Kilichokukwamisha Mpaka Sasa Ushindwe Kusoma Neno La Mungu Ni Hiki Hapa.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Hatutachoka kumrudishia sifa na utukufu Mungu wetu kwa wema wake mkuu kwetu wanadamu, kama alivyo yeye Baba hachoki kuendelea kutuvumilia yale mabaya tunayomtenda, kama alivyo hachoki kutupa pumzi yake.

Zipo sababu nyingi sana za watu kushindwa kusoma Neno la Mungu, kila mmoja ana kisingizio chake cha kumfanya aendelee kubaki vilevile bila kusoma Neno la Mungu hata kwa wiki mara tatu. Mtu huyu anayeona kusoma biblia ni shida kwake, ana huduma ya kiroho anayotoa kwa wengine. Hebu fikiria waimbaji wasipokuwa wasomaji wa Neno la Mungu hizo nyimbo watazitoa wapi ikiwa wanayemwimbia hawamjui.

Kinachowakwamisha wengi katika eneo hili la kusoma Neno la Mungu ni kutokuwa na UVUMILIVU, mwanzo mtu anaposikia kusoma neno la Mungu anahamasika sana na kujiambia atafanya hilo zoezi kila siku. Hasa mtu ukimwambia soma sura moja tu kwa siku itakusaidia, mwanzo ataona kama kusoma sura moja ni kujichelewesha badala yake ataona bora asome sura tatu au tano kwa siku moja.

Kweli ataenda vizuri na hizi sura nyingi kwa siku za mwanzo, baada ya mwezi au miezi kadhaa ukija kumuuliza vipi bado unaendelea na utaratibu wako wa kusoma Neno la Mungu? Jibu atakalokupa linaweza kusikitisha kidogo.

Moja ya majibu ya wengi wetu tukiacha kusoma Neno la Mungu ni haya; sina muda, nasoma lakini sielewi, nimepumzika kidogo ila nitarudi kusoma tena, na mengine mengi sana ya mtu kujitia moyo kuendelea kukaa bila kusoma Neno la Mungu.

Uvumilivu unapomwondoka mtu hata nidhamu yake lazima ishuke kwa kile anachokifanya, kwanini, kwa sababu anaanza kuona kile alichokuwa anakifanya anajua kina umhimu kwake ila ndani yake hasikii tena msukumo wowote wa kukifanya.

Kitu kingine kinachoondoa watu kwenye utaratibu wa kusoma Neno la Mungu ni changamoto za maisha ya kila siku, hapa mtu asipokuwa mvumilivu na nidhamu kwa kile alichokuwa anakifanya lazima asitishe kile alichokuwa anakifanya.

Mtu anapata tatizo fulani la kifamilia au la kikazi, analishikilia hilo tatizo kiasi kwamba anaona ndio nguzo yake ya kusimamia, ukimuuliza shida nini anakwambia nilipatwa na jambo fulani miezi kadhaa iliyopita nimeamua kumpumzika kwanza kusoma Neno la Mungu.

Kama utakuwa mtu wa kuabudu matatizo yanayokupata, itakuwa ngumu sana kwako kufikia viwango vya KiMungu anavyovitaka kwako. Utakuwa mkristo wa msimu fulani, ukikwazwa kidogo unaacha kusoma Neno la Mungu, ukipatwa na msiba ndio kabisaa na Mungu unamweka pembeni, biashara yako ikichangamka na mambo ya Mungu unaona huna muda nayo, hiyo hiyo biashara ikiharibika unakuwa mtu wa hasira na kuona mambo ya kusoma Neno la Mungu ni adhabu kwako.

Kipi kitakuwa kizuri kwako mpaka ukasema sasa leo naanza kuwa mtu anayetenga muda wa kusoma Neno la Mungu, changamoto haziishi kila siku zinakuja tofauti tofauti. Unakuta leo umepatwa na hili, kesho likaibuka lingine kabisa, kwa hali kama hii unafikiri utamjuaje BABA yako.

Unapaswa kuwa mtu mwenye uvumilivu ndani ya moyo wako, vipo vitu sio vya kukufanya ukashindwa kutulia kusoma Neno la Mungu. Japo zipo kweli sababu ambazo zinakuwa zina uzito wake kwa muda fulani, na sio kila siku, huwezi kuacha mambo ya Mungu kwa sababu ulifiwa na mtu wako wa Karibu sana, huwezi kuacha kusoma Neno la Mungu kwa sababu mchumba mliyetegemea kuanza naye maisha ya ndoa hivi karibuni amekuacha. Utaumia kwa muda ila kuumia kwako kuwe na kiasi, usiwe kama mtu asiye na Mungu ndani yake, haiwezekani kuanzia JANUARY mpaka Leo MEI wewe ni mtu wa kujipa visababu.

Unapaswa kujiuliza mbona muda wa kuzurura mtaani unaupata, mbona muda wa kukaa vijiweni na marafiki unaupata, mbona muda wa kuzurura kwenye mitandao ya kijamii unaupata, mbona muda wa kulala masaa nane unaupata. Kinachokufanya ukose muda wa kusoma neno la Mungu ni kitu gani?

Haijalishi upo katika mazingira ya namna gani, kama mazingira hayo hayakukatazi kasoma Neno la Mungu, fanya hivyo, elewa changamoto hazitakaa ziishe kamwe. Endelea kuwa mvumilivu, unapatwa na tatizo leo ache likuumize leo ila kesho rudi tena kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, umeweza kusoma ujumbe huu fahamu hata Neno la Mungu utaweza.

Endelea kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

Chapeo@chapeotz.com

+255759808081.