Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, jina lipitalo majina yote dunia, litamkwapo na watakatifu mapepo hukimbia. Bila shaka umeamka salama, kama ipo changamoto inakukabili labda ya kuumwa ama ya kuunguliwa, Mungu bado ni mwema kwako.

Tunaposisitizana umhimu wa kujifunza NENO la MUNGU, ujue ni jambo la msingi sana katika maisha yako ya KIROHO. Roho Mtakatifu anajua ni jinsi gani watu wa Mungu wanapotezwa na hila za mwovu shetani kwa kukosa maarifa.

Sio jambo la kawaida biblia tunazo ndani ya simu/laptop zetu lakini tunazifungua siku za jpili, au ikitokea semina katikati ya wiki ndio tunapata muda wa kuifungua biblia baada ya kuambiwa fungua mstari fulani.

Maarifa tunayo wenyewe ndani ya biblia zetu, kama hujanunua biblia naamini simu umenunua. Hujaona umhimu wa biblia ya sh. 25,000 bali umeona umhimu wa simu ya 100,000, hili nalo la kujihoji kwanini huna biblia ya mkononi una simu/tablet.

Basi kama umeona umhimu wa kununua smartphone ya zaidi ya laki, fanya kupakua App ya biblia kutoka playstore ni bure kabisa, unaweza kupakua ya lugha yeyote unayoipenda wewe.

Jambo la kushangaza lingine ni kwamba, biblia zinachakaa kwa vumbi la kutoshikwa mara kwa mara. Na zingine mpaka zimivamiwa na panya kwa kusahaulika kabisa ndani ya droo zetu na ndani ya sanduku zetu.

Nafikiri gharama tuliyotumia kuomba Mungu alete mvua, nguvu ileile tuitumie kujiombea wenyewe na kuombea wengine ili Mungu alete uamsho ndani yao/yetu ya kusoma NENO lake.

Ajabu sana mtu ana ratiba ya kununua gazeti la kila siku na vitabu vingine, ila hana ratiba ya kusoma NENO la Mungu. Na ukute mtu yule hana hata agano jipya, kama analo ujue alilipata shuleni/kanisani kwenye mgao wa chama cha WaGidion.

Neno la Mungu ni dira ya mkristo, kila linakutokea sasa lilishaandikwa ndani ya biblia. Haijalishi lililokupata ni zuri au baya, limeandikwa ndani ya biblia yako unayoiona kama urembo.

Labda umekaa na kujifariji ya kwamba; biblia ni kwa ajili ya wakristo fulani wenye karama hiyo ya kusoma la hasha! Kusoma biblia sio kipaji ambacho anakuwa nacho mtu fulani tu.

Neno la Mungu ni chakula cha mkristo, hakuna mwenye kipaji cha kula badala yake kila mmoja anakula.

Katika group la wasap la Chapeo Ya Wokovu, tunaendelea na utaratibu huu wa kusoma NENO kila siku. Ambapo leo tupo kitabu cha 1 Nyakati 12, sio miujiza ila tumefika hapo.

Nakusihi sana utenge muda wako wa kujifunza NENO, usikubali kubaki nyuma. Tafuta rafiki/marafiki ambao watakuwa wanakuhamasisha kila siku kutenga muda kwa ajili ya kusoma NENO.

Marafiki hao wanapatikana Chapeo Ya Wokovu wasap group, unaweza kuungana nao leo kwa mawasiliano nitakayotoa hapo chini.

Mungu akupe ufahamu wa kujua umhimu wa NENO LAKE.

Samson Ernest.

+255759808081.