Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa imempendeza Bwana kutupa kibali cha kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye maana ni mwenza wa yote, kutupa fursa ya kwenda kufanya yatupasayo kumzalia matunda.

Tumezoea kuona marafiki wanaoaminiana vizuri huwa wanafanya mambo mengi pasipo mashaka, lakini inatokea wakati mwingine mmoja wapo akaonekana sio mwaminifu kama mwenzake alivyokuwa anamwona. Hapo ndipo utasikia zile kauli, nilikuamini na kukuona ni mtu mzuri kumbe ulikuwa umevaa ngozi ya kondoo.

Inaonekana ni kauli ya kawaida ila ina ujumbe mzito iliyobeba ndani yake, kwa mtu aliyetendewa jambo ambalo hakutegemea kama angetendewa na mtu anayemwamini kiasi kile. Huyu mlalamikaji anashindwa kutambua kuwa alijiaminisha haraka kwa mtu ambaye hajafanya uchunguzi vizuri.

Ukimwelewa vizuri na ukamwamini ndugu/rafiki yako, hata kama ukute watu wanamsema vibaya kiasi gani, moja kwa moja utajua ni chuki zao binafsi au utajua wanachosema kibaya juu yake ni sahihi. Hata kama kinachosemwa ni kibaya juu yake hutokuwa na mashaka na maneno yao, wala hutokubali wakupotoshe kama wanamsema kinyume na unavyomjua.

Ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu, mtu anayemjua Mungu wake vizuri hawezi kufika hatua akamwona Mungu hawezi kumtendea jambo fulani linalomsumbua, kwa sababu tu hakumjibu kama alivyokuwa anataka. Kiwango chetu kidogo cha kumjua Mungu ndicho kinatufanya tuikane imani yetu, usishangae leo kumwona mkristo akiwa anapanga safari kwenda kutafuta msaada wa kiroho/kimwili kwa waganga wa kienyeji.

Usishangae kumwona mkristo akiikana imani yake, na kuamua kugeukia imani nyingine isiyomwamini Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Shida hii inakuja kwa wale walioona sifa kuitwa mkristo inatosha, pasipo kujua wanapaswa kuweka juhudi kumjua zaidi Mungu wao.

Sio ajabu leo mtu kufiwa na mume/mke wake, na wokovu wake ndio unakuwa umeishia hapo baada ya kuondokewa na mwenzi wake. Sio ajabu leo kaka/dada kuachwa na mchumba wake, na habari ya wokovu inakuwa imeishia hapo. Sio ajabu leo mtu kupoteza mali zake, na habari za wokovu zinakuwa zimeishia hapo.

Wakati huu wa majaribu makali kwake ndio ulikuwa wakati wake mzuri watu wengine wasiomjua Kristo kuliinua jina lake, lakini anakuja mtu anampotosha na kumwacha Mungu wake wa kweli. Usije ukafiri wana wa Israel kumwambia Haruni awatengenezee sanamu wapate kuiabudu baada ya Musa kukawia, usije ukafikiri hawakuona matendo makuu ya Mungu tangu wapo Misri na mpaka kuvuka bahari ya shamu.

Walikuwa wanaelewa vizuri ila hawakuwa na imani kwa Mungu wao kuwa anaweza nyakati zote, hata kama Musa alichelewa kurudi bado wangetambua Mungu wao ni mkuu na muumba wa vyote. Yaani nasema Kumwelewa tu Mungu kuwa alikuponya ugonjwa alafu ukaishia hapo, hiyo haitoshi. Siku ukiumwa zaidi ya ulivyoumwa mwanzo na ukaombewa huku na kule bila majibu, itafika saa utasema ulikosea kusema Yesu Kristo anaponya.

Kumwelewa Mungu wetu vizuri ni kwa kusoma Neno lake na kulitafakari kila wakati, pasipo kufanya hivyo ndugu yangu katika Kristo. Nakwambia upo wakati ambao watu watataka wathibitishe imani yako kama ni ya kweli, ni imani iliyosimama kweli mbele za Mungu au ni maneno tu.

Usifikiri Daniel kukubali kutupwa Kwenye zizi la simba, huku akiwa na msimamo wake wa kutoabudu mungu mwingine zaidi ya Mungu wake. Usije ukafikiri ilikuwa ni imani ya mkristo wa Jumapili/Jumamosi tu, ilikuwa ni imani ya mtu anayemjua Mungu wake vizuri sana.

Unakataa nini wakati kuna dada zetu kibao wanatafuta kazi akiambiwa ili apate kazi, ni lazima wafanya ngono na anayetoa nafasi za kazi. Wanakuwa tayari kutoa miili yao kufanya uasherati/uzinzi, na bado wanaingia makanisani kusema Yesu ni Bwana, na wanatoa shukrani mbele ya madhabahu kuwa Mungu amewasaidia kupata kazi. Kumbe kilichomsaidia kupata kazi ni kutoa mwili wake utumiwe na mtu mwingine kwa ngono.

Kama kweli unampenda Yesu Kristo, unapaswa kumjua vizuri kupitia Neno lake, usibaki kusema mchungaji wangu alisema hivi. Unapaswa kujua wewe kama wewe Neno la Mungu linasemaje, kujua kwako kuna kupa nafasi kubwa kusimama na miguu yako sehemu yeyote ile. Hata itokee mchungaji wako ameasi imani, bado utaendelea kusema Yesu ni mzuri, kwa sababu hukuwa na imani inayomwegamia mchungaji wako.

Soma Neno la Mungu kwa bidii zote, hakikisha unamtumia Roho Mtakatifu vizuri katika eneo hili la kusoma Neno la Mungu. Unapaswa kusimama wewe kama wewe, kama ilivyokuwa kwa Luthu enzi za Sodoma na Gomora. Hata kama nchi nzima ilimwasi Mungu, bado Luthu na wanaye wawili walisimama katika kweli ya Mungu, hii ni kwa sababu walimjua na kumtii Mungu wao.

Hata kwako inawezekana kama utakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu Mungu, usiwe na imani nusu nusu ya kuegamia kwenye vitu. Siku vitu vikiisha utamwacha Yesu wako, kwa sababu ulikuwa umemwamini ulivyokuwa na kazi nzuri, familia nzuri, mke/mume mzuri na biashara nzuri. Lakini hivyo vitu vilipopotea na Yesu wako naye akapotea kwako.

Bila shaka mpaka hapo utakuwa umeelewa na kuona umuhimu wa kusoma Neno la Mungu, husomi Neno la Mungu ili uwe na uwezo wa kujibishana na watu. Unasoma kwa faida yako mwenyewe, itakayokusaidia kusimama kwa miguu yako hata kama hutakuwa na uwezo wa kuongea.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.