Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, ni wakati mwingine tena wa kushirikishana yale mambo mhimu kutoka ndani ya Biblia.

Leo nasukumwa kuzungumza nawe kuhusu kusikia, hasa kusikia ujumbe wa Mungu kupitia Neno lake. Ambao hupitia kwa watumishi wake, au kwa kusoma mwenyewe Neno la Mungu.

Watumishi wa Mungu wanaweza kukuhubiri sana kweli ya Mungu, lakini ukawa husikii wala huelewi chochote kuhusu kile unahubiriwa.

Unaweza kusoma sana Neno la Mungu, lakini ukawa husikii, yaani ukawa hufuati vile unaelekezwa na Neno la Mungu.

Muda mwingine sio kwamba unafanya makusudi, ipo roho mbaya ndani yako iliyo kinyume na mpango wa Mungu inayofanya kazi.

Kuelewa kama kuna roho isiyo ya kawaida ndani yako inaweza isiwe kwa haraka sana, ila kuna dalili utakuwa nazo.

Dalili hizo zinaweza kuwa, utaelezwa kweli ya Mungu, ila utaipuuza, na utakuwa unathamini sana mambo ya dini yako kuliko Mungu.

Upo tayari kutetea dini yako kuliko Yesu Kristo, upo tayari kujitoa kwa ajili ya dini yako kuliko kusudi aliloweka Mungu ndani yako.

Ili uweze kutoka eneo hilo, sikio lako lipaswa kuzibuka, ndio sikio lako la ndani linapaswa kuzibuka ili uweze kusikia iliyo kweli ya Mungu.

Sikio lako la ndani likishazibuka, hutojisikia vibaya unapoambiwa iliyo kweli ya Mungu, hutoona unasemwa vibaya pale unaposikia mtumishi wa Mungu akihubiri injili ya kweli.

Sikio lako la ndani likizibuka, utasoma Neno la Mungu na kulielewa vizuri, na ukishaanza kulielewa, utaanza kulipenda kulisoma bila kusukumwa na mtu yeyote.

Unapaswa kuombea sana hili, mwambie Mungu azibue masikio yako ya ndani uweze kusikia mafundisho ya Neno lake kupitia kwa watumishi wake, uweze kuelewa vizuri zaidi Neno lake unapolisoma. Bila hivyo utakuwa huelewi unachosoma, na utaona ni mzigo kwako kusoma Neno la Mungu.

Rejea: Naam, hukusikia; naam, hukujua; naam, tokea zamani sikio lako halikuzibuka; maana nalijua ya kuwa wewe watenda kwa hila nyingi, nawe umeitwa mkosaji tangu kuzaliwa kwako. ISA. 48:8 SUV.

Upo umhimu mkubwa sana wa kuzibuka masikio yako ya ndani, kutakufanya uwe vizuri zaidi kuliko ulivyokuwa mwanzo.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Website: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081