Ndugu kama ulikuwa hujui uhusiano wa Magendo huwa upo, leo utaenda kuufahamu, twende pamoja katika somo hili utaelewa namaanisha nini ninaposema uhusiano wa Magendo.

Kabla ya kulalamika wadada ni wabaya, kabla hatujawatupia lawama wakaka, tunapaswa kujiuliza mahusiano tunayokuwa nayo au tunayoanzisha huwa yanamtukuza Mungu au huwa yanasababisha jina la Bwana litukanwe.

Dada anaanzisha uhusiano kwa siri na kaka/mwanaume, anaenda guest house kwa siri kufanya uasherati. Wanatoka kwa siri, hapa wanakuwa wanafanya vitendo hivi kwa kificho, yaani wanaficha uhusiano wao usijulikane na watu.

Dada anaenda kwa kaka, anaingia kwa kificho kwa kaka au mwanaume, baada ya kumaliza uchafu wao, dada huyu huyu anatolewa kwa siri/kificho. Tena anatolewa wakati wa giza nene, inaweza ikawa ni alfajiri sana au usiku.

Vile vile kaka, anakuwa na dada kwa siri, wanafanya kila kitu kwa kificho kikubwa, mchana wanaonekana kama vijana wanaoheshimiana sana. Nyuma yake wanafanya vitendo vichafu sana, huku wakijipongeza kwa vificho vyao, wakijiona wao ni wajanja wa kuficha siri.

Wanaweza wakawa wanasali pamoja, wanaweza wakawa wanasali tofauti, wanaweza wakawa wanatoa huduma pamoja. Vyovyote vile ila wanakuwa wanafanya uchafu pasipo watu wengi kujua, wao wawili na marafiki zao wachache wanakuwa wanajua uhusiano huo.

Mahusiano/uhusiano wa namna hii unaitwa uhusiano wa magendo, uhusiano wa vificho, uhusiano usiopaswa kujulikana na wazazi, watumishi wa Mungu, washirika wenzake.

Kama hujui magendo yakoje, yapo hivi, ni kitu kinachokatazwa na serikali au jamii ila watu baadhi wanakuwa wanapenda kukitumia hicho kitu.

Mfano, bangi haipaswi kulimwa wala kutumiwa katika nchi yetu ya Tanzania, pamoja na haipaswi kulimwa, bado kuna watu wanalima na wengine wanakuwa wanaitumia. Kulima bangi, hicho ni kilimo cha magendo, na kusafirisha bangi huo unaitwa usafirishaji wa bidhaa ya Magendo.

Huwezi kukuta mtu analima bangi katika mazingira ya wazi, wala huwezi kukuta bangi ikiuzwa mazingira ya wazi, na wala huwezi kukuta bangi inasafirishwa kwa uwazi kama vitu vingine. Maana ni kitu kinachokatazwa na serikali yetu.

Magendo yapo pia kwenye mahusiano, mahusiano yanayoanzishwa kwa siri huku waanzishaji hao wakijua wanachokifanya ni kosa. Ndio watafanya kwa vificho vikubwa wasiweze kuonekana kwa watu wengine.

Mahusiano haya ya Magendo ndio zimepatikana mimba humo, mimba zilizokataliwa na wahusika, mimba zilizoleta maumivu makali kwa wadada wengi.

Mahusiano haya ya Magendo ndio yamesababisha watoto wengi hawajulikani baba zao ni akina nani ila mama zao ndio wanafahamika.

Mahusiano haya ya Magendo, mengi yamesababisha kuongezeka idadi ya watoto wa mtaani(chokaraa) japo sio kila mtoto wa mtaani ametokana na mahusiano ya Magendo.

Mahusiano haya ya Magendo, ndio yameleta msemo wa wanaume/wanawake wote ni wale wale, hapo mtu baada ya kujeruhiwa vibaya na mahusiano ya Magendo.

Hebu we fikiri, dada ameingizwa kwenye nyumba ya mwanaume kwa vificho, na akatolewa kwa vificho. Huyu anapaswa kumlaumu nani siku likimtokea baya? Anashindwa kujiuliza huwa tunaingizwa wangapi humu kwa mtindo kama wangu?

Dada acha mahusiano ya Magendo ni kosa kubwa mbele za Mungu, Kaka acha mahusiano ya Magendo ni kosa kubwa mbele za Mungu.

Leo utashupaza shingo yako ukaendelea kufanya hayo mauchafu yako kwa Magendo, ila uwe na uhakika hayo magendo yako yakishakushinda. Hata tusiojua lazima tutajua tu.

Fanya kwa siri, msafirishe dada wa watu kwa siri, mwingize kwako kwa siri, mwingize nyumba za wageni kwa siri. Maana si Magendo? Yakishakuharibikia huko uwe mpole, asiwepo wa kumtupia lawama.

Na wewe kubali kuwa biashara ya Magendo, nenda kwa mwanaume kwa siri, fanyeni uchafu wenu wote kwa siri. Maana wewe si bidhaa ya Magendo! Siku ukipewa mimba, siku ukiachiwa mtoto wako hapo, usianze kulalamika, ulikubali mwenyewe.

Sikia haya, acha hizo tabia, Mrudie Mungu wako kabla una nafasi ya kufanya hivyo. Usisubiri maji yakufike shingoni, wakati ambao huna uwezo wa kujiokoa, Mungu wetu ni mwingi wa rehema atakusamehe.

Mwenye masikio na asikie maneno haya, na mwenye kudharau na adharau haya maneno. Binafsi nimenawa mikono yangu, nimekuambia usiwe bidhaa ya Magendo, nimekuonya usifanye biashara ya Magendo.

Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
WhatsApp: +255759808081.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com