Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za muda huu ndugu yangu katika Kristo, hongera kwa ushindi wa siku ya leo. Ni ushindi mkubwa sana kufikia wakati huu, unapaswa kumshukuru sana MUNGU kwa nafasi hii adimu.
Kila mmoja amepewa uwezo wa kujua mema na mabaya ilimradi ana akili timamu, kila mmoja akitumia akili yake ipasavyo. Kuna uwezekano mkubwa sana kuibua mambo makubwa ambayo yatakuwa alama njema kwa dunia nzima.
Mungu kutupa akili za kuweza kufikiri vitu na kuunda mambo mbalimbali, hii ilikuwa ni zawadi tosha kwetu kutoka kwa Mungu. Kuweza kuzitumia akili zetu ipasavyo kutuzalia matunda mema aliyoyatarajia kwetu.
Yapo mambo mengi yameharibika kwa kushindwa kutumia uwezo wa akili tulizonazo ndani yetu, huenda tungelijua hili mapema ingewasaidia wengi wetu kutokufanya vitu bila kufikiri kwa kina.
Laiti tungejua madhara ya kufanya mzaha kwa jambo fulani katika maisha yetu, tungekuwa makini sana katika ujana wetu. Vilevile tungetumia ujana wetu vizuri sana wakati bado tuna nguvu za kumtumikia Mungu.
Nina uhakika tusipotumika vizuri sasa hivi mbele za Mungu wakati bado tuna nguvu za kutosha, itafika wakati tutaukumbuka ujana huu.
Nina uhakika tusipotumia akili zetu vizuri kujilinda na vyakula vya ovyo, tutajikuta siku za mbeleni tukiwa na afya mbovu. Ambazo baadaye tutashindwa kufurahia matunda ya mafanikio yetu kwa kuwa na afya mbovu.
Nina uhakika tusipotumia akili zetu ipasavyo kulinda umoja wa familia zetu usipotee, itafika wakati tutajuta kwanini hatukutengeneza mahusiano mazuri na familia zetu.
Nina uhakika tusipotumia akili zetu vizuri, kujiwekea mipango mizuri ya maisha yetu, kwa kuweka misingi mizuri ya kifedha na miradi mbalimbali. Tutajikuta tukiwa kwenye hali mbaya kiuchumi na wakati mwingine kugeuka ombaomba, wakati tulikuwa na uwezo wa kuepukana na hilo mapema.
Unaweza sasa hivi usijue kuwa kazi yako unayofanya ni kianzio kizuri cha wewe kutengeneza misingi ya kutoka kwenye utumwa, na kuingia uhuru wa kifedha. Utafanya kazi tu ilimradi unalipwa, ila baada ya kuacha hiyo kazi utakuwa umebaki kwenye utumwa uleule.
Yapo maeneo mengi sana tunapaswa kutumia uwezo wa akili alizotupa Mungu, wakati mwingine tunaweza kubaki kwenye hali fulani duni kwa kushindwa kutumia akili zetu vizuri.
Usipotumia akili yako vizuri sasa hivi, unaweza kuja kugundua ulifanya makosa makubwa kwa kutokujua kwako. Na wakati huo tayari umekuwa mzee, na hauna uwezo tena wa kurudi nyuma enzi zako za kuweza kukimbizana.
Usifanye vitu kama mtu asiyejua kitu kabisa, pangalia vitu vyako wakati una nafasi ya kufanya hivyo, hili ni jambo la busara sana katika maisha yako. Una uwezo wa kuwatengenezea wanao misingi mizuri ya kuja kuwaachia urithi mzuri, fanya hivyo sasa.
Hili tunajifunza kwa kiongozi huyu ambaye tunaenda kuona jinsi alivyotumia busara/akili. Kuwatanya wanaye maeneo mbalimbali ili wapate kurithi sehemu alizowaandalia.
Rejea: Rehoboamu akamsimamisha Abiya, mwana wa Maaka, kuwa mkuu, mtawala kati ya nduguze, kwa kuwa aliazimia kumtawaza awe mfalme. Akafanya kwa akili, akawatawanya wanawe wote kati ya nchi zote za Yuda na Benyamini, katika kila mji wenye boma; akawapa vyakula tele. Akawatafutia wake wengi. 2 NYA. 11:22-23 SUV.
Sijui kama unanipata vizuri hapa, ipo hivi, unajua mtoto uliyemzaa leo baada ya miaka mitano ijayo utahitaji uwe umempeleka shule. Ila kwa sasa huna mipango yeyote ya kumtengenezea misingi mizuri mwanao, zaidi unakula tu starehe kwa kiasi cha fedha unachopata. Inapofika muda wa mtoto kwenda shule unaanza kuhaha huku na kule.
Lakini tukiwa na jicho la kuona mbali na kujua wajibu wako ni nini, tutakuwa makini sana kama Rehoboamu alivyofanya jambo la busara kwa watoto wake.
Najua akili unazo na Mungu amekupa, hebu zitumie sasa kuepuka majuto, bali ziwe matokeo ya furaha kwa kuwa uliwaza vyema, ukatenda vyema.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Endelea kutembelea mtandao wetu,
Chapeo Ya Wokovu.
WhatsApp +255759808081.