Hazina Njema Itakayokusaidia Nyakati Zote Ni Hii.

Asifiwe Yesu Kristo aliye hai wana wa Mungu, siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona tena leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye kwa matendo yake makuu kwetu sisi wanadamu, wengi waliitamani hii siku hawakuweza kuiona, ila mimi na wewe tupata fursa hii ya kuiona.

Tunaweza kufanya mambo mengi sana na makubwa kwa kutumia uwezo aliotupa Mungu, uwezo uliopo ndani yetu ni mkubwa sana wa kuweza kufanikisha mambo ambayo mengine dunia itajiuliza uliwezaje kuyafanya hayo.

Huenda hapo ulipo hata robo ya uwezo uliopo ndani yako bado hujautumia kabisa, na hii inaweza ikaletwa na jinsi unavyojitazama kwa unyonge na mazingira uliyonayo sasa.

Utajuaje sasa uwezo uliopo ndani yako ili uweze kuutumia vizuri muda wako, utajuaje uwezo uliopo ndani yako ili uweze kuutumia vizuri ujana wako, utajuaje sasa uwezo uliojificha ndani yako ili uweze kuutumia sasa mama/baba.

Moja ya maswali ambayo yanatutesa wengi sana, na huenda hata wale wanaozani wamefika hatua za juu za kutambua Kusudi lao, bado hawajaweza kulifanya kwa ufasaha ambao Mungu alitaka walifanye.

Huenda muda mwingi waliupoteza kwenye mambo ambayo hayakuwa ya msingi sana huko nyuma, ndio maana zamani ukisoma Vitabu vingi vya Neno la Mungu kwenye Agano la kale. Unaona wafalme wengi walianza kuongoza taifa la Israel wakiwa na miaka 7/8 na kuendelea zaidi.

Huwezi kuongoza wazee ukiwa ndani yako huna uwezo huo, kuna vitu vilikuwa vinawekezwa kwa watoto hawa mpaka wakawa na uwezo wa kurithi nafasi za baba zao za kifalme. Leo hii ukianza kutafuta vijana wanaomtumikia Mungu katika umri mdogo idadi yao inaweza isiwe kubwa sana, kutokana na kujiona bado wanao muda wa kutosha kufanya mambo yao yasiyofaa mbele za Mungu.

Mfalme Daudi wakati anaachia kiti chake cha kifalme, alimpa wosia mwanaye Suleiman atakayerithi kile kiti kwa maneno haya;

Rejea; Kisha Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Uwe hodari, mwenye moyo mkuu, ukatende hivyo; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu, Mungu wangu, yu pamoja nawe; yeye hatakupungukia wala kukuacha, hata itakapomalizika kazi yote ya huo utumishi wa nyumba ya Bwana. 1 Nyakati 28:20.

Moyo wa ushujaa unakujaje ikiwa hatumjui vizuri tunayemtumikia, tutawezaje kuzishinda hila za shetani ikiwa hatujui namna ya kumshinda. Hivi mtu anawezaje kuitumia silaha ikiwa haijui namna inavyotumika, kweli anajua inapiga, je atapigaje ikiwa hajajifunza?

Uhodari wetu unaletwa na Neno la Mungu, tuna ujasiri wa kumweleza adui yetu anachotaka kutudanganya Mungu amekataza kupitia Neno lake. Tutajuaje Mungu amekataza, lazima tutakuwa wasomaji wa Neno lake.

Uwezo mkubwa uliopo ndani yetu, unaiuliwa na kupikwa vizuri na Neno la Mungu, pasipo Neno la Mungu tunajidanganya bure. Hatuwezi kuenenda sawa sawa na mapenzi ya Mungu pasipo kuwa na Neno la Mungu.

Hatuwezi kujua Baba yetu anatutaka tuenende vipi pasipo kujua Neno la Mungu, huwezi kujipangia namna ya kuishi maisha unayotaka huku unasema wewe ni mwana wa Mungu. Neno linatuweka katika mstari ambao tunakuwa tofauti na wasiomjua Kristo.

Tutawezaje kuwa na nguvu ya kushinda dhambi ikiwa Neno la Mungu halipo ndani yetu, imani inajengwa na Neno la Mungu, ufahamu wa kiMungu ndani ya mwamini unajengwa na Neno la Mungu, utumishi mwema na unaompendeza Mungu unajengwa na msingi wa Neno la Mungu.

Karama/Vipawa vyetu Mungu alivyoweka ndani yetu ili tumtukuze yeye, vinajengeka vizuri ndani mwa mtu akiwa ana bidii ya kumjua Mungu. Hutokuwa na msukumo wa kujiombea ikiwa hujajua Neno la Mungu, hutokuwa na msukumo wa kujizuia kutenda dhambi ikiwa hutokuwa na Neno la Mungu.

Neno la Mungu limebeba kila eneo la maisha yako, husomi Neno la Mungu ili uwe na uwezo wa kubishana na mataifa wasiomjua Kristo. Unasoma Neno la Mungu kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, ambalo Neno limebeba maisha yako kiroho na kimwili.

Mahali ambapo unapaswa kuwekeza muda wako vizuri ni kwenye kusoma Neno la Mungu, yaani hupaswi kumaliza siku bila kusoma Neno la Mungu. Hakikisha hili jambo linaingia kwenye damu yako yaani huwezi kulala bila kushika biblia yako ukasoma angalau mlango mmoja.

Utaratibu huu ukiujenga vizuri utawaambukiza na watoto wako, utawaambukiza na marafiki zako, utawaambukiza na ndugu zako. Kwanini usiwe miongoni mwa watu ambao wakiandikwa historia yao huwezi kuacha kuandika bidii yao ya kusoma Neno la Mungu.

Huenda hili jambo linaonekana ni gumu kwako na lipo kinyume sana na matarajio yako katika wokovu wako, ila ndio ukweli ulivyo. Huwezi kuwa na huduma iliyosimama kama husomi Neno la Mungu, huwezi kutupa nyimbo zenye mguso wa kiMungu ikiwa huna muda wa kujifunza Neno la Mungu, huwezi kutuhubiria habari za Yesu Kristo ikiwa huna muda wa kujifunza Neno lake.

Hazina yetu kubwa kwa waaminio jina la Yesu Kristo aliye hai kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu, ni kukubali kutoa muda wetu kulisoma Neno la Mungu. Huenda kila siku unasikia hizi habari za kusoma neno la Mungu unazipuuza na kuona ni hadithi tu, nakuambia leo sio hadithi, ni kweli.

Bila shaka umepata mengi sana ya kufanyia kazi, usiache kuchochea kile umajifunza na kukiweka katika matendo. Haijalishi mazingira uliyopo sasa unapaswa kusoma Neno la Mungu, shule haiwezi kukuzuia wewe kuwa na nusu saa au saa moja kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu. Ukiona mambo yako yanakubana zaidi na kuona huna muda wa kusoma biblia ujue bado unahitaji msaada wa kiroho, maana bado hujamjua vizuri unayemwamini.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu. Kama bado hujajiunga na wenzako wanaosoma Neno la Mungu kila siku, unakaribishwa sana wasap group kwa sharti la kujitoa kila siku kusoma Neno la Mungu.

Usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com