Usikivu Wako Wa Ndani Unakuwaje Pale Unaposikia Neno la Mungu.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana wetu Yesu Kristo ametupa tena kibali mbele zake cha kuiona. Fursa kwetu kuendelea kulitimiza kusudi lake alilotuleta hapa dunia, haijalishi unaona matokeo ya unachofanya kwa kiwango kidogo sana, endelea kuweka juhudi kubwa Mungu atakubarikia kupitia hicho hicho kidogo.

Leo napenda kukufikirisha kuhusu upokeaji wako wa Neno la Mungu, unaposikia mtu anakuambia habari za Neno la Mungu. Huwa ndani yako unajisikiaje au unachukulia kama hadithi fulani tu ya kawaida kwako.

Kujitathimini ni jambo la msingi sana katika maisha yako ya wokovu, kuna vitu unaweza kuona upo sawa kumbe una shida ndani yako. Lazima uwe na wakati wa kutulia na kujichunguza hatua zako, usije ukawa umemfukuza Roho Mtakatifu ndani yako siku nyingi alafu ukaendelea kujiona upo salama.

Lazima ukae chini uangalie kiwango chako cha upokeaji Neno la Mungu kipo kivipi, yaani unaposikia sasa hivi Neno la Mungu, moyoni mwako unasikia uzito gani na ndani yako kunajengeka nini. Kama hakuna uzito wowote ndani yako, usikifikiri ni jambo ndogo sana na zuri sana kwako.

Wakati mwingine umeacha kusoma Neno la Mungu kwa bidii sio kwa sababu huna muda wa kutosha kufanya hilo jambo. Maana wewe ndio unajijua muda wako huwa unaupoteza wapi na vitu gani huwa vinakula sana muda wako, lakini mtu anaweza akukuuliza mbona husomi Neno la Mungu ukamjibu huna muda wa kusoma.

Ukiona hivyo ujue tatizo halipo katika muda wako, tatizo lipo ndani yako, huna ule uzito wa kukusukuma usome Neno la Mungu. Hii hali huenda imeletwa na kuona Neno la Mungu sio jambo la kuweka kipaumbele sana kwako katika ratiba zako za kila siku.

Lakini wale wanaojua umhimu wa hii kitu huwezi kumwondoa kwenye Neno la Mungu, huwezi kumweleza habari za sina muda wa kusoma Neno la Mungu. Muda tunao wa kutosha sana sema huwa tunachukulia kusoma Neno la Mungu ni suala la ziada sana, halihitaji kuwa kipaumbele sana cha siku.

Tutaendelea kuona kusoma Neno la Mungu ni mzigo/adhabu kwetu kwa sababu hatuna ule mwamko wa ndani, unaotukusuma na kutuamsha tusome Neno la Mungu bila kujiuliza mara mbili mbili usome au usisome.

Huenda wewe ni msomaji mzuri kabisa wa Neno la Mungu, lakini katika kusoma kwako unasoma ila hupati ile ladha wala hupati msisimko wowote, na unaona Mungu anakuonya na kukufundisha namna ya kuishi maisha ya kumpendeza yeye.

Bila kukuficha jambo lolote wala bila kukuzunguka eneo lolote, hiyo ni dalili mbaya ya kukaukiwa kiroho, hiyo dalili ya mtu aliyepoteza uhusiano wake na Mungu wake, hiyo ni dalili ya mtu anayeleta mazoea kwa mambo ya Mungu, hiyo ni dalili ya mtu ambaye njia zake hazipo sawa mbele za Mungu.

Kati ya hizo dalili unaweza kujiangalia wewe upo wapi hapo, haiwezekani hushtuki wala hujali unaposikia habari za Neno la Mungu. Ndio maana hadi wengine wanakaukiwa mpaka wakati mchungaji anaendelea kuhubiri mbele yeye anaendelea kuchati na mtu kwenye simu yake. Mtu mwenyewe anayechati naye amekaa tu mtaani wala hajaenda kanisani, au wanachati wote wakiwa kanisani humo humo au yupo kanisa lingine na anayechati naye.

Tabia mbovu wakati mwingine tunaziendekeza wenyewe, hali gani hiyo usiyoweza kuzuia mpaka umalize ibada? Ndio hizi hizi hali zinahamia kwenye kula muda wako mwingi kuchati alafu mtu akikuuliza mbona husomi biblia. Unachoweza kumweleza ni huna muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu.

Tufike wakati tujiulize tuna ukristo wa namna gani usioweza kutamani mambo ya Mungu, ikiwa tunaye Mungu ndani yetu nini kinatushinda kumwambia Mungu nahitaji kiu ya kulisoma na kulijua Neno lako. Huwezi kupata kitu usichokitaka kiwe chako, unapewa kile unahitaji na umeomba, sasa wewe huombi huku unasingizia vitu ambavyo havisiani kabisa na kukwama kwako.

Unaweza kuamua leo uanze kusikia kiu ndani yako ya kusoma Neno la Mungu, njia moja wapo ya kutibua kiu ndani yako ni kujua pasipo Mungu wewe usingekuwa hivyo ulivyo. Huenda hapo ulipo kuna wakati hospital zote zilikushindwa kukutibu ila mkono wa Mungu ukakuinua, elimu uliyonayo sio kwa ujanja wako bali Mungu tu alikupigania. Mafanikio uliyonayo huenda unafikiri ni kwa sababu ya maarifa uliyonayo, kumbe ni Mungu anakupigia usiku na mchana kuzuia maadui wasiharibu njia za kipato chako.

Hakikisha ndani yako unasikia msukumo wa kusoma Neno la Mungu, huoni hiyo hali ingia magotini kudai haki yako. Huko ni kupoteza kitu cha msingi sana ndani ya maisha yako, kupoteza kifaa cha kukuongoza porini ili usipotee njia ni hatari kubwa sana kwako.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, nakusihi sana kuzingatia usalama wako wa kusoma Neno la Mungu unabaki salama.

Usiache kufuatilia ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.

Chapeo@chapeotz.com