Jaribu Kukiweka Katika Matendo Kile Kizuri Unachojifunza Ndani Ya Biblia.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, jina lipitalo majina yote, likitajwa pepo wachafu wanamtoka mtu, ukiomba kwa jina lake wagonjwa wanapona. Hili ndilo jina kuu lipitalo majina yote, tunapaswa kujua ndani ya mioyo yetu jina hili ili tuweze kulitumia ipasavyo.
Nimetumia Neno kujaribu ili uweze kunielewa vyema kile ninachokikusudia kwako ukielewa, naamini baada ya kumaliza kusoma ujumbe huu utakuwa umenielewa kwa kiasi kikubwa. Lengo ni wewe uendelee kuwa imara katika usomaji wako wa Neno la Mungu na si vinginevyo ndugu yangu katika Kristo.
Wengi wetu tunasoma Neno la Mungu na kuishia katika kulisoma tu, ila hatuliweki katika matendo kujua linawezaje kutusaidia pale tunapokuwa wahitaji wa jambo ambalo tulisoma ndani ya biblia tukifanya hivi tunaweza kupata hiki.
Ndio maana tumefika hatua tunaona hatuna haja tena ya kuendelea kuweka juhudi za kujifunza Neno la Mungu. Hii ipo na inaendelea kuwatokea wengi wanaohamasika na hili jambo la kusoma Neno la Mungu, lakini ukija kumfuatilia baada ya siku chache kupita utamkuta ameshaacha kabisa. Na mwingine anakuwa anasoma ila hapati ile ladha yenyewe ya Neno la Mungu maana anaona kama hadithi fulani hivi za kwenye vitabu vya kale.
Unapoambiwa ukiomba kwa jina la Yesu Kristo wagonjwa wanapona amini hivyo kweli na jaribu kufanya zoezi hilo uone ukweli wenyewe. Ukiambiwa ukikemea pepo kwa jina la Yesu Kristo, mapepo yanakimbia usiishie kukubali tu bali jaribu na wewe kwa ujasiri mkubwa ndani yako.
Siku moja nilijua vizuri kuwa jina la Yesu Kristo ni kiboko ya mambo yote baada ya kuombea mtu aliyekuwa anasumbuliwa na nguvu za giza. Nilikuwa kwenye mazoezi baada ya kusoma na kusikia jina la Yesu Kristo linaponya, kweli mtu yule alitokwa na pepo wabaya. Inaweza isiwe habari kubwa sana kwako maana hata neno linasema tusifurahie kwa kutoa pepo bali tufurahie kwa kuwa majina yetu yameandikwa mbinguni. Ila najaribu kukuambia umhimu wa kuweka katika matendo kile unachojifunza ndani ya biblia.
Kipindi cha nyuma wakati tunasoma katika kitabu cha Mathayo, nakumbuka siku hiyo niliamka asubuhi sana ya saa kumi na moja. Nilivyokuwa nasoma kitabu kile nilikutana na habari za kusamehe aliyekukosea, hii habari naijua muda mrefu sana na nilishaifanya kwa kuwaachilia walionikosea miaka mingi iliyopita ambao nilipanga kuwalipiza kisasi ila nilivyokutana na Yesu Kristo niliwasamehe. Lakini wakati nasoma kitabu hichi nilikuwa napitia kipindi kigumu sana ambacho nilihitaji kujua kwanini inatokea hivyo, na nilikuwa najihesabu kuwa sina kosa lolote.
Huwezi amini baada ya kusoma Neno la Mungu nilipata ujasiri wa kuliweka Neno katika matendo kwa kumwomba mtu msamaha aliyenikosea yeye. Yaani badala mimi kuombwa msamaha na aliyenikosea, mimi ndio nilichukua hatua ya kumwomba yeye msamaha kwa upendo mzuri tu. Kwanini nilifanya hivyo, nilikuwa najaribu kukiweka kile nilichojifunza katika matendo.
Unaweza kurahisisha sana kitu ambacho hakijakupata ila kikikupata ndio utaelewa vizuri kile unaambiwa. Ndio maana ninapomwambia mtu unapaswa kusamehe aliyekukosea huona kama hapaswi kufanya hivyo na sijui uchungu anaopitia yeye kwa kuumizwa na huyo ninayemwambia unapaswa kumsamehe. Weka katika matendo, Neno la Mungu halidanganyi kabisa, unachopaswa ni kuamini kwanza kisha kukiweka katika matendo.
Zipo shuhuda nyingi sana naweza kukupa, labda nikupe moja ya mwisho ili uweze kunielewa vizuri. Neno la Mungu linakataza uzinzi/uasherati lakini wapo watu wanasema huwezi kuishi bila hayo, na huwezi kuvuka ujana mpaka ndoa bila kufanya uasherati. Wengine wanaenda mbali kabisa wanasema mwanamke hawezi kutulia na mume wake huyohuyo mmoja lazima atakuwa na mwanaume mwingine wa nje. Na mwanaume hawezi kutulia na mke wake lazima awe na wanawake wengine wa kuzini nao huko nje.
Vijana ndio tuna changamoto kubwa katika eneo hili, tunaona maisha ya ujana bila ya kuwa na dada/kaka wa kukupoza tamaa zako za ngono huwezi kuishi. Tumejikuta tunatanga tanga huku na kule kulala ovyo na wakaka/wadada/wamama/wababa kwa kujiona hatuwezi kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Badala yake tumejikuta tunaharibu maisha yetu kwa kupata magonjwa mabaya na wadada kupata watoto wasiowatarajia, na wengine kufanya fashion ya kutoa mimba.
Wakati inawezekana kuishi bila ngono, mimi ni kijana mwenzako nakueleza kitu halisi usije ukasema kwa sababu nimeoa ndio maana nakueleza haya kirahisi. Ukasema sijui sana ninachokisema, shida ipo kwenye kuamini na kuweka katika matendo.
Hiyo ni mifano hai michache niliyokupa ipo mingi sana naweza kukupa na mingine unaweza kuchukua muda kuamini, na wakati mwingine usiweze kuamini kabisa. Ila kutokana na muda sitaweza kufanya hivyo, moyo wa somo hili haswa ni wewe kukuhimiza kuanza kuweka katika matendo kile unajifunza ndani ya biblia yako.
Haijalishi ni kwa hatua ndogo kiasi gani kukiweka katika matendo hicho unachotaka, hiyo isikupe shida wewe jaribu. Ukikosea tubu kwa Mungu alafu inuka ujaribu tena na tena, baada ya muda utaona umekuwa mkomavu anayempendeza Mungu na wengine watajiuliza uliwezaje kufikia hatua uliyonayo sasa.
Nilikuahidi tangu mwanzo utaondoka na kitu cha kukusaidia katika safari yako ya wokovu, ambayo imeambatana na usomaji wako wa Neno la Mungu. Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia, siwezi kujua umeguswa na neno gani kati ya haya mengi, ila naamini lipo moja hata kama sio mengi limekusaidia.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Wasap & calls; +255759808081.
Email; chapeo@chapeotz.com
Website; www.chapeotz.com