Kabla Ya Kuonekana Kwa Wengine Tumepoteza Mwelekeo, Huwa Kuna Dalili Fulani Tunaanza Kuziona Kwetu Ila Huwa Tunazipuuza.
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona tena leo. Sifa na shukrani tumrudishie yeye kwa wema wake mkuu anaoendelea kututendea wanadamu wote, wapo hawakustahili kuishi, ila leo wamepewa nafasi nyingine ya kutubu makosa yao.
Kila mmoja anaelewa alipoanzisha uzembe wake fulani ukamgharimu maisha yake, mwingine kilema alichonacho leo. Ilikuwa ni uzembe ambao alikuwa anapuuzia kwa kile alichokuwa anaona kabisa kinaenda kumsababishia ajali.
Huenda huo uzembe hakusabaisha yeye ila dereva aliyekuwa anaendesha gari/pikipiki ile alikosa umakini wakagongana na chombo kingine cha moto.
Kabla ya mtu yeyote kuona ulivyopoteana kwa kile ulichokuwa na bidii nacho, kuna vitabia fulani vya kupotea kwako huwa vinajitokeza kwanza kwako. Lakini huwa tunavipuuza na kuendelea na mambo yetu, huku zile tabia zikiendelea kukua na kujenga mizizi imara ndani yetu.
Tunapoendelea kuziacha tabia fulani za kutuvuta nyuma zikue ndani yetu, tabia zile huzaa matokeo mabaya sana. Ambapo matokeo yake ya mambo tuliyoyapuuza huonekana zaidi kwa marafiki zetu na wote wanaotuzunguka. Ndio maana unaanza kusikia huyu ndugu alikuwa vizuri sana kipindi cha nyuma, ila sasa amepoteana kabisa.
Kama ni bidii yako ya kufanya kazi kupungua kazini kwako, huwa unaanza kuiona wewe kabla ya boss wako kuiona na kukuambia. Kama ni upendo kupungua kwa mke/mume wako, huwa unaanza kuona wewe mwenyewe kabla ya mke/mume wako kuanza kukulalamikia siku hizi humpendi.
Ikiwa ni kwenye masomo yako, kabla mwalimu wako hajakusemesha Chochote, huwa unaona wewe kwanza uzembe ulioanzisha utakupeleka pa baya. Ila wakati huo unaweza ukapuuza ila baadaye unaona matokeo mabaya zaidi ya yale uliyoona mwenyewe.
Kama ni nidhamu yako imepungua kwenye matumizi yako ya fedha, unaanza kuona wewe kabla watu wa nje hawajakuona na kuanza kukusema kuhusu tabia yako mbaya.
Kama ni utapeli wa kuchukua pesa za marafiki zako, ukiwadanganya utarudisha na wakati moyoni mwako unajua kabisa hutorudisha. Huwa kunaanza ndani mwako kabla hujawa na kesi nyingi za kuwachukulia watu pesa zao.
Kama ni kushuka kiwango chako cha maombi, huwa unaanza kuona mwenyewe kabla ya mtu yeyote kukuona kuwa huyu sio yule wa mwaka jana au mwaka juzi au wa miaka mitano iliyopita.
Ndivyo ilivyo hata katika usomaji wa Neno la Mungu, haitokei siku moja mtu akapoteza bidii yake ya kusoma neno la Mungu. Huwa inaanza tabia kidogo kidogo ndani yake, ule uzembe anaoona mtu ndani yake bila kuuchukulia hatua za haraka, ndio unaozaa matokeo makubwa mabaya.
Usifikiri huwa inatokea tu unamwona mtu yupo vizuri kiroho ukafikiri yeye mwenyewe hakujua hilo. Huwa mtu mwenyewe anaona kabisa zile bidii na kiu ya kumtafuta Mungu, ndio imezaa matokea makubwa mazuri ambayo kila mtu anatamani kuwa kama yeye.
Matokeo mazuri mnayoona leo kwa mtu fulani, ana taarifa yake mhusika, matokeo mabaya mnayoona kwa mtu leo, ana taarifa yake jinsi alivyoanza kulea tabia fulani iliyompelekea kufika hapo alipo.
Usipochunga mwenendo wako vizuri uwe na uhakika adui atakuondolea bidii yako ya kuutafuta uso wa Mungu. Kinachoondoa bidii yako sio kitu kikubwa sana kwa jinsi ya mwili, ila kwa jinsi ya rohoni ina maana kubwa sana.
Vile vitabia vibaya vibaya unavyovipuuza leo, ule uzembe uzembe unaoulea leo, ule utani utani kwa mambo ya Mungu unaouchekea leo, ipo siku utajutia kwanini uliruhusu vitu kama vile kukutawala.
Usisubiri tabia mbaya ikue ndani yako ndio uanze kuchukua hatua, unajijua mwenyewe. Unaona kitu hakipo sawa na kinaenda kukuondoa Kwenye mstari wa kiMungu, fanya upesi kuchukua hatua. Usisubiri tangazo kutoka kwa mchungaji, usisubiri kukemewa au kuonywa au kukumbushwa. Wewe mwenyewe bila kusukumwa na mtu yeyote, kataa hali hiyo mbaya inayokupelekea upotevuni.
Unaona bidii yako ya kusoma Neno la Mungu inashuka siku hadi siku, chukua hatua mapema ya kuondoa makosa yote madogo madogo yanayosababisha uwe mzembe. Nakwambia utabaki umesimama kila siku, watu watusubiri sana urudi nyuma na hutorudi nyuma.
Tabia ya kujitathimini kwa kila unachokifanya ni njema sana, uzuri kwa kila jambo unaloanza kulifanya. Huwa tunaanza kulifanya kwa hamasa kubwa na bidii nyingi sana. Baadaye jinsi tunavyozidi kukutana na changamoto kwa kile tunachofanya, ile bidii ya mwanzo huondoka taratibu taratibu, na mwisho bidii ile huondoka kabisa.
Ili usifike sehemu ukaanguka kabisa, fanyia kazi zile tabia mbaya unazoona zinajitokeza kwako. Usiseme haina shida utafanyia kazi kesho, hujui ya kesho yataongezeka yapi mapya. Leo ni mhimu sana kuliko kuisubiri kesho usiyoijua.
Bila shaka kuna kitu umejifunza, nami nina imani kuna somo umeondoka nalo la kukusaidia katika safari yako ya wokovu, fanyia kazi yale umejifunza.
Mungu akubariki sana kwa muda wako, usiache kutembelea mtandao wetu kwa masomo mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com