Kinachokufanya Usimpe Mungu Muda Wako Ujue Ipo Siku Hicho Kitu Kitaondoka/Kitaharibika.
Tumsifu Yesu Kristo mwana wa Mungu, siku nyingine tena ya ijumaa kuu tukimwazimisha Yesu Kristo kwa kukumbuka mateso yake kwa ajili yetu sisi wanadamu.
Tumekuwa tukisongwa na shughuli nyingi za kila siku kiasi kwamba tunakosa muda kabisa wa kusoma Neno la Mungu na wakati mwingine kushindwa kabisa hata kupata muda wa kuomba. Wengine wanafika hadi hatua ya kushindwa kabisa kwenda kanisani kujumuika pamoja na wenzao katika kumwabudu Mungu.
Kweli zipo shughuli zinatubana kiasi kwamba unatamani kwenda kanisani Lakini unashindwa kutokana na kazi anazokupa mwajiri wako. Na wengine wana shughuli zao binafsi ila wanaona tabu kutoa muda kwa ajili ya Bwana wao.
Kuna wakati nilifanya kazi na mtu fulani mwenye kampuni yake, kama miaka mitatu iliyopita, wakati nasaini mkataba wa kazi. Niliona kufanya kazi ni mpaka jpili, kwanza nilitulia na kumwambia kama ni kufanya kazi mpaka jpili sitaweza kufanya kazi na wewe.
Ukweli nilikuwa nahitaji ile kazi ila niliona inataka kunibana mpaka nisiweze kwenda kanisani, huyo ndugu alivyoona nimesimamia msimamo wangu ilimbidi na yeye abadili maamzi. Pamoja na mimi nilikuwa nahitaji hiyo kazi, na yeye alikuwa ananihitaji sana nifanye naye kazi, basi kila mmoja alitumia nafasi yake kutetea upande wake.
Kazi yeyote inayoninyima uhuru wa kumwabudu Mungu wangu, hiyo sio rafiki kwangu labda itokee tu dharura ambayo nakuwa sina namna ya kuikwepa kutokana na sababu maalum. Ila sio nibanwe kila siku ili nisiweze kwenda kanisani.
Mungu wetu ni wa mhimu sana kuliko vitu vingine vyote, tunapaswa kuwa na kiasi katika shughuli zetu. Ikiwa unaona biashara yako ni ya mhimu sana kuliko Mungu, ujue umepotea, ukiwa unaona kazi yako ni ya mhimu sana kuliko Mungu, ujue umepoteza.
Uwe na kazi nzuri sana inayokulipa mamilioni ya fedha, ipo siku hutokuwa na hiyo kazi, uwe na biashara nzuri sana inayokupa matrilioni ya fedha uwe na uhakika hiyo biashara haitadumu milele.
Leo unaweza kulala una kazi nzuri inayoweza kuhudumia kila eneo la maisha yako, ila ukaamka kesho huna hiyo kazi. Leo unaweza kulala billionaire, kesho ukaamka huna kitu. Hii ipo na ndio maana unasikia tajiri fulani amejinyonga au amejipiga risasi, ni kwa sababu waliwekeza kwenye vitu vya nje kuliko kuwekeza na ndani yao.
Unahitajika sana kutoa muda wako kwa ajili ya Mungu wako, ikiwa una biashara yako hakikisha inapofika muda wa kwenda ibadani toa saa moja au masaa mawili kwa ajili ya Bwana. Hakuna hasara kwa hili, ndio maana wale wanaomjua Mungu wao vizuri huwa hawana shida kwa hili.
Tukiachana na hayo ya kanisani, turudi sasa kwenye kusoma Neno la Mungu, hapa hahitaji kwenda kanisani wala kwenda sehemu nyingine. Ni suala la wewe binafsi kutoa muda wako kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu, hakuna kisingizio hapa.
Wengi tunaweka vipaombele sana kwa vitu vya kupotea kama nilivyokueleza kwenye mifano ya kazi na biashara hapo juu. Vtu vyote ulivyonavyo leo vinaweza kuondoka ukabaki kama ulivyozaliwa, ndio hapo unapoona mtu anahangaika na kutafuta kuombewa, wakati yupo vizuri alikuwa hataki hata kusikia habari za Yesu Kristo.
Sio vibaya kutafuta msaada wa maombi ila kwanini wakati huna shida hutaki kumpa Mungu muda wako? Hichi ndicho cha kujihoji mwenyewe, kwanini unafikiri Mungu wetu ni wa kukumbuka wakati unahitaji mke/mume au wakati unapita kwenye moto wa majaribu.
Wengi tumepotea eneo hili, tunaanza kuwa siriaz na Mungu tukifika wakati tunataka kuoa/kuolewa, hapo utamwona mkaka/mdada yupo bize kweli na Mungu. Ila akishampata tu aliyekuwa anamhitaji anaacha na kumtegemea Mungu, wakishaenda kwa siku kadhaa ikitokea wameachana ndio anakumbuka tena kama huwa kuna Mungu.
Kila jambo la kimwili linakuja na kuondoka, ukiwekeza sana kwenye vitu vya kimwili pasipo kuwekeza na vitu vya rohoni. Uwe na uhakika ipo siku utahitaji msaada wa kiMungu, na wakati huo utaona kama umetengwa na kila mtu.
Unapendwa sasa hivi na hao ndugu, marafiki, mke, mume kwa sababu una pesa au kazi nzuri. Siku vimepotea hivyo vitu uwe na uhakika unaweza asiwepo hata mmoja wa kukutia moyo katika mapito yako. Zaidi utabaki na Mungu wako, sasa iwe ulikuwa huna mpango naye, hapo utafanya kazi mbili kwa wakati mmoja. Kwanza utapaswa kutengeneza mahusiano yako na Mungu wako huku ukipita katika upweke, na pili utapaswa kutumia Neno la Mungu likusaidie wakati huo huna hata mstari mmoja.
Pesa zako zisikupe kiburi cha kuona kila kitu kitaendeshwa na hizo pesa, elewa kuna wakati hupotea kabisa hizo pesa, furaha na Upendo wa familia yako usikupe kiburi cha kupuuza mambo ya Mungu. Upo wakati upendo ule utakauka na hutoelewa nini kimetokea, kama hukuwa na muda na Mungu utateseka sana.
Wekeza muda wako na Mungu, tengeneza mahusiano yako na Mungu kila inapoitwa leo. Usiwe na tabia za kuona Mungu ni wa zaida sana, toa muda wako kusoma Neno lake kwa bidii. Haijalishi watu wanakuona vipi, tenga saa moja kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu na kulitafakari.
Ukilijua Neno la Mungu hakuna atakayekulazimisha kutoa sadaka, hakuna atakayekulazimisha kuomba Mungu, hakuna atakayekusukuma kujitoa kwa ajili ya kusapoti kazi ya Mungu. Kila eneo la maisha yako litakuwa salama kwa sababu lipo Neno la Mungu linakuongoza kufanya jambo kwa wakati husika.
Sijui sana kama unanielewa ninachokuambia hapa, huenda hapo ulipo mambo yako safi sana na uhakika upo wa kula na kunywa. Unaweza kusema nimekosa kitu cha kukuambia, ila nakwambia toa muda wako kusoma Neno la Mungu, utavuna vitu ambavyo hukuwahi kuvivuna.
Haitajalisha kesho tutaamka hatuna kazi, hatuna watoto, hatuna wazazi, hatuna mke/mume, hatuna vile vitu tulivyovitegemea katika maisha yetu. Bado tutakuwa na BABA yetu mwenye vyote, yeye hatatuacha wala kututenga kwa sababu ya magonjwa yaliyoshindikana kwa madaktari, wala hatatuacha kwa sababu hatuna kazi.
Soma Neno la Mungu ukue kiroho uweze kufanya huduma yako vyema, uweze kuishi maisha ya wokovu, uweze kuenenda sawasawa na mapenzi ya Mungu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com