“Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia”, Mwa 33:4 SUV.

Kitendo cha Yakobo kuchukua baraka ya uzaliwa wa kwanza, kwa Esau ilimkaa vibaya sana na kupelekea ugomvi kati ya Yakobo na Esau, baada ya miaka mingi kupita tunaona Yakobo alitaka kurejea kwenye nchi yake.

Kabla ya kufika alianza kutengeneza mazingira ya kupatana na ndugu yake Esau, Yakobo alimaanisha haswa kwa kile alikuwa anataka Esau akifanye kwake, alitaka msamaha kwa ndugu yake Esau, aliwatanguliza watu kwenda kumsihi Esau amsamehe.

“Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu. Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, nami nina ng’ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako”, Mwa 32:3‭-‬5 SUV.

Ujio wa Esau kwa Yakobo na kumkumbatia kwake ilikuwa ni ishara njema sana, moyo wa Esau wa kirafiki ulikuwa ni jibu la Mungu kwa maombi ya Yakobo.

“Uniokoe sasa na mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama pamoja na wana”, Mwa 32:11 SUV.

Tunajifunza nini hapa? Lipo kubwa sana la kujifunza kwenye maisha yetu haya. Wapo watu wanatukosea, wapo watu tunawakosea, tunahitaji kutafuta suluhu kwa namna yeyote ile, tunamwona Yakobo aliandaa zawadi nzuri ya kumpa Esau.

Zawadi hizo ilikuwa ni kuonyesha kutubu na kumtaka asahau yaliyopita, tunaweza kusema aliitafuta toba kwa gharama kubwa sana, ambapo alikuwa tayari kutoa mali zake nyingi ili moyo wa Esau umwachilie.

Yesu alishalipa gharama kwa ajili ya dhambi zetu ila tunapaswa kutafuta kupatana na wale ambao tuliwakosea katika maisha yetu, wapo watu tuliwaumiza mioyo yao na kuwakimbia, tunahitaji kurejea na kuomba msamaha.

Yupo mwanamke alipewa mimba na mwanaume, mwanaume huyu akawa amekimbia ujazito, mwanamke huyu anayo maumivu mengi, ya kuachiwa mtoto na kukimbiwa akiwa kwenye hali ngumu ya ujauzito. Mwanaume wa namna hii anahitaji kurejea kuomba msamaha, hata kama kila mtu ana maisha yake.

Kukosea kupo, tunahitaji kurejea kuomba msamaha, tukiwa na nia hii njema Mungu ataambatana nasi kutupatanisha na wale tuliowakosea, bila kujalisha miaka mingapi imepita, na bila kujalisha wale tuliowakosea wametusamehe, tunahitaji kurejea kwao kuomba msamaha.

Usiufanye moyo wako mgumu, ulimkosea ndugu yako, mpendwa mwenzako, nenda kamwombe msamaha, kufanya hivyo utakuwa umefanya jema sana mbele za Mungu na mbele ya yule uliyemkosea.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081