Uelewa Wako Wa Baadhi Ya Maandiko Usikufanye Ukajiona Unajua Sana Ukaacha Kujifunza Zaidi.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa na njema machoni mwa Bwana ametupa kibali cha kuiona tena leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye maana Neema yake ni kuu sana kwetu.
Karibu sana tujifunze pamoja mambo ya kukusaidia kuwa imara katika eneo lako la usomaji wako wa Neno la Mungu. Hupaswi kuendelea kuwa kama jana unapaswa kuendelea kukua zaidi kiroho kwa kadri unavyozidi kumjua Mungu kupitia Neno lake.
Kuna tabia ambayo inakuwa ndani ya mtu baada ya kufahamu baadhi ya maandiko Matakatifu, anajiona amejua kila kitu na hahitaji tena kujua zaidi Neno la Mungu.
Tabia kama hizi inapomwingia mtu ujue inaenda kumpoteza zaidi na sio kumjenga, unapaswa kujua hakuna siku utafika kikomo cha kujifunza, kujifunza ni kila siku unayopata fursa ya kuiona. Ukifika hatua ukajiona hutaki tena kujifunza mambo ya Mungu kwa sababu unajua baadhi ya vitu, ujue huko ni kupotea.
Hatuli chakula kizuri cha mwili kwa siku moja tukasema imetosha kula, haijalishi jana ulikula vizuri sana utapaswa kula tena na tena. Hakuna siku utasema sasa imetosha kula chakula maana tangu umezaliwa mpaka sasa umekula miaka mingi. Mpaka pale utapoondoka duniani ndio utakuwa ukomo wako wa kula chakula.
Unakutana na mtu anajivuna kwa maneno mengi kwa kumaliza kusoma biblia yote, ukimuuliza umemaliza lini atakuambia labda mwaka mmoja uliopita au miaka miwili/mitatu iliyopita. Kumaliza kwake ameona hahitaji tena kuendelea kujifunza Neno la Mungu, ni kweli huyu mtu anapaswa kupongezwa kwa hatua aliyofikia. Ila roho iliyomwingia ya kujiona amemaliza kila kitu ndio ilipo shida yake, huyu mtu alipaswa kuendelea kujifunza zaidi Neno la Mungu kwa kurudia tena na tena.
Umechagua kuwa mwanafunzi mwaminifu wa Yesu Kristo, unapaswa kuwa mtu wa kujifunza Neno lake kila siku. Ili uendelee kujengeka zaidi kiroho, na kujengeka zaidi kiroho hakujengwi siku moja ukasema imetosha. Ndio maana hatuachi kukusanyika pamoja katika nyumba za ibada, hatujafika wakati tukasema imetosha kwenda kanisani.
Ukitaka kujipoteza kwenye mambo ya Mungu, fika wakati ukaona umejua kila kitu na huhitaji tena kujifunza chochote ndani ya biblia. Haijalishi umesoma sana Neno la Mungu, unapaswa kusikia kiu ndani yako siku hadi siku, maana hakuna siku utashiba moja kwa moja.
Kuna mpendwa mmoja aliyesoma chuo cha biblia akaniandikia ujumbe huu;
Group hili la Chapeo Ya Wokovu ni zuri mnoo, hata mimi ninakua kiroho zaidi ya nilivyofundishwa katika CHUO CHA BIBILIA NILICHOSOMA. KAKA TUPO PAMOJA BINAFSI NAPATA VITU VYA TOFAUTI MNO NINAPOKUWA HAPA CHAPEO YA WOKOVU.
Huyu ni ndugu yetu aliyefanikiwa kuingia chuo cha biblia akajifunza mengi huko, ila bado ana kiu ya kujifunza zaidi Neno la Mungu. Na ameona mabadiliko zaidi kwa jinsi anavyozidi kusoma Neno la Mungu, hakuona yeye amemaliza kila kitu na hapaswi kutenga muda tena wa kusoma NENO.
Shetani mjanja, anaweza kukupa ridhiko la moyo ukajiona huna haja tena ya kusoma biblia kwa kuwa umewahi kuisoma yote. Nakwambia ukishafikia hapo ujue usipokataa hiyo hali unaenda kupotea, maana hakuna kushiba mambo ya Mungu siku moja ikatosha.
Neno la Mungu ni jipya kila siku, tunalisoma kila wakati bila kuchoka yapo mambo tunaendelea kuimarishwa ndani yetu. Kuna dhambi zinaweza kukung’ania kabisa kwa kuwa huna Neno la kutosha ndani yako, ukafika hatua ukaona kama vile ni sawa wewe kufanya hivyo kumbe sio sawa.
Tenga muda wako kila siku kusoma Neno la Mungu, hakuna kuhitimu hili, ndio maana wazee waliomjua Mungu wao vizuri. Utamkuta ameng’ang’ana na biblia hata kama macho yake hayamruhusu kusoma, bado atafuta miwani ya kumsaidia kuona vizuri.
Mahusiano yetu na Mungu wetu ni ya kila siku, hakuna siku tutasema tumechoka kumtegemea Mungu, huko ni kupotea wala sio hali ya kawaida kwa mwamini. Neno la Mungu linakujenga maeneo yote ya maisha yako, iwe kiroho au kimwili, Neno la Mungu ndio mwongozo wako.
Hupaswi kuhitimu kusoma Neno la Mungu kama ilivyo huwezi kuhitimu kula chakula cha tumbo. Kila siku unaweka juhudi kufanya kazi ili usije ukakosa kula chakula, hii inatufundisha pia tuwe na bidii katika kula chakula cha kiroho ambacho ni Neno la Mungu.
Bila shaka kipo kitu umejifunza kupitia ujumbe huu, kama ulipunguza bidii ya kusoma Neno la Mungu. Kuanzia sasa amua kujitoa kwa upya katika kusoma Neno la Mungu, acha uvivu wa kujifariji kila siku utasoma kesho. Kama umeweza kusoma ujumbe huu, utaweza pia kusoma Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Usiache kufuatilia ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
0759808081/0715591559.
chapeo@chapeotz.com