Umetangaza Wewe Ni Mwana Wa Nuru, Hawategemei Kukuona Unafanya Mambo Ya Wana Wa Giza.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya Bwana ametupa kibali cha kuiona leo. Sifa na utukufu anaye yeye Yesu Kristo, maana fadhili zake ni kuu kwetu sisi wanadamu.
Karibu sana tushirikishane maneno machache ya kutusaidia katika safari yetu ya usomaji neno la Mungu. Tunaposoma Neno la Mungu, kuna maeneo mengi sana tunaonywa na kufundishwa namna ya kuishi maisha ya kumpendeza yeye.
Neno la Mungu halitusaidii tu mambo ya rohoni, linatupa pia ufahamu mzuri wa kuweza kuishi maisha ya kimwili pasipo kumtenda dhambi Mungu. Hatuwi tu wa rohoni sanaa, hata mwilini tunakuwa vizuri maana tunaongozwa na Roho wa Mungu.
Unapojiita mkristo na kutangaza wewe umeokoka, ujue umetangaza jambo ambalo linakufanya kila mtu aweke masikio na macho yake kwako. Kila mtu anajua sifa ya mtu aliyeokoka, haijalishi mtu yule ameokoka au hajaokoka, wanajua mtu aliyeokoka ana mipaka yake ambayo haifanani na wao wasiomjua Kristo.
Umewahi kufika mahali mpo kikundi cha watu mchanganyiko, yaani wanaomwamini Kristo na wasiomwamini. Lakini unashangaa wewe unapewa nafasi ya kuomba Mungu kwa ajili ya chakula au kuombea safari, sio kwamba umejitokeza mwenyewe wanakuteua wenyewe ombea safari/chakula.
Wanajua kabisa mtu aliyeokoka hawezi kutegemea nguvu zingine za miungu mingine zaidi ya Yesu Kristo, wanajua kabisa aliyeokoka hawezi kufanya jambo la kipuuzi kama wao wasiokoka. Sasa itawashangaza pale utakapopata matatizo magumu unaanza kusema utaenda kwa bibi/babu fulani kukurekebishia mambo yako yaende vizuri.
Unakuta mkristo kabisa anasema humjui bibi/babu yangu wewe, akiwa na maana anaenda kumloga mwenzake kwa kosa alilomfanyia. Au mwingine anapata kushawishiwa na wenzake afanye jambo la namna ile kwa kwenda kwa waganga wa kienyeji.
Kuna mambo kama mkristo hupaswi kuonekana unashindwa, hupaswi kufanana na mtu asiye na Yesu Kristo moyoni. Sawa na watu wanalalamika kuingia kwenye ndoa ni sawa na kujipeleka gereza la mateso, anaenda mbali zaidi mtu yule kusema bora kutokuoa/kuolewa uwe huru kufanya mambo yako. Ukihitaji mtoto utafuta mtu wa kumzalisha au kuzaa naye ukapata mtoto, na wewe tunayetegemea umeokoka unajiunga na hilo kundi lililopotea njia.
Mtu aliyeshiba Neno la Mungu hana mashaka na Yesu wake, watu watazungumza weee jambo fulani la kushindwa. Lakini wewe utakuwa na uhakika wa kupeleka hitaji lako kwa Baba yako anayehusika na mambo yote kwako.
Utofauti wako sio kuitwa jina zuri la watu wanaomjua Kristo, utofauti wako wa kukutambulisha umeokoka ni matendo yako mema yanayofanana na mkristo mwenye safari. Sio unapatwa na tatizo kidogo unaanza kushawishika kunywa pombe utulize mawazo, hayo sio mawazo ya mtu aliye nuruni, ni mawazo ya mtu aliye gizani.
Mtu aliyekomaa kiroho hawezi kufanya kitu cha kipuuzi alafu asijisikie vibaya moyoni mwake, tena sifa ya mtu aliye wa nuruni ukimwonya anaonyeka haraka sana. Tena akisikia imeandikwa mstari fulani mtu asiwe hivi na vile, anaumia sana na kutubu haraka.
Mtu aliye na Yesu Kristo moyoni na sio mdomoni tu, huwezi kusumbuana naye kwenye mavazi. Haipo ndugu, we chunguza mwenyewe vizuri, wote wanajua tabia ya mkristo aliyeokoka anapaswa kuwaje. Roho Mtakatifu aliye ndani yangu ni yule yule aliye ndani yako, haiwezekani ukawa kwazo kwa mavazi yako kwa wengine Alafu wewe ukawa unaona sawa tu.
Utasema wanasumbuliwa na ushamba wao tu, kweli wanaweza kuwa wana utamaduni wao ambao wanajua anayevaa mavazi fulani ni asiyemjua Kristo na wanaovaa mavazi fulani ni wale wanaojiheshimu na kumjua Kristo. Ila fahamu kwamba jambo linalofanyika kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, haliwezi kuwaingiza wengine majaribuni. Nguo yako mama/dada isingewapa watu shida kama ingekuwa na maadili, huenda nguo uliyopaswa kumvalia mume wako ndani wewe unaivaa nje.
Nakupa mifano mbalimbali kuweza kufahamu na kujitofautisha na wenzako wasiomjua Kristo wanavyokutazama wewe. Jinsi watu wanavyokutazama unapaswa kumtangaza Yesu wako vile vile, ukienda kinyume ujue una haribu ushuhuda.
Soma Neno la Mungu likusaidie wewe na wengine ambao bado wameokoka lakini bado wanafanya vitu kama watu wasiomjua Kristo. Ukomavu wako kiroho unakusaidia zaidi kuonyesha wakati watu wanawaza hasi wewe unakuwa unawaza chanya. Maana unajua uliye naye ni mkuu sana, anaweza kubadili chochote kwenye mazingira yeyote magumu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com