Wakati Herode anapanga mpango wa kumuua Yesu Kristo, habari hizo zilimfikia Yesu Kristo. Yesu aliwapa majibu Mafarisayo waliomletea taarifa hizo, majibu ambayo yalikuwa yanaonyesha dharau kubwa ya kumpuuza.
Majibu ambayo ukimjibu mkristo wa leo ambaye hajakomaa vizuri kiroho, anaweza kukuona bado hujaokoka vizuri kutokana na maneno uliyomwambia. Ambapo wewe unakuwa unajua hukutamka kwa bahati mbaya hayo maneno.
Yesu Kristo alijua kazi iliyomleta Duniani, hakuwa na wasiwasi na aliyokuwa anakutana nayo, hata shetani alipojaribu kumshawishi mambo yasiyofaa. Hakusita kumkemea waziwazi, maana alijua amekuja kufanya kazi gani, na kwa wakati gani.
Ujasiri tunaupata wapi? Hasa sisi tuliokubali kuitwa na tukaitika, ujasiri tunaupata pale tu tunapotambua kuwa aliyetuita na kutuchagua tumtumikie yeye. Yupo Pamoja nasi, vita vinavyopangwa juu yetu, vita hivyo ni vya kwake aliyetuchagua.
Ukiwa kama mtumishi wa Mungu, hupaswi kutetereka na vitisho vya shetani anapotumia watu wake kukutisha ili uache kuharibu kazi zake. Hili tunajifunza kwa Yesu Kristo mwenyewe, pale Herode alipoanza kutengeneza njama za kumshika, alijua hilo linapaswa kutendeka ila muda ulikuwa bado.
Rejea: Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. LK. 13:32 SUV.
Mtu anayetembea kwenye kusudi la Mungu, anajua majira na nyakati, ndivyo ilivyokuwa kwa Yesu Kristo. Tena akaendelea kuwaambia hao Mafarisayo, nabii hawezi kuangamizwa nje ya Yerusalemu.
Rejea: Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu. LK. 13:33 SUV.
Yesu Kristo alijua mahali pa kwenda kukinywea kikombe chake ni wapi, Yesu alijua siku ambayo ataanza kupata hayo mateso kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu.
Yesu hakutaka kusikiliza vitisho vya Herode, tena alimwita mbweha, hii ni kuonyesha dharau, kwa maana nyingine asimtetereshe kwenye kusudi lake. Yesu akaendelea kutoa pepo wachafu na kuponya wagonjwa, maana alijua amebakisha siku ngapi.
Yesu Kristo asingejua kusudi lake, angeyumbishwa na maneno ya Mafarisayo waliokuja kumwambia mpango wa Herode aliokuwa anaupanga juu yake. Hili hata kwetu linaweza kututokea katika maisha yetu ya wokovu na huduma.
Simama imara katika kulitimiza kusudi la Mungu katika maisha yako, kusudi ambalo Yesu Kristo alikuitia ulifanye. Vikwazo na vitisho mbalimbali, usikubali vikuondoe kwenye mpango wa Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com