Litazame Neno La Mungu Kwa Mtazamo Wa Juu Sana Unapolisoma.
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana anaendelea kutupa kibali cha kuendelea kuwepo hai mpaka leo. Sio kwa bahati mimi na wewe kuifikia leo, lipo kusudi la Mungu kukupa nafasi kama hii ufanye jambo jema kwake.
Tunaweza kulichukulia Neno la Mungu ni jambo la kawaida sana, ndio maana wakati mwingine mtu anaambiwa jenga utaratibu wa kusoma Neno la Mungu anaona kama vile mateso.
Ukijua umhimu wa jambo lolote lile hutofanya utani katika jambo hilo, kinachotukwamisha wengi ni ukawaida wa Neno la Mungu. Unaweza kuona mateso, na unaweza kuona unasumbuliwa, na unaweza kuona usumbufu kushikashika biblia kwa sababu hujajua umhimu wake.
Lakini tukifika hatua tukajua umhimu wa sisi kuwa na Neno la kutosha mioyoni mwetu, tutaanza kulitafuta kwa bidii sana bila kuchoka. Bidii yetu ni ndogo kwa sababu ya uelewa wetu mdogo kuhusu Neno la Mungu.
Unaweza ukajiuliza neno la Mungu utalitumia wapi wakati wewe si mhubiri, si mwalimu, si mchungaji, wala si mwimbaji. Hoja yako inaweza ikawa sahihi kwa jinsi unavyofikiria, ila upo ukweli mkubwa sana kwenye Neno la Mungu.
Labda nikupe kisa kimoja kilichonikuta mimi mwenyewe siku tatu nyuma, kabla sijaendelea sana mbele, unaweza ukapata kitu cha kukusaidia kusonga mbele.
Juzi nilipoteza kiasi cha shilingi laki nne, ambacho hichi kiasi nilishakipangia bajeti zangu nyingi tu. Kinaweza kikaonekana ni kiasi kidogo sana ila kwangu kilikuwa ni kiasi kikubwa sana, mwanzoni sikuamini sana na nilipata mshangao fulani na mpaka sasa nakuja kuona kama nipo ndotoni ila ndio ukweli wenyewe.
Kibinadamu hili jambo lilinifedhehesha kiasi fulani, ila baada ya muda kidogo nilijisikia amani kubwa sana moyoni. Hii amani ilifanya utulivu wa moyo wangu kuwa kwa kiasi kikubwa sana, ambapo bila kukuambia ulikuwa huna uwezo wa kujua kama napita kwenye mawazo mazito.
Nguvu hii niliyoipata ya kuliona hili jambo ni la kawaida, ilitokana na Neno la Mungu, nasema ukweli pasipo Neno la Mungu ilikuwa ngumu kuniona naandika hizi kurasa za kila siku. Roho Mtakatifu amepata urahisi wa kunisaidia hili kwa sababu ya Neno la Mungu, vinginevyo ningeshindwa kufanya mambo ya msingi mpaka leo.
Ukiwa mfuatiliaji mzuri wa hizi jumbe ninazoandika humu, utakumbuka ukurasa wa 157 niliandika ujumbe ambao hata mwenyewe nilivyousoma. Nilijua kabisa ni ujumbe wangu mwenyewe, ulinitia moyo sana na kuona kwamba hatumtumikii Mungu kwa sababu ya vitu.
Kwanini nakueleza haya, sio kwamba mimi nayaweza sana mambo mazito kama haya, binafsi nahitaji msaada wa Mungu kama wewe. Nilichotaka ujifunze hapa ni kujua kwamba Neno la Mungu limechukua kila nafasi ya maisha yetu, upaswa kulijua hili kabisa.
Mungu anaweza kusema na sisi kwa urahisi sana tukiwa na Neno la Mungu mioyoni mwetu, Mungu anaweza kutuepusha na hatari iliyo mbele yetu kwa sababu tuna usikivu ndani yetu wa kusikia maelekezo anayotupa kupitia Neno lake.
Neno la Mungu linakupa kujua unayemwamini yupo vipi, Neno la Mungu linakupa uwezo wa kutambua unayemtumikia ana sifa zipi. Ukapomjua vizuri uliyenaye ni nani, nakwambia utatembea kwa ujasiri kiasi kwamba utaanza kuleta maswali kwa wasiomjua Kristo.
Kwa hiyo lichukulie Neno la Mungu kama sehemu ya maisha yako yote, popote ulipo sikia kupungukiwa na kitu kama hujasoma Neno la Mungu. Tafuta kila mbinu ikupe nafasi ya kusoma Neno la Mungu, nakwambia siku zote utajiona una amani moyoni.
Elimu na maarifa yanayopatikana kwenye Neno la Mungu, ni maarifa makubwa sana ya kukufanya usirudi nyuma kiroho kwa sababu ya changamoto fulani imekupata. Utalia kama mtu tu ila moyoni mwako utakuwa na tumaini la Mungu juu ya maisha yako.
Huhitaji pesa ndio uweze kufanikisha hili jambo, unahitaji kutoa muda wako ndio uweze kufanikiwa katika hili suala la kusoma Neno la Mungu. Visingizio vinakuja kwa sababu hujajua thamani inayopatikana ndani ya Neno la Mungu, unaweza kujitetea sana ila kama husomi biblia. Unapoteza vitu vingi sana ambavyo vingekusaidia kusonga mbele, huenda hapo ulipo upo njia panda kuhusu imani yako kwa sababu huna maarifa ya Neno la Mungu.
Unalitazama Neno la Mungu kwa sura ipi mpaka sasa? Najua umeongeza kitu ndani yako baada ya kusoma ujumbe huu. Husomi Neno la Mungu ili uwe na uwezo wa kuwajibu watu wengine maswali watakayokuuliza, hiyo ni ziada tu, lipo jambo kubwa zaidi juu yako.
Imarisha msingi wa imani yako kwa kusoma Neno la Mungu, bomoa msingi mbovu uliojengwa ndani yako kwa kuijua kweli ya Neno la Mungu mwenyewe.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com