Usipotoshe Watu Maandiko Matakatifu Kwa Kuwa Yanaenda Kinyume Na Matakwa Yako.
Haleluya, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona tena. Hii ni neema kwetu kupata kibali cha kuiona siku ambayo wengi waliitamani lakini hawakuweza kuifikia. Tunapaswa kuhakikisha tunaitumia vyema siku hii ya leo kumletea Mungu sifa na utukufu.
Kila mmoja wetu ana namna Mungu anamsaidia kuelewa maandiko Matakatifu ili yaweze kumsaidia katika maisha yake ya kila siku. Uelewa ule Mungu anaompa kila mmoja wetu haufanyi tuwe wapotoshaji wa maandiko wala haitufanyi tuwe tofauti kubwa na wengine katika maana.
Haijalishi mtu yule anahubiriwa na wenzake pamoja, anaweza kupokea na kuelewa tofauti kabisa na wenzake. Utofauti ule sio kwamba umebadilisha maana, maana ni ile ile ila kila mmoja anaelewa zaidi kwa jinsi Roho Mtakatifu anavyoona itakuwa rahisi kwake kupata kitu.
Mungu anaweza kutumia mifano hai ya mazingira husika ya watu wakaelewa kile anakizungumza, na mwingine aliopo nje ya Tanzania akapewa naye mfano halisi wa mazingira yake ya huko aliko kuelewa zaidi kile Mungu anakizungumza.
Mwalimu akiwa anafundisha hesabu darasani hawezi kutoa maswali bila kukupa mifano kadhaa uelewe kile unachoenda kukifanya. Mwalimu hakupi mifano ya hesabu ya kugawanya alafu akakuachia maswali ya kujumlisha.
Tunapolifafanua Neno la Mungu katika mazingira ya kwetu, tunapolitafasiri Neno la Mungu katika lugha/kabila zetu. Haifanyi maana ya maandiko Matakatifu ikabadilika, maana ipo palepale hata kama kila mmoja anasoma kwa lugha yake.
Wengine wamefika hatua kusema Yesu Kristo alitoa mifano ya uongo isiyo halisi, biblia haijasema uongo ndio maana kama kuna mazungumzo ambayo yanamzungumza Yesu Kristo vibaya, yanajisema yenyewe na kujifafanua vizuri.
Narudia kusema kuna vitu unaweza kufundisha kutumia mifano hai ya mazingira husika, na mwingine akatumia andiko lile lile kulitumia mazingira mengine kutoa mfano tofauti. Itategemeana na jinsi gani Mungu atamfunulia mtu kuelewa vizuri kile anapaswa kuelewa.
Ndio maana unakuta darasani kuna mwalimu mwingine anafundisha na kueleweka vizuri zaidi ya wengine. Hii haimanishi huyu mwalimu asiyeeleweka anatumia kitabu tofauti na yule mwalimu mwingine anayeeleweka vizuri akifundisha la hasha, huyu anaeleweka kuna namna anaitumia kuwasaidia wanafunzi wake kuelewa.
Hebu wewe fikiri unasoma biblia inakupa habari za Israel mara inakuambia Yerusalem mara inakuambia Misri mara inakuambia kanaani. Hivi kweli Roho Mtakatifu asipokusaidia kufafanulia mazingira ya sasa ulipo utaweza kuelewa vizuri Neno la Mungu? Kwanza huenda hiyo miji yote unayoambiwa hapo hujawahi kufika wala anayekufundisha naye hajawahi kufika Israel.
Mpaka hapo unaweza kunielewa nazungumza nini, hii itakusaidia kuepuka kupotosha maandiko Matakatifu. Labda itokee ukashindwa kuelewa maana ya Neno fulani kwenye biblia, ndio tunarudi utaeleweshwa hilo neno kwa kile kitu unachokifahamu wewe.
Najua umewahi kufurahia jinsi mtumishi fulani alivyofafanua andiko fulani, mpaka unashangaa imekuwaje ulikuwa unapata shida kuelewa mstari huo ila kupitia fundisho lake umepata kuelewa vizuri zaidi. Kufundisha kwake ukamwelewa vizuri haimaniishi watumishi wengine walikuwa hawafundishi, ni ile namna alivyomtumia Roho Mtakatifu kuingia ndani zaidi.
Pamoja na kutumia njia mbalimbali kuelewesha watu, ukiwadanganya watajua tu. Hapa ndipo tunasema kupotosha maandiko Matakatifu, ukienda kinyume na kile Mungu amesema watu watajua huyu anatudanganya.
Haijalishi somo linalofundishwa ni gumu kiasi gani, kama Roho Mtakatifu ameruhusu hilo watu wataelewa hata kwa kuchelewa. Lakini upotoshwaji utabaki kuwa utoposhwaji, hakuna atakayekubali uongo kwa sababu anajua anachokiambiwa si kweli.
Wakati mwingine watu wanaweza kuona umesema uongo kwa sababu walikuwa hawajui andiko la namna ulivyosema. Ila utakapotoa andiko, wataona na watakubali ni kweli unachokisema. Maana Roho Mtakatifu aliye ndani yako ndiye yule yule aliye ndani yao, haiwezekani usipate kibali kwa watu wote isipokuwa kwa wale mlio kitu kimoja kuunga mkono uongo wako.
Pamoja na Yesu Kristo kupingwa na wakuu mbalimbali kutokana na uweze aliokuwa nao, wapo waliendelea kuamini na kumfuata Yesu. Hata wakati wa kusulubiliwa wapo wakuu waliona hana hatia, ila kutokana na maamzi yaliyotolewa asubuliwe hawakuwa na nguvu ya kuzuia.
Usije ukawadanganya watu wakafikiri hawatajua, biblia ipo wazi tena wanaoisoma wanaufahamu kujua huyu ametuingiza sio penyewe. Mungu hawezi kuzuia jambo fulani kwa baadhi ya watu wake alafu wengine akaruhusu, nasema hivi; Mungu hawezi kuzuia uzinzi/uasherati alafu akaruhusu kwa baadhi ya watu, haipo.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako, usiache kusoma Neno la Mungu maana linatupa kujua mengi zaidi tusiyoyajua.
Endelea kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com