Haleluya mwana wa Mungu, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai. Siku nyingine tena Bwana ametuzawaidia wote ili tuendelee kumzalia matunda.

Kujifunza ni hiari ya mtu binafsi kuamua mwenyewe ajifunze jambo fulani au asijifunze kabisa hilo jambo.

Pamoja na uhiari huo, mtoto akiwa mdogo kila kitu yeye hulazimishwa, usipomlazimisha kula hatakula, usipomlazimisha kuamka aende shule hataenda, usipomlazimisha kuoga hataoga.

Wakati mwingine hafanyi hivyo kwa makusudi, wakati mwingine hajielewi, wakati mwingine hajui umhimu wa kile unachomlazimisha.

Utoto/uchanga wake ndio unamfanya awe hivyo, sio kana kwamba anakataa kufanya kile unapenda kwa makusudi. Hajui umhimu wa kile unamhimiza afanye, angejua usingesumbuana naye.

Mtoto huyu pamoja na unamkataza asitembee bila viatu, bado ukamkuta anatembea, mara nyingine sio anapenda sana au sio kana kwamba umemfundisha wewe. Bali mtoto huyu amefundishwa na watoto wenzake, anaona ni jinsi watoto wenzake wanavyopekua na kufukua michanga.

Mzazi hujamfundisha mtoto wako awe vile ila amefundishwa na watoto wenzie huko nje, anaona mbona mtoto mwingine anatembea peku na wala mzazi wake hamkemei.

Mtoto huyu hajui kuwa mtoto yule anatembea bila viatu kutokana na hali ya wazazi wake, hajapenda kuwa vile ila anajikuta analazimika kutembea bila viatu kutokana na umasikini wa wazazi/mzazi wake.

Jambo la kushangaza sana mtoto huyu huwezi kumwona akililia kutembea uchi, mara chache utamwona mtoto anakataa kuvaa nguo kabisa. Ukiona hivyo fuatilia watoto anaocheza nao, utagundua mchezo ni ule ule wa watoto anaocheza nao hupenda kushinda bila nguo.

Najua unajiuliza imekuwaje wewe sio mtoto, ila nakuelezea habari za watoto, ina maana wewe ni mtoto? La hasha! Biblia yangu inasema tusiwe kama watoto wachanga.

Tabia ya mtoto mchanga ni za kushangaza sana kutokana na uchanga wake, nimejaribu kukumbusha tabia za watoto ili unielewe kile nataka kusema hapa.

Kusoma biblia sio jambo la kusukumana kwa nguvu sana, kama kila mmoja atajua umhimu wa hili jambo. Utasema ina maana wewe tangu uokoke hujajua tu umhimu wa kusoma NENO la Mungu?

Swali zuri sana; hujui kabisa, ungejua ungepata muda wa kukaa chini na kuanza kujifunza NENO la MUNGU kila siku. Huenda hapo unajiona unajua ila huna muda wa kusoma NENO, labda mimi nikuulize; hivi ipo siku uliacha kula siku nzima kwa sababu ulibanwa sana? Ipo siku uliacha simu nyumbani siku nzima bila kupata shida moyoni kwa sababu ulikuwa bize sana?

Huenda kuna siku ulikuwa bize masaa kadhaa ukashindwa kula, huenda ulikuwa na haraka ukaacha simu nyumbani. Ila hayo yote hukuchukua siku mbili bila kugusa, nasema hivi; hukuacha kula siku mbili kwa sababu ulikuwa bize labda uwe umefunga.

Kumbe kuna vitu hatuwezi kuviacha kuvifanya hata tumechoka sana, au hata kama tupo bize sana, tunajikuta tunavifanya kwa sababu tunajua ni mhimu kwetu.

Vilevile suala na kusoma NENO, linawezekana ikiwa mtu mwenyewe atadhamiria kutoka ndani, dhamira hii inakuja pale mtu mwenyewe anapoona mazingira fulani yanamlazimu kila siku kufanya kile mhimu kwake.

Ndio maana nimekuandalia group la wasap, ambapo nia haswa ni kukulazimisha kufanya wajibu wako, najua hujazoea kuwa na marafiki wanaopenda kusoma sana biblia zaidi ya vitabu vingine. Ila kupitia group hili la wasap unapata marafiki wanaojua umhimu wa hili jambo.

Kutokana na kuwa na marafiki wa namna hii, utajikuta ile tabia yako ya utoto ya kuiga vitu ambavyo havikufai. Utaanza kuiga vitu vinavyofaa, utaanza kupandiwa tabia njema ya kujifunza NENO.

Tabia hii ukishapandiwa ndani yako alafu ikakulea vizuri, jua na wewe unaenda kumwambukiza mtu mwingine roho ileile iliyo ndani yako. Na mtu yule ataenda kumwambukiza mwingine, na mwingine anamwambukiza mwingine.

Mwisho wa siku tutaenda kuacha kizazi cha wanafunzi wa YESU Kristo, wanaopenda maarifa, wanaopenda kujitoa kila siku kwa ajili ya NENO.

Penda maarifa, maarifa yatakupa mwanga na mwelekeo kwa safari yako ya WOKOVU, upo upotoshwaji mwingi sana. Unahitajika uwe na miguu ya kujitegemea, huwezi kushinda na mchungaji wako kila saa, zaidi ya ibada za kanisani.

Sasa usipoweza kujisimamia kwa miguu yako mwenyewe, ni rahisi kuchukuliwa na hila za shetani, mpaka uje ugundue kuwa huko ulipo sio kwenu, utakuwa umetumiwa sana.

Usiache kusoma NENO la MUNGU, ukiona huna msukumo ndani yako lakini unapenda kuwa kama wenzako wanavyojitoa kwa ajili ya NENO. Ingia magotini umweleze Mungu, nenda na mzigo huu kwenye maombi, Mungu atakusaidia kabisa.

Usikae kama kinda wa ndege anayesubiria mama yake amletee chakula mdomoni, tafuta mwenyewe maarifa ya kukusaidia katika safari yako ya WOKOVU.

Mungu afungue ufahamu wako upate kuelewa umhimu wa hili jambo.

Samson Ernest.

+255759808081.