Haleluya, atukuzwe Yesu Kristo kwa matendo yake makuu katika maisha yetu ya kila siku.
Kumwelewa Mungu ni kazi sana ila ukiamua kuwa na mahusiano naye ya karibu, una nafasi kubwa sana kuendelea kujifunza Neno lake ili uendelee kujenga ufahamu wako.
Kumwelewa Mungu inakupa nguvu hata pale unaposhutumiwa, kwa makosa usiyotenda mbele za Mungu. Utakuwa na ujasiri wa kukiri na kueleza ukuu wake katikati ya shida yako, kwa sababu unajua jinsi alivyo mkuu.
Hakuna mtu ataweza kukujaza maneno mabaya kuhusu Mungu, utaelewa Mungu wako si vile wanakusema watu na kumfikiria wao, kutokana na hali uliyonayo.
Utakuwa na maelezo ya kutosha hata pale unapojikuta upo peke yako, ukishamjua Mungu huhitaji tena watu kukuunga mkono kwa lile unaloona litapoteza uhusiano wako na Mungu.
Kwa akili za kibinadamu tunaweza kuona kipo sahihi, lakini wewe uliye na uhusiano mzuri na Mungu wako. Yapo mengi utayatambua kuwa ni uongo, hata kama yanafanana na ukweli.
Utawezaje kufika kiwango cha juu cha kumjua Mungu wako vizuri bila kuyumbishwa na mtu, ni kuamua kuwa na bidii yako na kujenga nidhamu katika kulisoma Neno la Mungu kwa bidii. Kadri unavyozidi kufanya hivyo taratibu utaanza kuona mabadiliko ndani yako.
Wakati mwingine natamani kiwango alichokuwa nacho Ayubu cha kumjua Mungu, isipokuwa sitamani jaribu gumu alilopitia.
Kuna maeneo unaweza kujifunza kwa mtumishi wa Mungu Ayubu, utaona imani aliyokuwa nayo kwa Mungu ilikuwa ni pana sana.
Rejea; Yeye hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu, Na kuutundika ulimwengu pasipo kitu. Huyafunga maji ndani ya mawingu yake mazito; Na hilo wingu halipasuki chini yake. Husitiri uso wa kiti chake cha enzi, Na kulitandaza wingu lake juu yake. AYU. 26:7-9 SUV.
Ayubu wakati anapata maneno mbalimbali kwa marafiki zake, yeye alikuwa anaona Mungu ni mkuu sana kuliko vyote. Akaona kama Mungu anaweza kuhifadhi maji ya mvua katika mawingu, hatashindwa kufanya mambo mengine yanayoonekana kibinadamu hayawezekani.
Weka bidii katika kumjua Mungu kupitia Neno lake, utaona uweza wake na nguvu zake katika maisha yako ya wokovu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.