Tunawezaje Kuwa Na Imani Thabiti Isiyo Tetereka Hata Pale Watu Wengine Wapoona Haiwezekani Kabisa.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona tena, sifa na utukufu tumrudishie yeye Mungu mweza wa yote.

Kumekuwa na utata na sintofahamu nyingi juu ya waamini, tukiwa kwenye furaha tunakuwa na ujasiri wa kusema Yesu Kristo ni mweza wa yote. Ila tukikumbwa na misukosuko ule ujasiri wetu wa kusema Yesu Kristo anaweza unaisha kabisa, wakati mwingine mtu akija kwako akakuambia endelea kumwamini Mungu atakusaidia tunaona kama anatusanifu.

Imefika kipindi mtu yupo kanisani na anasema Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yake, ila anafikia kipindi anaenda kwa waganga wa kienyeji kutafuta msaada zaidi baada ya kuona alipofikia Mungu hakumsaidia. Tuna shida gani inayotufanya tufike wakati tunaona wachawi wana weza kuliko Mungu, nini inatufanya tushawishike kwa waganga wa kienyeji.

Unaweza kusema kirahisi hao hawana Mungu ndio maana wanafanya hivyo, ndugu usifanye haraka kusema hivyo…labda wewe unayewafikiria hivyo kesho tukakuona unaongozana kwenda kutafuta msaada kwa miungu mingine. We unafikiri wana wa Israel kujitengenezea mungu wao baada ya kuona Musa amekawia kurudi toka mlimani, hawakujua uweza wa Mungu wao aliyewavusha bahari ya shamu? Lazima walijua.

Mtu mmoja akahoji hili, inakuwaje wakristo inafika kipindi tunaona Mungu anaweza mambo mengine, na mambo mengine Mungu hawezi. Badala yake tunaona waganga wa nguvu za giza wanaweza kutusaidia kuliko Mungu. Unaweza kuona ni swali la kawaida sana ila lina maana kubwa sana, leo hii watu wapo makanisani ila kwenye maduka yao wamechimbia hirizi, leo hii wakristo wapo makanisani wakipatwa na tatizo kidogo wanakimbilia kwa bibi/babu fulani.

Kuna shida gani ambayo inapelekea watu kutomwona Mungu ndio mweza wa yote, nini inatufanya siku za mwanzo tunakuwa na imani iliyoshiba. Ila kadri tatizo linavyozidi kutukandamiza ndivyo imani yetu inazidi kushuka, hata ile bidii yetu ya kumwomba Mungu juu ya jambo fulani inaisha kabisa.

Kuna siku moja nilienda hospital kumwona ndugu mmoja alikuwa anaumwa sana, nilivyomwangalia kweli alikuwa hatamaniki na nilivyowaangalia waliokuwa wanamuuguza walikuwa hawana tena tumaini. Hawa ndugu walikuwa wakristo tena haya makanisa tunayoyaita ya kilokole, sasa niliwaambia tumwamini Mungu atamponya. Niliwaomba nimwombee yule ndugu, nilivyomwekea mkono kwenye mwili wake nilisikia kama shoti fulani kwenye mkono wangu na nilisikia kama mkono wangu unakosa nguvu, moja kwa moja nilijua kuna kitu kisicho cha kawaida.

Baadaye nilivyofuatilia niliambiwa walienda kwa waganga wa nguvu za giza kutafuta msaada, yaani kwa kifupi walichanganya Mungu wa kweli na miungu mingine, na si unajua Mungu wetu alivyo hapendi kuchanganywa na miungu mingine. Kwa hiyo hapo hospital walikuwa wapo kama geresha tu ila kuna mambo mengine yalikuwa yanaendelea chini kwa chini.

Unaweza kuona ni kiasi gani kuna mambo mabaya yanaweza kuendelea ndani ya kanisa kwa waamini bila sisi wenyewe kujua. Unaweza kuona upo pamoja na ndugu yako katika safari ya wokovu kumbe mwenzako ana tegemeo lingine la miungu yake. Lakini mnaenda wote kanisani na mnatoka wote kwa pamoja, na huduma mbalimbali za kanisa anashiriki vizuri kabisa bila tatizo lolote.

Kanisa lisipokuwa na jicho la rohoni na kuchukua hatua, utashangaa hata wale viongozi wa makundi mbalimbali ndani ya kanisa ni wachawi. Utasema unaongea nini wewe, kamuulize Simoni aliyetenda mambo yake makuu kwa watu kutumia nguvu za giza tangu utoto wake. Labda unasema mtumishi unanidanganya na habari zako za uchawi hakuna kitu kama hicho, hebu soma hapa;

Rejea;Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka. MDO 8:9‭-‬13 SUV.

Bila shaka umeona mwenyewe hizo habari za Simoni, jiuliza tuna akina Simoni wangapi makanisani, jiulize tuna akina Simoni wangapi kwenye idara mbalimbali za uongozi, jiulize tuna akina Simoni wangapi kwenye biashara na kazi zetu. Hayo ni machache niliyoweza kukushirikisha kuhusu imani za watu zinavyoweza kuhama kutoka kwa Mungu wa kweli na kuhamia kwenye miungu mingine.

Nikirudi Kwenye moyo wa somo hili, tunaweza kusema imani yetu huwa inashuka na kuanza kuchepuka kwenye miungu mingine kwa sababu hatuna Neno la Mungu. Neno la Mungu likiwa ndani yetu kwa wingi hatutamtenda Mungu dhambi, maana ile hofu ya Mungu itakuwa ndani yetu. Na tutaweza kusimama kwa ujasiri kusema Mungu wetu anaweza hata pale ndugu zetu wanapotushawishi tugeuze mawazo yetu kwenda kutafuta msaada mwingine.

Yesu alisema hivi; Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli. Mathayo 8:10 SUV.Yaani Yesu Kristo katika toa yake yote ya huduma hakuwahi kuona imani kubwa ya namna hii, zaidi sana alikuwa anaona imani kama hii;

Rejea; Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Mathayo 8:26.

Wengi tunateswa na imani haba, na imani zetu haziwezi kuongezeka na kukomaa kama hatutakuwa watu wa kusoma Neno la Mungu na kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu. Kadri unavyosoma Neno la Mungu ndivyo imani yako inazidi kuongezeka na kujengeka ndani yako.

Hebu jenga utaratibu wa kusoma Neno la Mungu, ndani ya Neno la Mungu ndimo palipo na kila kitu, kadri unavyojifunza Neno la Mungu ndivyo unavyozidi kuzijua na hila za mwovu shetani na kuweza kujitenga nazo. Utakuwa na uwezo wa kulipa Jaribu lako andiko linasema hivi, halitaweza kukuingiza kwenye dhambi kwa sababu tayari utakuwa unaelewa mtengo wa kupatwa hilo jaribu ni ili umkosee Mungu wako.

Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia katika safari yako ya wokovu, hakikisha uliyojifunza unayaweka katika matendo. Kusoma Neno la Mungu ni kwa faida yako mwenyewe wala si yangu ninayokuandikia haya, mimi nakukumbusha wajibu wako kama mtu mwenye safari ya kwenda mbinguni. Na kama mtu anayetamani kuishi maisha ya umilele baada ya haya.

Usiache kutoa maoni yako hapo chini kwenye sehemu ya comment, unaweza kutushirikisha changamoto yako kupitia comment au kupitia hizo namba nitakazotoa au kupitia email address.

Facebook; Chapeo Ya Wokovu.

Email; chapeo@chapeotz.com

WhatsApp &Calls; +255759808081.