Kadri Unavyozidi Kumjua Mungu Ndivyo Utii Na Unyenyekevu Wako Unazidi Kuongezeka Mbele Zake.
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona tena, sifa na utukufu tumrudishie yeye kwa kuwa yu mwema kwetu. Usije ukaacha kumtegemea Mungu katika mapito yako yote, uwe unapita wakati mgumu mtegemee Mungu, uwe unapita wakati wa furaha na amani mtegemee Mungu.
Karibu tujifunze pamoja somo leo, naamini hutatoka mtupu bali utaondoka na vitu/mambo mengi ya kukusaidia katika safari yako ya wokovu. Hongera kwa sababu umechagua fungu lililojema, kwanza hongera kwa kuamua kumpa Yesu maisha yako, na hongera kwa kuchagua kujifunza. Moja ya vitu ambavyo hupaswi kuhitimu ni kujifunza, endelea kuweka mikakati mizuri ya wewe kuendelea kujifunza zaidi na zaidi yaani hakuna kustafu maisha yako yote.
Kuna mambo mengine tunaweza kuwa tunafanya bila hofu yeyote kwa sababu hatuna uhusiano mzuri na Mungu wetu, tunaweza kuwa tunahimizana na kusukumana kutenda/kufanya vitu vya msingi ambapo hatukupaswa kusukumwa bali tulipaswa kujitoa wenyewe.
Wakati mwingine tunakuwa wakosefu ila kwa kutojua kwetu tunakuwa tunajihesabia haki wakati tu wakosevu. Hatuwezi kujua tunachokifanya na kukiamini kuwa ni sahihi kwetu wakati sio sahihi, ni mpaka pale tutapoamua kuitafuta kweli ya Mungu wenyewe.
Zipo tabia sugu ambazo zimejengwa ndani mwetu kwa mazingira mbalimbali tuliyokulia, tabia hizi sugu na mbaya zinaondolewa kadri unavyozidi kumjua Mungu wako. Bidii yako mbele za Mungu inakufanya uendelee kugundua vitu ambavyo hukuwahi kujua kama ni sahihi kwako kuvifanya, bidii yako itakusaidia kujua mwenendo wako mbele za Mungu ni sahihi au sio sahihi.
Mataifa wanajua sifa ya mtu aliye ndani ya Kristo, ndio maana kuna wakati unafanya vitu mpaka wasiomjua Kristo wanakushangaa. Kwa akili yako unaweza kufikiri ni ushamba wao kumbe sivyo, maana wamezoea kuona unayofanya wewe huwa wanafanya wao wasiomjua Kristo.
Tutawezaje sasa kumjua vizuri zaidi Mungu wetu na ndani yetu tukabadilika? Ni kwa kujifunza Neno la Mungu, Neno la Mungu lina nguvu ya kubadilisha msimamo wako mbaya na kusimamisha msimamo mzuri na imara ndani ya fikra zako.
Ipo misingi potofu tuliijenga ndani mwetu kwa sababu ya mazingira na mapokeo ya dini zetu, lakini kadri tunavyozidi kuijua kweli ya Mungu. Kuna mienendo ambayo tulikuwa tunaenenda nayo isiyompendeza Mungu wetu, tutaiacha baada ya kuijua kweli ya Neno la Mungu.
Biblia haina upendeleo wa mtu yeyote, biblia haina upendeleo wa dhehebu/dini fulani, yenyewe inaeleza iliyo kweli. Haiangalii nafasi ya mtu katika jamii yenyewe inatuelekeza wote tuwe katika njia moja ya wokovu.
Uzuri wa kusoma Neno la Mungu tunaweza kuusema kwa namna nyingi sana, na kila sifa ina msingi wake mzuri wa kukusaidia kuzidi kuwa imara katika maisha yako ya wokovu. Lakini leo nimependa kukueleza kadri unavyozidi kumjua Mungu ndani yako kunajengeka utii na unyenyekevu wa hali ya juu sana.
Wakati mwingine tumekosa utii na unyenyekevu mbele za Mungu kwa sababu hatuna maarifa ya kutosha ndani yetu, wakati mwingine tumejihesabia haki tukijua tunavyoenenda ni sahihi kumbe sivyo. Inafika wakati tunahalalisha uovu tukifikiri tupo sahihi kufanya hivyo, wakati mwingine nidhamu yetu mbele za Mungu imetoweka kwa kukosa maarifa ya Neno la Mungu.
Hebu nikushauri leo ndugu yangu, hebu anza kuona Neno la Mungu kwa sura ya tofauti mno nikiwa namaanisha ondoa mazoea na ule ukawaida wakuona ni kitu cha kawaida kwako. Nakwambia utaona mabadiliko makubwa sana katika usomaji wako wa biblia, huenda sasa hivi huoni utofauti wowote ni kwa sababu ya mazoea yako.
Binafsi najiona upo utofauti mkubwa sana ndani yangu, ndio maana ninachokueleza hapa sio nimeona kwa mtu mwingine tu, nimejiona mwenyewe pamoja na ninazidi kuona wengine wakibadilika. Kinachotakiwa sasa ni kuongeza bidii zaidi, bidii yako ina matunda mengi sana.
Hakikisha siku yako haiishi bila kusoma Neno la Mungu, Neno la Mungu lina kila sifa unayoijua wewe na usiyoijua. Kadri unavyozidi kujifunza ndivyo unavyozidi kujiepusha na mazingira ya kumtenda Mungu dhambi, kadri unavyozidi kujifunza ndivyo hekima ya kiMungu inazidi kujengeka ndani yako.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp +255759808081.