Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, matumaini yangu unaendelea vyema kabisa.
Karibu tushirikishane mambo machache ya Mungu, naamini utaondoka na kitu kupitia tafakari hii.
Wengi wetu tuna mazoea mabaya sana katika kazi zetu za kila siku, tunafanya mambo kwa ulegevu katika nafasi zetu. Tukijua tukifanya kwa bidii sana tutawanufaisha sana waliotuajiri kwenye kazi hizo.
Ndio maana unaweza kuona wapo watu makazani wanafanya kazi kwa bidii sana, na wapo wafanyakazi wanafanya kazi kwa mkono mlegevu sana. Ila inapotokea mwenzao amepandishwa daraja kwa bidii yake ya utendaji kazi, waanza kusema amependelewa.
Wengine tumepewa nafasi ndogo tu lakini tumeshindwa kuzitumia kwa kupuuza baadhi ya mambo madogo. Lakini nafasi hizohizo wenzetu wamezitumia vizuri na wamefika mbali sana kimafanikio.
Ulipo unaweza kujitofautisha na wote mnaofanya nao kazi kwa bidii yako, haijalishi kazi mnayofanya wengi wanaidharau sana. Nakusihi sana wewe uifanye kwa umakini na kwa ufanisi mkubwa sana.
Haijalishi unafagia au kudeki kwenye ofisi za watu, fanya usafi kiasi kwamba boss akiingia ajiulize mara mbilimbili kwa jinsi ulivyosafisha ofisi yake.
Haijalishi upo eneo fulani la chini sana, fanya kwa umakini sana, kupitia hali hiyo ya chini Mungu atakuinua humohumo. Mpaka wale mliokuwa nao watabaki kusema tulikuwa naye huyu miaka kadhaa iliyopita, wakati huo haupo nao tena.
Hata kwenye masomo, kama Mungu amekufungilia mlango wa kusoma, jitahidi sana kujitofautisha na wengine kwa bidii yako ya masomo. Usifanye utani na maigizo katika eneo hilo la masomo, fanya vizuri kwa manufaa yako.
Kila mmoja akiwajibika kwenye eneo lake dogo alipo, dunia itakuwa bora sana kwenye nyanja mbalimbali. Kupuuza kwetu vitu, kumefanya kuharibika kwa kazi nyingi sana tunazopewa na waajiri wetu.
Bidii ile ile iwe pia katika mambo ya Mungu, hajailishi upo katika nafasi gani katika nyumba ya Bwana. Unapaswa kuitenda kazi ya Bwana kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote. Kufanya hivyo utamletea Mungu sifa na utukufu maeneo mengi sana.
Hakuna mtu yeyote aliye siriaz na mambo ya Mungu, Mungu akamtupa kwenye huduma yake. Yeyote anayemtumikia Mungu kwa mkono usio mlegevu, huinuliwa maeneo mengi sana katika maisha yake.
Haya tunajifunza kutoka kwa mtumishi wa Mungu Uzia, ambaye naenda kukupitisha kwenye maandiko uweze kuona bidii yake.
Rejea; Na Waamoni wakampa Uzia zawadi; likaenea jina lake mpaka pa kuingilia Misri; kwa kuwa akaongezeka nguvu mno. Tena Uzia akaujengea Yerusalemu minara, penye lango la pembeni, na penye lango la bonde, na ugeukapo ukuta, akaitia nguvu. Akajenga minara tena nyikani, akachimba mabirika mengi, maana alikuwa na ngombe tele; katika Shefela pia, na katika nchi tambarare; tena alikuwa na wakulima na watunza mizabibu milimani, na katika mashamba ya neema; maana yeye alipenda ukulima. 2 NYA. 26:8-10 SUV.
Hizo ndizo zilikuwa sifa za Uzia nyakati za utawala wake, je mimi na wewe tunaweza kuleta msaada kwa wengine kupitia kazi zetu tunazofanya. Au tunafanya kwa kulipua ilimradi siku ziende tulipwe mishahara yetu? jibu unalo mwenyewe ndugu.
Nikutakie wakati mwema, tukutane tena wakati mwingine.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com