Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, asubuhi nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuiona.
Bado unaendelea kujifunza NENO la Mungu au tayari umeanza kuvunjika moyo, au bado hujaanza kabisa kusoma NENO ukijiahidi utaanza kesho.
Tulianza na ahadi nyingi sana, unakumbuka ulichoahidi kuwa mwaka huu ni wa kusoma NENO, swali langu ni je umeanza, na kama umeanza bado unaendelea?
Napenda kukumbusha mapema sana usije ukasema niliona nijipe muda kidogo, lakini mpaka sasa unafikiri muda huo utafika.
Ninachoweza kukushauri, anza kusoma NENO kuanzia LEO, utasema sina muda, nami nikuuliza huo muda wa kuzunguka kwenye mitandao ya kijamii unaupata wapi.
Mbona hukosekani online, mbona hukosekani kusoma jumbe mbalimbali zenye kukutamikia baraka za mwaka na siku. Sio vibaya kusoma, na sio vibaya kutamkiwa baraka, swali langu kwako huo muda wa kuzunguka kwenye mitandao unautoa wapi?
Tunapenda sana sababu, tuna hoja nzuri sana za kutetea uvivu wetu, mtu yupo tayari kuzurura kwenye mitandao masaa matatu, ila hayupo tayari kutenga nusu saa kwa ajili ya kusoma NENO.
Mtu huyu huyu ndio wa kwanza kutaka atendewe miujiza, hana muda na Mungu, kanisani kwenyewe hafiki kwenye vipindi kwa sababu ya uvivu wake, na si kana kwamba amebanwa sana na kazi.
Mtu huyu huyu akishaona mambo yamemwendea vibaya, ndio mtu wa kwanza kuwasumbua watumishi, lakini wakati ana muda wa kumtafuta Mungu kwa kusoma NENO lake ili apate maarifa hakufanya hivyo.
Mtu huyu wakati ana muda wa kuomba hakufanya hivyo, amesubiri adui ameingia anaanza kusumbua wengine .
Dira ya maisha yetu kiroho na kimwili ni NENO la Mungu, hakuna namna tunaweza kukwepa hili. Ili tufanikiwe kiroho na kimwili lazima tulijue NENO na tuwe watendaji wa NENO.
Kwanini tuendelee kuruhusu kuangamizwa kwa kukosa maarifa wakati tuna uwezo wa kujitoa kwa ajili ya kusoma maandiko matakatifu.
Hakuna kisingizio, zipo biblia za sauti unawaza kuzipakua kwenye play store, kama unaona kusoma ni shida unaweza kusikiliza wakati umetulia zako ofisini au kwenye eneo lako la biashara, au ukiwa safarini.
Ushindwe mwenyewe tecnolojia imekurahisishia kila kitu, leo tupo 2 Wafalme 18.
Samson Ernest.
+255759808081