Usipokuwa Na Neno La Mungu Moyoni Mwako Utaamini Kila Unabii Na Ndoto Unayoota.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana wetu mweza wa yote kwa matendo yake makuu kwetu.

Zipo sababu za msingi sana kuhimizana kusoma Neno la Mungu na kulifanya kama sehemu yetu ya maisha, bila kujali umri tulionao na bila kujali miaka tuliyokaa ndani ya wokovu. Kila mmoja anapaswa kulichukulia hili jambo la kusoma Neno la Mungu kwa uzito mkubwa sana ndani ya moyo wake.

Tumekuwa tunachukulia kawaida sana tunapozungumzia umhimu wa mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni, awe na ratiba ya kujifunza Neno la Mungu kila siku. Haijalishi anatoa huduma madhabahuni au hatoi, ilimradi ni mkristo mwenye matarajio ya kuishi maisha mengine ya umilele baada ya haya duniani, anapaswa kusoma na kulijua Neno la Mungu.

Pamoja na kuhimizana hilo bado wengi wetu wanachukulia ni jambo linalowahusu watu fulani ila wao haliwahusu, ndio maana tumezidi kuona madhara mengi ndani ya kanisa. Vilevile tumezidi kuona faida kubwa ndani ya kanisa kadri watu wanavyozidi kulijua Neno la Mungu.

Kupitia Neno la Mungu ndio unakuta yale mapokeo ya dini na mila, na desturi kwa vitu visivyofaa mbele za Mungu, vinazidi kunyonywa taratibu kadri watu wanavyozidi kumjua Mungu wao na kubaki Neno la Mungu limesimama. Japo bado safari ni ndefu sana katika eneo hili lakini tukiendelea kuweka bidii na kumruhusu Roho Mtakatifu ndani ya mioyo yetu atufundishe, tutaona mambo makuu yakitendeka katika maisha yetu ya wokovu.

Siku hizi kumeibuka vitu vya ajabu sana, mtu anakwambia nimeotoshwe jambo fulani na Mungu. Ukimhoji vizuri unagundua kabisa sio Mungu aliyehusika katika ndoto hiyo bali ni ulimwengu mwingine wa giza umehusika katika eneo hilo.

Dada mmoja akaniambia siku moja, nimeonyeshwa kaka fulani mtumishi ndio atakuwa mume wangu nitakayeishi naye. Kwa maelezo yake nilipata wasiwasi ndani yangu, nilichomwambia una uhakika na ulichoonyeshwa? Akaniambia ndio nina uhakika. Basi nikamwambia tumwombe Mungu kama ni kweli itajulikana na kama ni uongo napo itajulikana.

Baada ya kama wiki hivi, alikuja tena akaniambia mtumishi ile ndoto haikuwa kweli, nimeona yule kaka niliyeonyeshwa sio mume wangu. Nilimuuliza kwa nini asiwe mume wako na wakati uliniambia umeonyeshwa na Mungu? Alijizungushazungusha tu kwa maneno ila nilichojua ni maombi yale niliyomwambia tuombe.

Hebu fikiri wangapi wanaingia kwenye maombi wakiwa hawana Neno la Mungu mioyoni mwao, wanawezaje kuchuja habari za kweli na uongo. Maana shetani yupo kazini masaa 24, wangapi walisema Mungu amewaonyesha waume/wake wao wa kuoa/kuolewa ila wanateseka leo ndani ya ndoa. Na wengine wamekuta wameolewa mke wa pili kumbe yule mwanaume alikuwa na mke mwingine kwa siri, na watoto anao wa kutosha.

Wangapi wamekutana na wanaume wamewaambia wameonyeshwa na Mungu kuhusu dada fulani atakuwa mke wake, lakini wakishakubaliwa na hao wadada wanaanza kuomba wafanye nao uasherati/ngono. Na ukiwaangalia wanaonekana wameokoka vizuri kabisa kumbe ni picha tu ya nje, ila ndani mwao wamejaa tamaa mbovu na wanafanya huo uchafu kwa siri. Huyu kaka utasema Mungu huwa anamwonyesha watu wa kwenda kufanya nao mapenzi kwanza ndipo awaoe?

Unaweza kuona ni ni kitu gani nakueleza hapa, wengine wamedanganywa na mtu kujiita mtumishi wa Mungu. Alafu huyu mtumishi kijana ni mzinzi hujawahi kuona, dada anakwambia kweli nimeonyeshwa ni mume wangu. Kumbe ni pepo ndio linafanya hiyo kazi ya kuwapelekea picha ya huyu kaka kuonekana anafaa kwao.

Lakini tunengekuwa na Neno la Mungu tungejua kuchuja mbivu na mbichi, nabii zingine ni za kupotosha ili umtende Mungu dhambi. Ndoto zingine ni za kuharibu mahusiano yako na Mungu na wala sio kujenga uhusiano wako na Mungu.

Tunapaswa kuwa na akiba ya kutosha ya Neno la Mungu, haiwezekani ukapewa tango pori kwenye ndoto alafu Roho Mtakatifu akanyamaza kimya na ukawa na amani moyoni. Jambo la kiMungu huwezi kukosa amani, jambo la kiMungu huwezi kulilazimisha kwa akili zako huku moyoni unasikia kabisa kukosa amani. Sio kana kwamba una hofu, ni kengele ya Roho Mtakatifu inakuambia aisee hicho kitu sio sahihi kwako acha mara moja. Kwa kuwa huna Neno la Mungu moyoni mwako utakaidi.

Tunapaswa kuwa waombaji wazuri ila zaidi tunapaswa kuwa na Neno la Mungu ndani mwetu, vinginevyo tunaendelea kubaki kwenye vifungo fulani vya shetani tukijua ni Mungu anatuambia tubaki/tufanye hivyo. Watakuja manabii wa uongo kukulaghai upoteze uwelekeo wa wokovu wako, ila ukisimama vizuri na Neno la Mungu hawatakuweza.

Mafundisho ya Neno la Mungu ni mhimu sana kwako, hasa hasa sisi vijana tunaopitia changamoto za mambo mengi katika maisha ya ujana. Na wengine wanasikia msukumo wa kumtumikia Mungu katika eneo fulani, pasipo kula Neno la Mungu vya kutosha utajikuta umepoteana vibaya.

Hebu tuepukane na haya mambo ya unabii feki na ndoto feki nikiwa na maana hazitoki kwa Mungu hasa hasa sisi tuliokoka tunatafutwa sana, na wengi tumepotezwa sana eneo hili. Tukijua tumekutana na Mungu kweli kumbe ilikuwa mungu mwingine, ambapo baadaye unaona matokeo hasi badala ya chanya.

Bila shaka kuna kitu umekipata na umeona umhimu wa kujua Maandiko Matakatifu, fanyia kazi kwa vitendo uliyojifunza. Narudia tena kukuhimiza, penda Neno la Mungu, na penda mafundisho ya Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.