Usiwadanganye Watu Kwa Kufikiri Hawaelewi Chochote.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya Bwana ametupa kibali cha kuiona tena, sifa na utukufu tumrudishie yeye mweza wa yote. Hakuna mtu aliyelipia awepo siku ya leo bali ni neema ya Mungu imetufikisha hapa tulipo.

Tunafika mahali tunaanza kufanya vitu ambavyo tunafikiri tunaowafanyia hawezi kuelewa tulichowafanyia, kutokana labda na jinsi tunavyoona uelewa wao ni mdogo. Tunafika wakati tunaanza kupotosha maandiko Matakatifu na kuanza kumezesha watu vitu visivyofaa ilimradi wafanye vile tunataka sisi.

Wakati mwingine tunaweza kupotosha watu maandiko kwa kutojua kwetu Neno la Mungu, tukaona tupo sahihi kwa kile tunachokiamini na kuwaaminisha wengine. Hapa unaweza kuelewa kuwa si kila anayepotosha maandiko ni mpinga Kristo la hasha wengine hawajaelewa vizuri maandiko yanasemaje.

Hatari kubwa sana kufundisha wengine habari za Yesu Kristo, wakati huo wewe mwenyewe huna muda wa kusoma Neno la Mungu. Nasema hatari kwa sababu utawapa watu shuhuda mbalimbali alizokutendea Mungu ila itafika wakati utaanza kutoka nje ya mstari, kwa mapokeo fulani uliyomeza bila kujua yapo ndani ya Neno la Mungu au hayapo.

Hasa hasa watu wanaohudumu madhabahuni, nikiwa namaanisha waimbaji, walimu, mitume, manabii, na wachungaji. Hawa wanapaswa kuwa rafiki mkubwa wa biblia, sio kuipenda tu bali wanapaswa kuwa wasomaji wa Neno la Mungu kwa bidii zote.

Hata sisi ambao tunaona hatuna hizo huduma za kusimama mbele za watu wengine, tunapaswa kulijua Neno la Mungu kwa undani wake bila kujalisha wewe ni mshirika wa kawaida au una nafasi ambayo haikupi kibali cha kusimama mbele ya kanisa. Elewa wewe bado ni mtumishi wa Mungu, unaweza kumhubiri Kristo kwa matendo yako mema uliyojifunza kupitia Neno la Mungu.

Usipokuwa na Neno la Mungu ndani yako ni rahisi kwako kudanganyika ukaamini ulichosikia ni kweli, na wewe kwa sababu hujui na aliyesema unamwamini. Utalibeba lilivyo na kuanza kulisha wengine uongo bila kujua aliyekuambia naye alikuwa hajui, hapa ndipo huwa tunaanza kumsaidia shetani kazi yake bila sisi kujijua kama tunakosea. Lakini pamoja na kutokujua kwetu Mungu hufungua mtu mmoja fahamu katikati yetu ili kutusaidia kutufungua fahamu zetu. Na wakati mwingine hutuma watumishi wake kuja kutuonyesha tulichoamini sio sahihi, tunachopaswa kuamini ni hiki na kile.

Shida ipo kwa mtu anayejua Neno la Mungu linasemaje alafu anapotosha wengine kwa maslahi yake binafsi, hii ni hatari kubwa sana kwa kanisa hasa hasa kwa wasio na muda wa kusoma Neno la Mungu. Wanaosoma Neno la Mungu watajua aliyefundisha amewadanganya maana wanachojua wao neno halisemi hivyo.

Tusifikiri tunapowadanganya watu kwa makusudi au kwa kutokusudia, Mungu ataendelea kutuacha tuwadanganye hao watu wake. Tuwe na uhakika ataibua watenda kazi wake katika nyumba yake kuisema kweli ya Mungu, nakwambia utaumbuka tu na usanii usanii wako. Haitajalisha itachukua miaka mingapi, ipo siku watajua ulichowaaminisha ni mafundisho potofu.

Usifikiri hizi kampeni za kuhamasisha watu wasome Neno la Mungu zinapotea bure bila matunda yeyote, Mungu ana makusudi yake kuweka msukumo huu ndani ya watumishi wake ili kuijua kweli. Ndio maana kama upo makini kusikiliza mafundisho ya watumishi wa kweli lazima atakuambia jenga tabia ya kusoma Neno la Mungu.

Hakuna kisingizio kwa aliyeokoka ilimradi amemruhusu Roho Mtakatifu kuwa ndani yake, huyu Roho Mtakatifu ndiye atakayemsaidia kumfunulia Neno la Mungu. Watu wengine wasiomwamini Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao, wanaweza wasielewe kabisa walichosoma ila wewe mwana wa Mungu una kibali hicho cha kulielewa Neno la Mungu.

Rejea; Kwa maana sisi si kama walio wengi, walighoshio neno la Mungu; bali kama kwa weupe wa moyo, kama kutoka kwa Mungu, mbele za Mungu, twanena katika Kristo. 2 Wakorintho 2:17.

Umeona hapo jinsi Neno la Mungu linavyoweka wazi kwa wana wa Mungu, sisi sio kama wale wanaopindisha kweli ya Mungu. Bali sisi ni tunanena yale Kristo anatupa kibali ndani yetu kuyanena, na hii inakuja kwa kadri tunavyozidi kuijua kweli ya Mungu.

Tena ukisoma sehemu nyingine ya maandiko Matakatifu inasema hivi;
Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina. 1 Petro 4 :11.

Nguvu yetu na ujasiri wetu utatoka wapi ikiwa hatusomi Neno la Mungu, uwezo wetu wa kuwaambia wengine habari njema za Yesu Kristo zitatoka wapi ikiwa kweli ya Neno la Mungu haimo ndani yetu. Tunapaswa kunena yale ya kweli kutoka ndani ya biblia na sio kutokana na hekima za wadamu wasiomjua hata Kristo.

Rejea; Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. 1 Wakorintho 2:13.

Epuka sana kuwadanganya watu ukifikiri hawajui kitu, hata kama umeenda pori gani ambalo una uhakika hawana muda wa kufuatilia sana kinachoendelea duniani. Mungu ni wa wote hatakubali watoto wake waendelee kubaki pale pale, atainua watu wake ili wapate kuwaambia iliyo kweli ya Mungu.

Mimi na wewe ili kuepuka kudanganya wengine au kudanganywa na wengine, ni kutoa muda wetu kulisoma Neno la Mungu kwa bidii zote bila kujalisha mazingira tuliyopo. Kama tunaweza kupata muda wa kufanya mambo mengine hata muda wa kusoma Neno la Mungu tutaupata.

Bila shaka kuna kitu fulani umekipata ndani yako kupitia ujumbe huu, ulichokipata kiwe chanzo cha wewe kuwa balozi mwema wa kumshauri mwingine kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Website; www.chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.
Email; chapeo@chapeotz.com