“Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu”, Gal 3:28 SUV.
Hapa Paulo aeleza wazi na kuondoa tofauti zote za kikabila, kirangi, kitaifa, kijamii na kijinsia kuhusu uhusiano binafsi wa mtu na Yesu Kristo.
Ile Mimi wa kabila fulani, Mimi wa jinsia fulani, inaondolewa pale mtu anapomwamini Yesu Kristo. Wote wanakuwa watoto wa Baba mmoja bila kujalisha rangi, kabila, na jinsia yake.
Wote waliompokea Yesu ni warithi sawa, neema ya uzima sawa, ile ahadi ya Roho sawa, na kuhuishwa katika mfano wa Mungu sawa.
“Mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba. Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote”, Kol 3:10-11 SUV.
Upande mwingine kuhusu usawa mwanaume atabaki kuwa mwanaume, na mwanamke atabaki kuwa mwanamke.
Zile nafasi zao walizopewa na Mungu katika familia au jamii haziwezi kubadilika kwa mjibu wa maandiko.
“Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili”, Efe 5:22-23 SUV.
Usawa huu hauondoi ule uwajibikaji wa kila mmoja wetu kutokana na nafasi yake kijamii au kifamilia, mwanaume anapaswa kusimama katika nafasi yake na mwanamke vivyo hivyo.
Tunaporudi katika kumwamini Yesu, wote tunakuwa sawasawa, sio kwa sababu ni mwanamke basi atakuwa tofauti na yule mwanaume. Wote ahadi alizoziahidi Mungu kupitia neno lake wanazipata sawa.
Tunapaswa kuzingatia kuwa mbele za Mungu wote ni sawa, haijalishi kabila lako au jinsia yako, wote tupo sawasawa.
Usije ukafikiri kabila fulani lina upendeleo mkubwa kuliko kabila fulani, hiyo haipo mbele za Mungu kwa wale waliomwamini Yesu Kristo.
Usije ukajenga dhana kuwa wanawake wana nafasi fulani ya upendeleo mbele za Mungu, au wanaume wana nafasi kubwa mbele za Mungu kuliko wanawake, hiyo haipo mbele za Mungu.
Isipokuwa hatuwezi kuwa sawa kimajukumu kutokana na yale majukumu aliyoyagawanywa na Mungu kijamii na kifamilia, Mungu ametugawanya vizuri kati ya mwanaume na mwanamke.
“Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”, 1 Pet 3:1, 7 SUV.
Zingatia wanawake au wanaume au kabila fulani hawana neema zaidi kuliko wengine, au wanajazwa Roho Mtakatifu au wanaongozwa zaidi kuliko wengine. Wote tumempokea Roho Mmoja, Ahadi sawa, na neema sawa.
Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081