Haleluya mwana wa Mungu, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai. Mungu ni mwema ametupa kibali kingine cha kuiona leo, bila shaka una sababu ya kumshukuru MUNGU kwa wema na fadhili zake.
Hatujachoka bado kukumbushana umhimu wa kusoma NENO la MUNGU, maana ipo faida katika kujifunza NENO. Tukisema tumechoka kuambiana umhimu wa NENO, haitakuwa vyema kabisa.
Hatusomi NENO ili tuje tujibu mtihani wa darasani, zipo faida nyingi katika kujifunza NENO, moja wapo ni kukusaidia kutatua changamoto unazokutana nazo ndani ya WOKOVU wako.
Pamoja na hayo bado ipo faida nyingine ya kulijua NENO, ambapo unapata kujua haki zako za msingi mbele za Baba yako aliye mbinguni.
Unapoacha kusoma NENO, unakosa mambo mengi sana mazuri, ambayo yangekuwa msaada kwako katika safari yako ya wokovu.
Tunakuwa wepesi kukata tamaa kwa sababu hatujui lipi haswa la kushika pale tunapojikuta tupo njia panda, yaani unakuta mambo yanakuvuta huku na lingine linakuvuta kule. Nyakati kama hizi huwa tunaona bora tuachane nayo kumbe ndio tunakosa haki zetu za msingi.
Msingi wetu tulioliamini na kulikubali jina la Yesu Kristo, tunao wajibu wa kujitoa kwa hali zote kujua NENO la MUNGU. Haijalishi upo katika mazingira gani kama unapata fursa ya kushika biblia tumia nafasi hiyo.
Nimesema sana kuhusu hili; kama una simu, laptop, tablet una uwezo kuwa na biblia ya kusoma kawaida, ama ukawa na audio ambayo inakusaidia kusoma NENO kwa njia ya sauti.
Ukiwa makini na hili hakuna sababu ambayo itakufanya ukose NENO, huwezi kuzuiliwa kusoma NENO hata uwe mfungwa. Labda pawepo sababu maalum ya wewe kukatazwa kushika biblia.
Wengine watasema tupo kijijini hatuna uwezo wa kumiliki smartphone kwa sababu ya changamoto ya umeme. Upo sawa je hata biblia ya kawaida huna? Unayo soma NENO la Mungu.
Tuache uzembe, tuache uvivu, tuache visingizio, tuache mazoea, tujitoe kujifunza NENO la Mungu. Tukiwa na maarifa ya kutosha tutajua namna ya kuomba ipasavyo, tunaweza kuwa tunaomba vitu ambavyo hatukupaswa kuomba.
Umeanza hivi karibu kusoma NENO, ongeza juhudi, usije ukaishia njiani. Na wewe wa muda mrefu usisome kwa mazoea.
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255759808081.