Haleluya, ashukuriwe Mungu wetu atupaye kushinda, ametupa kibali kingine cha kuiona tena siku ya leo. Fursa kwetu kwenda kufanya yale yatupasayo kutenda ili kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.
Kuna vitu lazima ukae chini utafakari kwa kina bila kuangalia wengine wanasema nini, unapojifunza maana yake umechagua kubadilika kadri unavyozidi kumjua Mungu wako. Inaleta maswali pale unapojifunza kwa kujionea mwenyewe alafu unaendelea na kufanya yale yale ambayo hayamo ndani ya maandiko Matakatifu.
Kujifunza kwako Neno la Mungu kuna maana gani kwako, na unajifunza ili iweje, ikiwa wewe mwenyewe unaona kabisa hapo ulipo ulikuwa unaamini kilicho nje na Neno la Mungu. Sasa umejua ulikuwa unashikilia na kuamini kitu tofauti, kinakushinda nini kubadili msimamo wako wa awali?
Haina maana wewe kuendelea kujifunza kitu kilekile kila siku alafu unaendelea kuwa vilevile sawa na asiyejifunza chochote. Huwa unajifunza nini kama umeendelea kubaki na mapokeo yako yaleyale ambayo mengine sio sahihi kwako kama mwamini mwenye safari ya kwenda mbinguni.
Neno la Mungu linapaswa kukubadilisha wewe, na si wewe kulibadilisha Neno la Mungu, shika hili sana ndugu yangu katika Kristo. Hatuwezi kuendelea kusoma Maandiko Matakatifu kila siku alafu tunaendelea kuamini mila na desturi zetu huku zinakinzana na Neno la Mungu.
Hatuwezi kuendelea kusoma Maandiko Matakatifu alafu tunaendelea kuamini mila na desturi zetu zinazoabudu miungu mingine, na wewe mwenyewe umeona Mungu akizuia hili la kuabudu miungu mingine zaidi yake yeye.
Vitu vingi sana hatukubali kuviachilia sijui tunafikiri tutapoteza kitu gani, wakati huo ndio ulikuwa wakati wetu wa kujenga upya uhusiano wetu na Mungu. Mungu anajaribu kusema na wewe kupitia Neno lake ili upate kuondoa yale mapokeo yako ya zamani yaliyo kinyume na Mungu.
Pamoja na Mungu kukusaidia kuliewa Neno lake, bado umefanya shingo ngumu kushikilia unayoamini wewe. Na wakati mwingine unatamani Neno la Mungu lifuate kama unavyotaka wewe.
Mungu wetu anajua kila mmoja ana lugha na kabila lake, lakini pamoja na hayo yote anatuweka katika mwenendo mmoja kupitia Neno lake. Maana Neno lake ni lilelile, linapokuambia usiibe limemwambia kila mwanadamu/mwamini wa jina lake asifanye hivyo.
Hakuna kusema mbona kabila langu linaruhusu, hakuna kusema mbona wazazi wangu hawaniambii chochote, hakuna kusema mbona mchungaji wangu anasema haina shida, hakuna kusema kanisa/dhehebu/dini yangu haikatazi wewe kufanya/kutenda kama unavyoona wewe ni sahihi.
Kujifunza kwako Neno la Mungu kukusaidie kujenga mahusiano mazuri na unayemwamini alikukomboa kwa damu ya thamani, kama unaamini ulikombolewa na mbuzi mweupe/mwekundu. Hapo utakuwa unapingana na Maandiko Matakatifu mwenyewe bila kuelewa unachoamini, vyema ukaacha kusoma Neno la Mungu kama hadithi fulani zilizopita miaka mingi.
Mungu ameweka utaratibu wa namna wa kuenenda katika njia moja ya kumpendeza yeye, watu wa kabila zote na mataifa yote. Tunapaswa kufanana tabia zetu na Yesu Kristo, ukimkuta mtu ulaya awe ana hofu ya Mungu kama yako, ukimkuta mtu nchi yeyote ya Africa awe tabia sawa na nchi za ulaya. Kwanini? Kwa sababu Baba yetu ni mmoja.
Mungu wetu amesema tusizini au tusifanye uasherati, unaenda sehemu nyingine wanafanya hivyo kwa sababu mila na desturi zao zinaruhusu hilo. Moja kwa moja mtu anayejua Neno la Mungu utajua wamepotea njia, bila kutafuta ushahidi wowote utaelewa wanahitaji msaada wa kuondolewa hapo walipo.
Swali la msingi kwako, shida inakuwa wapi unaposoma Neno la Mungu lakini bado hutaki kubadilika? Bado umeshikilia mapokeo ya dini/dhehebu lako. Dhehebu/dini yako ndio Neno la Mungu au dhehebu/dini yako inapaswa kufuata Neno la Mungu linasemaje. Lazima ujiulize hilo swali la msingi kama kweli upo serious na safari yako vinginevyo utaendelea kujifariji na kushupaza shingo.
Jiulize kwanini zamani hukujua kama imeandikwa, ila sasa umejua imeandikwa ndani ya biblia usifanye hivi na vile. Ikiwa wewe unamwamini Kristo kwanini kuna vitu baadhi unavikataa alivyovifanya Kristo kama ishara njema kwetu tufanye.
Mungu hawezi kutuletea Roho Mtakatifu alafu wewe unayesema Yesu ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Ukamkataa Roho Mtakatifu na kuamini ya kwako, na kila siku unasoma watu walijazwa Roho Mtakatifu siku ya pentekosite wakanena kwa lugha mpya.
Ufike kipindi uchukie hali uliyonayo, inakuwaje unasoma Maandiko Matakatifu yanakuonya na kukuelekeza na kukufundisha namna ya kuenenda katika njia sahihi. Ila wewe hutaki na unaendelea kusimamia yale unayojua wewe ni sahihi kwako, hatuendi hivyo ndugu, tunaenda kwa maelekezo maalum kutoka Mungu mwenyewe.
Kweli ikuweke huru na urekebishe makosa uliyokuwa unafanya ukiamini Mungu anakutaka uenende hivyo. Kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu, uzidi kuona mabadiliko ndani yako, yote unayojifunza yaweke katika matendo na ujaribu kadri ya uwezo wako huku ukimwomba Mungu akusaidie. Ataachaje kukusaidia na wakati yeye mwenyewe ametoa agizo hilo, lazima atakusaidia ukimwamini kuwa anaweza kwako.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.