Moyo Wako Una Amani Kwa Unachotaka Kusema au Kufanya Hicho Kitu?
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tunamrudishia yeye kwa uweza na nguvu zake.
Kuna vitu unaweza kuvifanya katika mazingira yale yale ya kila siku vikawafanya watu wakaumia mioyo yao, na wakati mwingine katika mazingira yaleyale vitu vilivyofanya vikawaumiza mioyo yao. Unaweza kuvifanya katika mazingira yale yale vikawaletea furaha na vicheko.
Unapokuwa na Neno la Mungu ndani yako unamrahisishia Roho Mtakatifu kufanya kazi yake kwa urahisi na wewe. Utakuwa mwepesi wa kubadili mazungumzo ambayo unaona kabisa ndani yako umekosa amani ghafla, au kabla hujalisema hilo jambo utasikia ulimi mzito na moyoni unakosa amani ghafla. Ujue hiyo sio hali ya kawaida, hilo ni zuio halali la Roho Mtakatifu au alarm ya kukujulisha shetani amekasirika kwa unavyotoa siri zake.
Najua umewahi kukutana na hali kama hii, mtu anayechekesha watu na kuingiza utani kwenye vitu fulani. Kuna mazingira hawezi kufanya hivyo na watu wanakuwa hawahitaji huo utani, wakati huo wanahitaji vitu siriaz. Sasa kama mtu yule asipoelewa hilo akaingiza utani wake wa vichekesho uwe na uhakika atageuka mshangao usio wa kawaida kwa watu.
Hajalishi unaongea au unafanya jambo fulani, kuna mazingira utafika huwezi kwenda kama ulivyozoea wewe kwenda. Ipo mipaka unapaswa kuijua unapofika eneo lolote lile, ipo mipaka ya kuongea na ipo mipaka ya kufanya/kutenda.
Wengi wanafikiri jinsi wanavyoongea na familia zao ndani, wanaweza kuongea vilevile kwenye familia zingine. Ni sawa unaweza kufanya hivyo ila sio kila mazingira yatakuruhusu kufanya hivyo. Kila familia ina utaratibu wake, huenda wewe umezoea kusema na mzazi wako kama rafiki yako, ila wazazi wengine huwezi kusema nao hivyo watasema una dharau.
Wengi wetu tunakuja kukosea eneo hili, kwa kushindwa kusikiliza mazingira yanatuhitaji kufanya nini kwa wakati huo. Unaweza kufikiri umewafurahisha watu kumbe umewakera kiasi kwamba umesababisha wamefuta furaha yote waliyokuja nayo. Na wakafanya kosa ya kukushusha heshima yako, na kukuona huna adabu, ambapo mara nyingi mambo kama haya hutokea wakati una hasira, na wewe unakuwa huna hasira lakini umefanya.
Hata ukitaka kuzungumza na mtu chunguza kwanza amani ya moyo wako kile unachotaka kusema kama unajisikia amani. Ukiona unasitasita kusema ujue kuna mambo mawili; la kwanza una hofu na la pili unachotaka kusema kwa mtu/watu hawapo tayari kukipokea.
Ukizungumza kitu ambacho watu hawataki kukisikia kwa wakati huo, uwe na uhakika Mungu amesema na wewe na amekupa kibali useme tu hata kama hawataki. Ila kama utajisikia kukosa amani moyoni mwako kabisa na ukasikia kengele ya hatari ndani yako, ni vyema kusitisha hilo jambo haraka.
Usifikiri unavyozidi kuliweka neno la Mungu ndani yako litakusaidia tu kujua mambo fulani kiroho tu. Neno linakupa hekima na busara namna ya kuzungumza kwa mazingira husika. Labda nitolee mfano huu utanielewa zaidi; unaweza kufika mahali ukajitambulisha kwa kutaja jina la dhehebu/dini yako ukawa kikwazo kwa watu. Na unaweza kufika mahali ukataja dhehebu/dini yako watu wakafurahia na kujisikia vizuri, umeelewa hapo.
Unaweza kufika mahali kuzungumza na vijana wakakufurahia sana, ila mazungumzo yaleyale ukizungumza mbele ya wazazi wao watakuchukia. Sijui kama unanipata msomaji wangu, nataka uelewe vitu fulani namna moyo wako unavyoweza kukuongoza katika mazingira fulani.
Usikariri eneo lolote lile, kusoma mazingira moyo wako utakusaidia, maana unaweza kuwa shapu/mwepesi wa kufanya vitu na watu wakawa wanakufurahia sana. Ila ukafika sehemu nyingine wakakuona una kiherehere, sasa kama huna uwezo wa kutambua kosa haraka kwa kuwatazama watu na mazingira, unaweza kuendelea kuharibu zaidi.
Haijalishi upo vipi, jenga utaratibu wa kusikiliza Mungu anasema nini kupitia moyo wako, ukiona hali yeyote kwa kile unachotaka kufanya. Usiwe na haraka jirudi haraka kuangalia kuna usalama au kuna vitu unazuiliwa kusema/kufanya.
Uelewe pia yapo mazingira utafanya jambo watu wasikuelewe sana ila moyoni mwako ukawa na amani na msukumo wa kufanya hivyo. Hilo halina shida, ninachosema hapa ni ile kusikia zuio la moyo wako usiseme. Hata kama ulikuwa unataka kusema jambo nyeti kiasi gani la kuwasaidia watu, kaa kimya.
Penda kusoma biblia yako, itakufundisha hata namna ya kuketi mahali pa ugenini na sio kuzungumza tu. Unaweza kuwa ulikuwa unaona kawaida katika hili la kusoma Neno la Mungu, ila sasa utakuwa umepata mwanga kiasi fulani.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com