Umhimu Upo Mkubwa Sana Mtu Kujenga Umakini Na Kumaanisha Kile Anachokifanya.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, hongera kwa zawadi uliyozawadiwa na Mungu kuifikia siku ya leo tena. Sio kwa ujanja ujanja wako bali ni kwa neema yake Mungu imekuwezesha kuiona tena leo, huna budi kumrudishia sifa na utukufu kwa uweza wake.

Kabla ya yote napenda kukupongeza wewe uliyekuwa pamoja nasi wakati tunaanza kusoma kitabu cha Nehemia sura ya kwanza mpaka kufikia jana tukawa tumehitimisha sura 13. Pia nikupongeze wewe msomaji wangu wa makala hizi unayeendelea kutoa muda wako kusoma Neno la Mungu kwa mtiririko uliojiwekea wewe binafsi. Nakushauri sana usimamie msimamo wako usije ukaishia njiani, ukiona huwezi kujisimamia mwenyewe nakushauri utafute kikundi kinachoweza kukubana ukasoma Neno la Mungu kila siku.
Moja ya kikundi hicho ni CHAPEO YA WOKOVU ambacho kipo wasap, hichi kikundi kimejitoa na kuhakikisha mnafikia lengo mliojipangia/kukubaliana pamoja.

Baada ya utangulizi huo, karibu sana tujifunze pamoja umhimu wa kumaanisha kile unachokifanya hasahasa kwa upande wa kusoma Neno la Mungu. Tutaenda kujikita zaidi kwenye upande wa kusoma Neno la Mungu ambapo mtu akiwa makini na kumaanisha katika hili la kusoma biblia, lazima kuna faida nyingi atazipata.

Jambo lolote ukilifanya kwa uzembe na kulifanya ilimradi unafanya, siku zote huwa halina matokea chanya. Maana ukifanya sawa na usipofanya napo unaona sawa, lakini ukiwa unamaanisha kutoka ndani ya moyo wako kwa kile unachofanya lazima utavuna matunda ya bidii yako.

Wengi tunaanza kwa mbwembwe nyingi sana katika usomaji wetu wa Neno la Mungu, lakini ndani yetu haupo ule mhimizo wa kuona unachokifanya unapaswa kukifanya kwa bidii sana bila kujali sana mazingira uliopo wakati huo. Yapo mazingira ambayo unakuwepo ila sio kwamba yamekubana sana usiweze kutenga muda wako usome Neno la Mungu. Ila kwa sababu haumaanishi kile unachokifanya ndio maana unajikuta unajipa sababu zingine zisizo na msingi sana.

Ukimaanisha kabisa kusoma Neno la Mungu hutoruhusu mtu yeyote kula muda wako, utapambana kuhakikisha umepata hata nusu saa ya kutulia mbele za Mungu kulisoma Neno lake na kulitafakari. Kama huna msimamo na muda wako unaweza kumaliza siku yako kwa kupiga stori na marafiki zako kwa mambo ambayo mengine hayana faida yeyote kwako. Lakini kwa mtu ambaye anaheshimu muda wake ana ukomo wa kukaa na marafiki/ndugu zake, inapofika saa aliyojipangia kusoma Neno la Mungu utamwona akisimamisha kila kitu.

Nidhamu yako ya kusoma Neno la Mungu inawafanya hata wale wanaokufahamu kutokubughudhi pale unapowaambia ni saa ya kusoma Neno la Mungu. Ukiona ni ngumu kuwaambia unaenda kufanya nini ni bora kuwaanga kuwa unaenda kufanya jambo la mhimu sana, ni kweli ni la mhimu sana kwako hata kama kwao wataliona la kawaida.

Usipuuze hili katika safari yako ya kusoma Neno la Mungu, fahamu kabisa jambo unalofanya lina vita kali, shetani hapendi wewe ufunguliwe na kweli ya Mungu kwenye ufahamu wako. Anajua jinsi unavyozidi kulijua Neno la Mungu ndivyo unavyozidi kuongeza ulinzi zaidi wa yeye kushindwa kukudanganya. Kadri unavyozidi kumjua Mungu unaongeza idadi ya watu wanaopenda kujifunza kutoka kwako, na mtu yeyote akikukubali una nafasi kubwa sana ya kumshauri jambo akakusikiliza na kulitenda.

Hakikisha kila siku unajiuliza wewe kama wewe, je unamaanisha kweli katika usomaji wako wa Neno la Mungu au unafanya ilimradi siku imeisha na wewe uonekane ulishika biblia. Uzuri ni kwamba ukiamua kutulia na kuweka akili yako Kwenye kile unachokifanya wakati huo, hutoweza kusikia hata makelele wanayopiga watu kama utakuwa kwenye sehemu ambayo ina msongamano wa watu.

Ukweli ni kwamba hatutajikuta kila siku tupo sehemu za utulivu sana kutokana na shughuli mbalimbali za kila siku. Hii haiwezi kutufanya tukaacha kusoma Neno la Mungu wala haiwezi kutuzuia kwa sababu ndani yetu tunamaanisha kile tunachokifanya.

Jenga umakini na maanisha katika usomaji wako wa Neno la Mungu, utashangaa jinsi unavyojisukuma kushika biblia yako kila siku. Haijalishi umechoka utajikuta umejilazimisha kusoma Neno la Mungu, hii ni kwa sababu unaelewa sana umhimu wa wewe kuwa na muda wa kusoma Neno.

Swali la msingi kwako ni kujiuliza kwanini kusoma Neno la Mungu, ukishajijibu hilo swali utakuwa huna tena muda wa kuambiwa soma neno la Mungu bali utajisukuma mwenyewe kufanya hivyo.

Bila shaka umeona umhimu wa wewe kumaanisha kile unafanya, hii ni kwa maeneo yote ya maisha yako. Ukijitoa kufanya jambo fulani unapaswa kumaanisha kweli, hapo ndipo utaweza kufanikiwa na utaweza kuwahubiria na kuwafundisha wengine kupitia juhudi zako za matendo yako mema.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, bila shaka umeondoka na kitu cha kukusaidia katika safari yako ya usomaji wako wa Neno la Mungu.

Usiache kufuatilia ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Wasap&calls; +255759808081.
Website; www.chapeotz.com
Email; chapeo@chapeotz.com