Usiingize Mazoea Kwenye Mafanikio Madogo Uliyopata Bali Tumia Kile Kidogo Ulichokipata Kufikia Kikubwa Zaidi.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona tena. Kila mmoja anapaswa kumshukuru Mungu kwa fursa hii ya kuiona leo.

Ukiweka juhudi yako Kwenye jambo lolote lile pasipo kukata tamaa, lazima utaona mafanikio yake. Haijalishi yatakuja kwa taratibu sana na wala haijalishi yatachukua muda mrefu. Kinachoangaliwa ni yale matunda ya uvumilivu wako katika kufikia hapo ulipo.

Wengi tunapoona kuna matunda fulani tumepata kwa lile jambo tulilokuwa tunateseka nalo siku nyingi, huwa tunaanza kuridhika na kuacha ile bidii ya awali tuliyokuwa nayo. Unaweza usijione sana kama ulipo umeridhika na hali uliyonayo, ila unaweza kujiona kwenye bidii yako bado ni ileile au imepungua.

Bidii aliyokuwa nayo mtu wakati anamhitaji Mungu amsaidie Kwenye jambo fulani, anaweza asiwe nayo tena hiyo bidii baada ya kufanikiwa jambo lake. Kwa namna nyingine tunaweza kusema bidii yetu huwa inakuwa sana pale tunapotamani kufikia ngazi fulani.

Hatuwezi kuendelea kuishi maisha ya nyakati tulizokuwa nazo kwenye hali za chini, ila hatupaswi kuacha kuwa na bidii tuliyokuwa nayo mwanzo. Bidii haiondolewi na mafanikio yako kiroho au kimwili, wengi tumeshindwa kuelewa hili, kufanikiwa kwako sio tiketi ya kupunguza bidii.

Ukipunguza bidii na ukaanza kuwa mzembe kwa kile ulichokuwa unakifanya ujue unaanda mazingira ya kuanguka, na kuja kunyanyuka unahitaji Neema ya Mungu kukuinua tena.

Wengi walianza kwa tabu sana kusoma Neno la Mungu, mara nyingine alikuwa anasoma lakini kiwango chake cha uelewa kilikuwa kidogo sana. Ila alivyozidi kujifunza na kumwomba Mungu amsaidie kuelewa zaidi Neno lake, yalipoanza kuonekana mafanikio kwa kile alichokuwa anakihitaji. Badala ya kuongeza bidii zaidi, yeye anapunguza bidii yake.

Ukawaida huja kwa kiwango kidogo sana bila kuelewa, na ukawaida huu unaletwa pale unapojiona upo vizuri sana kimaandiko. Tunasahau kwamba tunapaswa kuwa na bidii
nyingi kila siku kujenga mahusiano yetu na Mungu.

Ulipo sasa tamani kumjua Mungu zaidi na zaidi, najua wapo ndio wanaanza wokovu sasa hivi, wanaweza kuwa wanatamani mambo mengi na bidii yao inaweza kuwa kubwa. Ila kama hawataweka mipango mizuri ya kuona kujifunza mambo ya Mungu ni kila siku, watajiona wamefika na ile bidii yao inaweza isiwepo kama awali.

Omba Mungu akupe roho ya unyenyekevu, hata unapoinuliwa na kulijua vizuri Neno lake, uwe na kiu ya kuendelea kuutafuta uso wa Mungu. Usione kuinuliwa kwako ndio mwisho wa mambo yote, bali huo ndio uwe mwanzo wako mwema wa kumsogelea Mungu zaidi.

Bidii uliyoanza nayo ya kusoma Neno la Mungu, hakikisha kila siku unaona jana ulikuwa na kiwango kidogo cha ufahamu. Ukiona hivyo kila siku hutakuwa na kiburi cha kuacha kusoma Neno la Mungu, bali utahitaji kuongeza muda wako zaidi wa kutafakari yale unayojifunza ndani ya biblia.

Tamani kufika ile hatua ya kuambukiza mwingine roho ya usomaji Neno la Mungu, watu wakikutazama watamani kuanza kujifunza Neno la Mungu kwa sababu unaonyesha una vitu vya pekee ndani yako. Upekee huo unaonekana kwa watu wengine, kwa sababu umetengenezwa na jinsi unavyosoma Neno la Mungu na kulitii hilo NENO.

Epuka sana tabia ya kuridhika mpaka unajisahau, usikubali kuishiwa ladha ya kusoma Neno la Mungu, popote ulipo unapokutwa na hali ya kukaukiwa kusoma Neno la Mungu. Omba Mungu akusaidie eneo hilo, hiyo sio hali ya kawaida usibaki unajifariji alafu unapoelekea unapotea.

Njia nyingine ya kuepuka kuwa katika kundi la mazoea, ni kujiona mhitaji kila wakati, ona unamhitaji kumjua Mungu zaidi ya ulivyo sasa. Ukijiona hivyo kila utakayemwona anamtafuta Mungu kwa bidii utatamani kuwa Karibu naye zaidi au kutamani kuambukizwa roho ya bidii aliyonayo.

Lakini ukikaukiwa mambo ya Mungu, utaona wale wenye bidii ya kusoma Neno la Mungu ni watu wasio na kazi za kufanya. Utaanza kuwaweka watu Kwenye makundi mbalimbali ilimradi tu ujitie moyo kuwa unachofanya ni sahihi.

Tamani kufanyika upya kiroho kila siku, kusudi la kuwa mwanafunzi anayependa kujifunza mambo ya Mungu. Sio udumae/ugote kwenye hatua fulani utakayofikia, bali unapaswa kuongezeka kiwango cha maarifa zaidi ndani yako.

Nasema hivi; mstari wa biblia uliosoma jana ukapata kitu cha kukusaidia, ukija kuusoma tena kesho upate kitu zaidi ya kile cha jana. Neno la Mungu ni lilelile ila jinsi unavyozidi kukaa nalo karibu ndivyo unavyozidi kulifahamu kwa kiwango alichotaka Mungu ulifahamu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, hakikisha pia unatoa muda wako kusoma Neno la Mungu.

Usisahau msingi wa maisha yako ni Neno la Mungu
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com