“Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi”, Mt 25:1 SUV.

Mfano wa wanawali kumi unasisitiza kwamba waamini wote wanapaswa au wanalazimika siku zote kuangalia hali zao za kiroho, kwa kuzingatia kuwa Kristo atarudi wakati wowote au wakati usiojulikana.

Wakristo tunapaswa kudumu siku zote katika imani sahihi ili wakati utakapofika, siku na saa itakapowadia tuweze kupokelewa na Bwana Yesu.

“Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa”, Mt 25:10 SUV.

Kushindwa kuwa katika uhusiano mzuri wa binafsi na Bwana Yesu, wakati atakapokuja hutaweza kwenda naye katika ufalme wake kwa sababu ya mahusiano yako mabaya na yeye.

Kitu kinachotofautisha mpumbavu na mwenye hekima ni kushindwa kwa mpumbavu kutambua kuwa kurudi kwa Bwana Yesu kutakuja pasipo kutarajiwa na mtu yeyote, wakati ambao hautatanguliwa na dalili fulani za waziwazi.

“Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa”, Mt 25:13 SUV.

Kristo anaonyesha wazi kuwa sehemu kubwa ya kanisa haitakuwa tayari wakati wa kurudi kwake (Mt 25:8-13). Hivyo, Kristo anaweka wazi kuwa hatangojea mpaka watu wote au makanisa yote yawe tayari kwa ajili ya kuja kwake.

Tunapaswa kufahamu kuwa wanawali wote waaminifu na wasio waaminifu, walijiwa ghafla na bwana harusi. Wale waliokuwa wametunza mafuta yao, taa zao zilifanya kazi na kupata kibali cha kuingia kwenye harusi na mlango ukawa umefungwa.

“Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao”, Mt 25:5‭-‬7 SUV.

Mfano huu wa wanawali kumi unawahusu hasa wale waamini wanaoishi kabla ya wakati wa dhiki kuu na si kwa wale watakaoishi wakati wa dhiki kuu, ambao watapokea ishara nyingi kabla ya kurudi kwa Kristo mwishoni mwa kipindi cha dhiki kuu.

Tunapaswa kuwa tayari wakati wote, siku zote, saa yeyote, ili Bwana wetu atakapokuja tuwe tayari kwenda pamoja naye, tusiwe kama wale wanawali wapumbavu, tuwe kama wanawali wenye busara.

Watu ambao tumekaa tayari kumgonja Bwana Yesu, mkao huo utatusaidia kujenga uhusiano mzuri na Bwana wetu katika maisha yetu yote.

Mwisho, nikualike kwenye kundi la wasap la kusoma neno la Mungu kila siku na kupata nafasi ya kutafakari na kushirikisha wenzako kwa kile ulichojifunza. Ili uweze kuunganishwa wasiliana nasi kwa wasap +255759808081.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest