Uwe Mwangalifu Na Changamoto Zinakupata Zisikuondoe Kwenye Kusudi La Mungu.

Nakusalimu katika jina lipitalo majina yote, jina la Yesu Kristo aliye hai, ni siku nyingine tena mpya kabisa Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona. Hatuna budi kumshukuru Mungu wetu na kumazalia matunda mema kwa kila mmoja aliopo nafasi yake. Haijalishi wewe ni mwanafunzi unapaswa kumzalia Bwana matunda kwa kile amekujalia ndani yako.

Leo nikukumbushe tena hili jambo la msingi sana ambalo usipokuwa nalo makini utajikuta unachanganywa na kutolewa nje ya kusudi la Mungu. Unaweza usielewe sana wakati unatolewa ila kukubali madhaifu na changamoto mbalimbali zinazokupata sasa, ni rahisi sana kuacha mambo ya msingi.

Kila kukicha yanaibuka mambo mapya, linaweza kuwa jipya kwako kwa jinsi litakavyokugusa maisha yako moja kwa moja. Hayo mambo yanaweza yasiwe mzigo kwa mtu mwingine wala yanaweza yasiwe shida kwa sababu hayawalengi wao moja kwa moja.

Tunaumizwa sana na mambo pale yanapotufika moja kwa moja, acha yale yanayowapata rafiki zetu. Hayo yanaweza yasiwe na uzito mkubwa sana kwenye moyo wako, wala yanaweza yasikunyime usingizi wowote. Ila hilo hilo jambo ulilokuwa unaliona la kawaida kwa mwenzeko, linaweza kukupelekesha sana pale litakapokukuta mhusika.

Leo rafiki yako anaweza kukuambia anauguliwa na mtoto wake, hiyo taarifa inaweza isiwe na uzito mkubwa sana kwako. Ila siku likifika kwako mwanao akapata shida ya mwili wake ukaanza kuhangaika huku na kule, wakati mwingine unaona kama huoni mabadiliko yeyote ya kupona pamoja na madaktari kumpa huduma. Hapo ndipo utaelewa nini maana ya kuuguliwa na mtoto, lakini kabla halijakupata utaona ni kawaida sana.

Leo unaweza kuletewa taarifa zisizo nzuri sana kwenye masikio yako, hizo taarifa zisipokutana na moyo uliojaa Neno la Mungu. Bila shaka hizo taarifa zinaweza kugharimu maisha yako kwa kiasi kikubwa sana, maumivu yale yanaweza kuwa ni chanzo cha kukuvurugia mipango yako yote.

Tunapozungumza Changamoto mbalimbali za maisha, kila mmoja anaguswa kutokana na uzito wa jambo lenyewe. Huwezi kuelewa sana kama hujashuhudia hilo jambo lililomkuta mwenzeko, unaweza usielewe sana hata kama mna ukaribu fulani. Unaweza kuwa na mwenzeko kwenye msiba, ukafikiri unalia na rafiki yako kumbe mwenzeko anaona kawaida tu.

Hayo ninayokueleza huwezi kumlazimisha mtu ajisikie uchungu unaoupata wewe, kila mtu anaguswa na jambo kutokana ukaribu aliyenaye na huyo mtu. Binafsi naweza kuumizwa na jambo la rafiki yangu kutegemeana na ukaribu tulionao, au wakati mwingine nisiumizwe kabisa kutoka ndani moyo wangu kutokana na umbali wetu.

Huwezi kuwa na kipimo halisi cha kujua watu ulionao wanalia pamoja na wewe, hata kama mmekaa pamoja mkiomboleza. Ila tunatiwa moyo pale tunapoona wenzetu wanatujali na kutufariji pale tunapokuwa kwenye shida fulani. Haijalishi wanaumia sana au wanaumia kidogo au hawaumii kabisa. Hilo haliwezi kuwa jambo la msingi sana kwetu, kinachotufanya tuone tupo pamoja na wenzetu ni pale wanapojumuika pamoja na sisi wakati wa majonzi yetu.

Kweli kabisa Changamoto zipo kama nilivyotangulia kusema hapo juu, hizi Changamoto tusipoziangalia kwa umakini. Zinaweza kutuondoa kabisa kwenye Kusudi la Mungu, unaweza kuwa mtumishi mzuri wa Mungu, lakini utakaporuhusu moyo wako kutaliwa na hali ngumu unayopitia leo. Hapo ndipo utaona hakuna haja tena ya kuendelea kumtumikia Mungu wako, hii inakuja katika hali ambayo huwezi kuielewa sana wakati huo.

Unaweza kupigwa na changamoto mbili tatu ukapoteza mwelekeo kabisa, ile nguvu ya Mungu uliyokuwa nayo ndani yako ikapotea kabisa. Hadi wale wanaokujua wanajua kabisa umepoa kiroho, zinaanza zile hadithi jamaa alikuwa vizuri sana zamani, huyu mama/dada alikuwa ni mtu mwingine kabisa kwenye mambo ya Mungu. Wakati huo watu wanasema alikuwa hivi na vile, huna tena ule moto wa kumtumikia Mungu au huna kabisa ule moto wa kuutafuta uso wa Mungu.

Wanayosema watu sio kwamba ni uongo, moyo wako unakushuhudia kabisa ndani yako umekaukiwa kabisa kiroho. Hata ukirajibu kujitutumua unaojiona unajilazimisha tu, ila ndani yako unaona hakuna kabisa ile chemichemi ya kiMungu kama ilivyokuwa zamani.

Sio lazima ujue haya mazingira ya kukurudisha nyuma, vinaanza vitu vidogo vidogo sana ambavyo mwanzoni unaweza kuona ni vya kawaida. Lakini kwa jinsi vinavyozidi kujenga mizizi ndani yako, ndivyo vinavyozidi kukupoteza. Na sasa hivi kuna kelele nyingi sana, ambapo usipokuwa makini na usipokuwa na chujio la kuchuja taarifa, utajikuta mtu wa kutangatanga huku na kule.

Nakueleza haya ili uwe makini na uchukue tahadhari mapema, uache kutawaliwa na matukio mabaya kiasi kwamba yanachukua nafasi ya Mungu ndani yako. Haijalishi jambo gani limeujeruhi moyo wako, hupaswi kuacha kumtumikia Mungu kwenye nafasi yako aliyokupa.

Hatuwezi kuacha kusoma Neno la Mungu kwa sababu kuna jambo lilitupata mwaka uliopita, basi limekuwa ndio sababu kwetu. Hilo limepita na maisha yanaendelea, mwingine mahusiano yalivunjika miezi iliyopita mpaka leo anasema bado hayupo vizuri. Ndugu unahitaji maombi tena unapaswa kuombewa haswa, yaani mchumba amekufanya uache kuutafuta uso wa Mungu!

Hatuwezi kurudishwa nyuma na vitu vya kupita, hakuna kitu kipya, kama ni msiba hata wewe utakufa, kama ni hasara hakuna bishara inayodumu milele. Chochote unachokiona leo hakitakuwezo miaka 100 ijayo, haijalishi unakipenda sana jua hivyo hakitakuwepo. Cha kuumiza zaidi hata wewe hutakuwepo kipindi hicho.

Hatozuia kuumizwa ila utaporuhusu yale maumivu kuwa ndio nyumba yako ya kuishi, huo ni uamzi hatari sana. Tuache Changamoto zipite kwa namna ambayo zitatupata, tuwe makini sana zisiwe chanzo cha sisi kuacha mambo ya msingi.

Haijulikani kesho utapatwa na changamoto gani, ila hakikisha hiyo Changamoto haikuondoi kwenye mpango wa kusoma Neno la Mungu. Acha hilo jambo likuumize hata wiki, ila liambie kabisa hilo tatizo upo imara, wiki inayofuata endelea na juhudi zako.

Umekosa wa kukutia moyo au wa kukufariji, yupo Roho Mtakatifu atakufariji, usikae na jambo moyoni likakunyanyasa kiasi kwamba unageuka kero hata wengine.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Kwa masomo mazuri zaidi endelea kufuatilia,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com