Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, ashukuriwe Mungu kwa Rehema na fadhili zake kwa kutupa kibali kingine tena cha kushirikishana yale yanayotujenga mioyo yetu.

Wapo ndugu zetu wamegeuka kero katika maisha yetu, kiasi kwamba umemwombea kwa Mungu mpaka umeona sasa sio mtu wa kawaida. Na muda mwingine unaona kabisa hiyo sio akili yake peke yake, ipo nguvu inayomwendesha.

Inafika wakati watu hawa Mungu anaamua kushusha adhabu juu ya maisha yao, pigo lile linaambatana na mambo mengi sana. Moja ya mambo hayo ni kuondolewa ule uthamani wako mbele za watu.

Vipo vifo vya watumishi wa Mungu vinagusa maisha ya watu wengine kiasi kwamba unaona mtu yule alikuwa na mchango mkubwa sana mbele ya jamii. Wapo wengine vifo vyao vinakuwa kama nafuu ya wengine maana waliichosha jamii kwa matendo yao mabaya.

Unaweza kusema vifo vya matajiri vina nguvu kubwa ila sio kwa mtu aliyefikia hatua ya kutengwa hadi na Mungu. Sio kutengwa tu anapigwa na pigo la kumwangamiza kabisa maisha yake.

Unakuta badala ya watu kuomboleza kwa kuondokewa na mpendwa wao, wanakuwa na furaha ndani ya mioyo yao. Maana uliwasababishia maumivu makali ukiwa hai, madaraka uliyokuwa nayo hukuyatumia vizuri.

Hili tunaliona kwa Yehoramu, aliyetenda mabaya mbele za Mungu, akapelekea Mungu kushusha pigo la ugonjwa mbaya juu yake. Hilo halikutosha, alipelekea kuzikwa makaburi nje na ya wafalme wenzake, tena kazikwa kwa kawaida sana kulingana na nafasi yake uongozi wake.

Rejea; Na baada ya hayo yote BWANA akampiga matumbo kwa ugonjwa usioponyeka. Ikawa baada ya siku, ikiisha miaka miwili, matumbo yake yakatokea kwa sababu ya ugonjwa wake, akafa akiugua vibaya. Wala watu wake hawakumfukizia mafukizo kama ya baba zake. Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu miaka minane; akafariki bila kutamaniwa; wakamzika mjini mwa Daudi, ila si katika makaburi ya wafalme. 2 NYA. 21:18‭-‬20 SUV.

Tunajifunza kitu kikubwa sana hapa, ukipewa nafasi itumie vizuri kujenga na sio kubomoa. Unaona Yehoramu anakufa lakini watu walikuwa hawana hamu naye kabisa, inaweza kuwa kibinadamu walisema bora amekufa japo kuwa haijaandikwa, ila mazingira yanaonyesha.

Jifunze hili litakusaidia sana, usitumie nafasi yako vibaya, itumie vizuri ili kukuzalia matunda mema.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com