Faida Ya Kusoma Neno La Mungu Mkiwa Katika Muundo Wa Kundi(group).

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametuchagua mimi na wewe tuweze kuiona na kwenda kumzalia matunda yaliyo mema. Tunapaswa kuitumia vyema siku ya leo ili tuendelee kuujenga mwili wa Kristo kwa matendo yetu mema, kwa kuwambia wengine habari zake njema, na kwa kuwasaidia wahitaji.

Leo napenda tujifunze jambo la msingi sana ambalo wengine huwa tunaliona la kawaida, ila lina msaada mkubwa sana kwa yeyote atakayejua umuhimu wa yeye kufanya hivyo. Najua ulipokuwa shule, walimu huwa wa mtindo wa kuwaweka wanafunzi katika makundi madogo madogo kujadili maswali fulani atakayowapa.

Kila mmoja ana mtazamo wake na picha yake kwa hicho anachokifikiri kwa wakati huo, lakini mnavyozidi kujadili kwa pamoja, sio kila atakayetoa hoja yake itakuwa ndio jibu sahihi. Na sio kila kundi litapatia jibu la swali ambalo mwalimu alitoa, ila kupitia kujadiliana pamoja hilo swali yupo anayeelewa na yupo asielewa kabisa.

Yule asiyeelewa ndio nafasi yake kuelewa kwa upana zaidi kupitia wanaoelewa vizuri, na ataelewa zaidi pale mwalimu atakapotoa majibu ya pamoja na kuhitimisha mada husika. Lakini katika kujifunza kwa makundi huwa kunaibuka upana zaidi wa jambo linalojadiliwa, hata mwalimu anapata nafasi ya kujua mengi kupitia mawazo mbalimbali ya wanafunzi wake.

Mtu asiyeelewa umhimu wa makundi(groups) anaweza asione sana hili ninalosema, ila makundi yanakupa nafasi ya kuuliza pale ambapo hukuelewa vizuri. Hata usipoouliza unapata nafasi ya kusoma/kusikiliza wengine wameelewaje kuhusu hilo mlilokuwa mnalijadili. Mnaweza kutofautiana katika kuwasilisha hoja zenu, ila katika hizo tofauti za hoja zenu zikawa zina lenga maana moja ya kile mnajadili. Hapo ndipo tunasema kupanua uelewa wako zaidi, kwa mawazo mengine zaidi ya wenzako.

Unaweza kuelewa kwa juu juu jambo hilo mnalojadili kwa pamoja, ila yupo mwenzako akaingia ndani zaidi kueleza hilo jambo. Kwa hiyo kama ulikuwa na hatua fulani fupi unaongezewa hatua zingine zaidi, hapa ndipo tubakubaliana wote kuwa kujifunza ni kila siku.

Usijisikie vibaya unapojua ulikuwa unaelewa tofauti kabisa na maana halisi, kwa anayejifunza huo ndio utakuwa mwanzo mzuri wa yeye kuelewa na kuondoa mawazo yale yasiyo sahihi. Ila itakuwa mbaya kama utaendelea kushikilia yale yasiyo sahihi kwako, ila kwa mwenye sifa za mwanafunzi ataona mwanzo alikuwa gizani sasa ametolewa huko kwa kujua lililo sahihi.

Makundi yana faida kubwa sana kama utakuwa unajifunza vitu vizuri vya kukujenga kiroho/kimwili, na makundi yale yale yana hasara kubwa sana kama utakuwa mnapotoshana. Si umesikia watu wakisema ukitaka kumjua mtu haraka tazama marafiki zake anaoambatana nao muda mwingi.

Ukitaka kupanua uwanja zaidi wa mawazo yako, penda kujifunza kwa wengine, penda kuwasikiliza wengine, penda kusoma vitabu vya wengine. Utaona uelewa wako ukapanuka zaidi, hapa uwe makini maana utakutana na wapotoshaji.

Nikija kwenye Neno la Mungu, mnaposoma kama kikundi kuna vitu vingi sana unaweza kujifunza kupitia wenzako. Maana kupitia andiko lile lile Roho Mtakatifu anaweza kumfunulia mwenzako tofauti kabisa na ulivyoelewa wewe mwanzo, bila kuharibu maana halisi ya andiko husika.

Vizuri sana ukapenda kusikia wengine wanasemaje zaidi kuhusu lile unaloelewa wewe, inakupa uwanja mpana zaidi wa kuepuka kukariri Maandiko Matakatifu na badala yake utakuwa unaelewa. Sikuambii kusoma biblia ukiwa peke yako ni vibaya la hasha ninachokuambia ni kupenda kujifunza kwa wengine zaidi.

Neno la Mungu linaweka mawazo yetu kuwa mamoja, Neno la Mungu linaweka tabia zetu kuwa za kufanana, Neno la Mungu linaweka sema yetu kuwa moja, Neno la Mungu linaondoa tabia mbaya za asili ambazo mtu alikuwa nazo. Ndio maana unaona waliokoka kweli wanatabia fulani hivi za kufanana, na walio nusu nusu nao tabia zao zinafanana kabisa.

Kundi hili unaweza kulitengeneza katika familia yako, ule wakati wa usiku ambao mnaomba pamoja kabla ya kulala. Hebu shirikishaneni Maandiko Matakatifu hata sura moja ya kitabu au mistari michache ya biblia, alafu pateni muda wa kuulizana maswali na kueleweshana pale ambapo mmoja wenu hakuelewa. Na wewe uliyeelewa unapata kuongoza maarifa mengine mengi zaidi.

Kundi lingine unaweza kulipata kanisani kwenye vile vipindi vya mafundisho ya Neno la Mungu, pale mtoa Neno anapomaliza kufundisha. Mara nyingi huwa wanaacha kipindi cha kuuliza maswali katika somo alilofundisha, vyema ukatumia nafasi hii kuuliza na kupata majibu ya uhakika zaidi ili kuondoa wasiwasi.

Kundi lingine la mwisho kabisa kulizungumzia, ni kundi la WhatsApp haya makundi ni mazuri sana kama utayatumia vizuri. Mfano mzuri ni hili la Chapeo Ya Wokovu unapata muda mzuri wa kusoma Maandiko Matakatifu, unapata nafasi ya kusoma tafakari mbalimbali za watu wengine, na unapata nafasi ya kuuliza swali eneo ambalo hukuelewa vizuri. Hizo ndio faida za makundi mbalimbali unapokuwepo humo.

Bila shaka kuna kitu umekipata na umejua umhimu wa makundi/kikundi, yale uliyojifunza hebu yaweke katika matendo utaona mabadiliko makubwa sana katika usomaji wako wa biblia.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kufuatilia mtandao wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

WhatsApp +255759808081.