Tabia Ya Kujihalalisha Baadhi Ya Vitu Ni Kufikiri Tunampendeza Mungu Kumbe Tunamchukiza.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Tuliopata kibali cha kuiona leo, tunapaswa kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Siku hizi bwana wakristo tunataka kuokoka kuliko Yesu Kristo mwenyewe, tukifikiri tunampendeza Mungu wetu kumbe tunaleta chukizo mbele zake. Tunafanya mambo ambayo mpaka shetani mwenyewe anatushangaa kwa jinsi tunavyofanya.

Yule mtu unayesema hana shida kwako, yeye mwenyewe anaona una shida kwake tena ni kikwazo kikubwa sana kwenye mambo yake. Usifikiri mchawi anaweza kukupenda kwa jinsi unavyomharibia kazi zake kupitia maombi yako, kwa sababu wote ni mmeumbwa na Mungu mmoja.

Adui yako ni adui yako tu, hata kama usimfanyie baya na hata kama usimchukie kwa jinsi Neno la Mungu linavyotuelekeza tusifanye hivyo. Na kweli hatupaswi kujenga chuki na maadui zetu, na wale wanaotutendea mabaya, na wale wanaotunenea mabaya juu yetu. Bali tunapaswa kuwaombea na kuwatendea mema.

Hatuwezi kung’ing’aniza kukaa na watu ambao tunajua kabisa zipo tabia mbaya wanatuambukiza, alafu sisi tukaona haina shida kabisa kwa sababu sisi tumeokoka. Wapo wengi wamerudi nyuma kiroho kwa kujidanganya hivyo, wanaofanya hivi kuketi na watu fulani wa makundi mabaya, ni wale wenye kazi zao maalum. Wale wenye kazi maalum inayowapelekea wawe pamoja na hao watu, na kiwango chao cha upeo kipo juu sana.

Inakuwaje unajiingiza kwenye makundi ambayo kila kona unakuwa unaambatana nayo hata kwenye kufanya mabaya yao. Huku unasingizia Yesu Kristo alikaa na walevi, wazinzi na wote watenda mabaya, kweli alikaa nao mbona yeye hakubadilishwa tabia akawa mzinzi/mwasherati, mbona yeye hakuingizwa kwenye ulevi/wizi.

Tunapenda sana kujihatarisha maisha yetu wenyewe, kwa mambo ambayo tayari Neno la Mungu lilishakataza kabisa. Lakini kwa kutojua na kukutana na wapotoshwaji wenye kutumia mwanya wa kutokujua kwetu, tunajikuta tumeingizwa kwenye dhambi kirahisi sana.

Hebu turejee hili andiko tuone linasemaje;
*Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Zaburi 1:1 SUV.*

Ukisoma biblia nyingine ya *Habari Njema* inasema hivi;
*Heri mtu asiyefuata shauri la waovu, asiyeshiriki njia za wenye dhambi, wala kujumuika na wenye dharau; Zaburi 1:1 BHND.*

Maneno ni yaleyale ya biblia ila hii imefafanua zaidi kwa kiswahili rahisi ambacho unaweza kuelewa vizuri zaidi. Nimekupa hiyo mistari uweze kuona neno la Mungu linasema nini kuhusu makundi fulani yenye tabia fulani mbaya. Bila shaka umejionea mwenyewe, sasa unapofika hatua unaanza kujihalalishia marafiki ambao wapo kinyume na imani yako, ujue umeamua kufuata njia ya upotevuni.

Kutokujua kwetu Neno la Mungu inatufanya tuone tupo sawa hata kuabudu nyumba yeyote ya ibada wanayomwabudu mungu wao. Tunafanya hivyo kwa mwavuli wa Mungu wetu ni mmoja, ikiwa Mungu wetu ni mmoja mbona hawataki kabisa kumsikia Yesu wako, wala hawataki kusikia ukiingiza ukristo wako kwenye mabaraza yao mnapoketi.

Hakuna muuza pombe yeyote atakayekupa kibali cha kuingia kwenye sehemu yake ya kuuzia pombe, ili uwahubirie watu habari njema za Yesu Kristo waache kunywa pombe. Akiwepo huyu mtu atakuwa sio mfanyabiashara wa hicho kileo.

Cheka na ndugu yako mwenye imani tofauti, lala na rafiki/ndugu yako kitanda kimoja mwenye imani tofauti na yako, fanya biashara na watu wasiomjua hata Kristo. Ila mtakapofika eneo la imani, hapo hakuna kuchangamana ndugu.

Keti na ndugu/rafiki zako kwa sababu maalum za kikazi au kimasomo au kibiashara, ila sio kwa kujumuika pamoja kwa mambo yasiyofaa. Kama vile kufanya starehe za pombe na wanawake/wanaume, au kuongea maneno machafu yasiyofaa kabisa katika imani yako.

Hebu tujikumbushe haya maandiko Matakatifu ambayo unayo kwenye biblia yako huenda ukanielewa zaidi;

*Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya. Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako. Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu. Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya jeuri. Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ingaayo, Ikizidi kungaa hata mchana mkamilifu. Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho. MIT. 4:14‭-‬19 SUV.*

Kama umepita haraka kwenye maandiko hayo ya kitabu cha Mithali naomba uyarudie tena na tena, umeona hapo, mtu mwovu lazima ahakikishe amemwangusha mwingine kwenye uovu wake maana ule mstari 16 unasema hivi;
*Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu. MIT. 4:16 SUV.*

Hebu tafakari hapo👆🏽uelewe ninachokisema hapa, wengi tunapenda kufanya vitu kwa kushindwa kujua haya. Ndio maana tunahimizana kusoma Neno la Mungu. Uwezekano upo hayo maandiko hukuwahi kufikiri kama yameandikwa kwenye biblia yako.

Sawa na kijana anasema ameachana na mchumba wake alafu bado anaendeleza mawasiliano yaleyale yenye kuambatana kabisa na watu waliopo ndani ya mahusiano ya uchumba. Uwe na uhakika kabisa ukiingia kwenye mahusiano na mtu wa namna hii, atakuumiza moyo wako kwa kukuacha au kuwaunganisha wawili kwenye mahusiano, ukifikiri nakutania uliza ndoa za namna hii.

Unapoambiwa mjue sana MUNGU uwe na amani na watu wote bila kujichanganya na vitu fulani vya ovyo, usifikiri unanyimwa uhuru wa kujitanua na marafiki zako. Neno la Mungu limekuwekea mipaka ya wewe kuishi na watu wote vizuri bila kumchanganya na miungu mingine.

Kutokusoma neno la Mungu ni hasara kwako wala sio ya mchungaji wako, ndio maana unasikia tangazo la kila siku watumishi wakikuhimiza umhimu wa kusoma Neno la Mungu.

Mungu afungue ufahamu wako ili akili zako ziweze kufikiri ipasavyo.

Endelea kutembelea ukurusa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com