bila vitendo, kuna mafundi wa kuongea kiasi kwamba unamwona kabisa kwa kauli hizi. Kesho tu ataimeza biblia yote, ukija kumfuatilia unakutana na hewa.

Hebu fikiri tulianze kusoma kitabu cha Nyakati, tumeenda hatua kwa hatua mpaka leo ninapokuandikia hapa tumemaliza Nyakati wa 1 &2. Unaweza kuona kama jambo rahisi sana au gumu sana, ila ukweli ni kwamba tulianze wengi. Lakini waliofanikiwa kufikia lengo hili ni nusu yake tulioanza nao, wengine wakaishia njiani.

Unaweza kuona ni jinsi gani unaweza kutengeneza akiba ya kutosha kwa kuanza na hatua uliyopo sasa. Labda nikutolee mfano huu utanielewa zaidi; ni sawa na mtu anayesubiri awe na mshahara mkubwa ndio ataanza kujiwekea akiba, anashangaa anapata huo mshahara matumizi nayo yanazidi kuwa makubwa zaidi.

Lile wazo lake la kuweka akiba anaona linakuwa gumu, anachofanya anajipa muda mwingine. Siku zinazidi kwenda na kustafu kwake kunakaribia, hapo ndipo anapobadili mawazo ya kuona akiba yake ni ile pesheni yake. Hapa nimekutolea mfano wa mfanyakazi wa serikali au shirika, bado wapo waajiriwa wa mkataba, bado wapo wafanyabiashara/wajasiliamali.

Wote tunaijua methali ya *haba na haba hujaza kibaba,* kuna maana kubwa sana kwa hii kauli ya haba na haba, yaani kwa lugha nyingine tunaweza kusema kidogo kidogo hujaza kitu kikubwa. Huwezi kuelewa sana ukiifikiri kwa kawaida na kwa upande mmoja, lakini kwa mifano hiyo naimani kuna kitu umekipata vizuri.

Furahia hatua ndogo unayopiga maana ndiyo inakupeleka kwenye hatua kubwa, usipoifurahia hiyo hatua ndogo unayopiga itakuwa ngumu kwako kufikia hatua kubwa.

Usibaki umekaa ukisubiri utafanya kwa pamoja, wengi wamesubiri hivyo ila mpaka leo wanaendelea kusubiri bila mafanikio yeyote. Wewe usikubali kuwa katika kundi hilo, kuwa kwenye kundi la watu wanaoanza na walichonacho mkononi.

Naona kama vile nakufundisha kuanzisha biashara!! yote ni mema ila mimi sipo huko sana, ninachokufundisha hapa ni namna ya kusoma Neno la Mungu. Kutoa muda wako kila siku kutakufanya ufike mbali sana, zingatia sana hili.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com