Kumtenda Mungu dhambi ina madhara mengi sana, yapo tusiyoweza kuyafahamu kwa haraka ila ukisoma Neno la Mungu utajua mengi sana.

Vizuri kujua madhara ya jambo, hata kama tutafanya jambo lolote linalomkosea Mungu wetu, tuwe tunafahamu madhara ya jambo hilo.

Tunaweza tusifanye mambo mabaya yanayomkosea Mungu wetu ila tunapofahamu madhara ya kumtenda Mungu dhambi. Hata wale wenzetu wakimkosea Mungu na wakaanza kutokewa na mambo ambayo sio mazuri kwao, tujue hayo ni matunda ya yale waliyoyatenda.

Dhambi utakayoifanya inaweza kukufanya ukawa lawama kwa watu, kila mtu akawa anakulaumu tu wewe. Hata kama utajitahidi kutenda sana mema, utashangaa watu wanakutupia lawama tu.

Unaweza ukashindwa kuelewa ni kitu gani ila unapaswa kufahamu hayo ni matokeo ya dhambi zako unazomtenda Mungu wako. Usishangae unaposimama mbele za watu, badala ya kukushangilia wakawa wanakuzomea kweli kweli.

Maovu yako Mbele za Mungu yanaweza kukufanya ukawa unafanyiwa dhihaka mbele za watu. Unaweza kutafuta umewakosea nini watu wale, na unaweza kutafuta umeikosea nini nchi yako.

Kumbe uliyemkosea ni Mungu wako, kwa kwenda kinyume na maagizo yake, yaani kuabudu miungu mingine, kuabudu sanamu, kufanya uasherati/uzinzi, muuaji na mengine mengi machafu. Utajiweka kwenye kundi baya sana ambalo litakufanya uonekane mtu usiye na maana mbele ya jamii yako.

Unaweza kukataa na kusema haiwezekani ukawa mtu wa lawama kwa watu, na unaweza kukataa na kusema haiwezekani ukawa mtu wa kudhihakiwa na nchi yako. Uzuri wake maandiko matakatifu yanatuthibitishia hili ninalokueleza hapa.

Rejea: Umekuwa na hatia katika damu yako uliyomwaga, nawe umekuwa na unajisi kwa vinyago vyako ulivyovifanya; nawe umezileta karibu siku zako, nawe umefika karibu na miaka yako; basi, kwa sababu ya hayo, nimekufanya kuwa lawama kwa mataifa, na kuwa dhihaka katika nchi zote. EZE. 22:4 SUV.

Umeona hilo andiko, hilo andiko limebeba kitu kikubwa sana, unaweza usilielewe kwa haraka ila fahamu kwamba kumtenda Mungu dhambi ni kujipaka matope mabaya. Ambapo kila atakayekutazama, atakutupia lawama, na atakudhihaki.

Epuka kujiingiza kwenye kundi la lawama, na epuka kujiingiza kwenye kundi la dhihaka. Hutokuwa na furaha ya maisha yako, kama kila kitu utakachokifanya badala ya kuwa baraka kinageuka kuwa lawama na dhihaka mbele za watu.

Wote tunajua sio kila kitu utafanya kitawafurahisha watu, yapo mazuri utafanya na bado watakutupia lawama, na wapo watakudhihaki. Pamoja na hayo yote, omba Mungu asikufanye uwe mtu wa Lawama, yaani uwe mtu wa kulaumiwa tu, hata kama utafanya mazuri gani, bado utalaumiwa.

Watu wenyewe wakudhihaki kwa wivu wao wa kibinadamu na sio Mungu aruhusu dhihaka kwako, kwa sababu ya dhambi zako. Utaona Dunia chungu, Utaona uongozi wako mgumu, utaona utumishi wako mgumu, chochote kile unachokifanya mbele ya jamii yako kitageuka kitanzi kwako, badala ya kuwa baraka kwako.

Jiepusha kumtenda Mungu wako dhambi, umeona ni jinsi gani dhambi inaweza kukupelekea pabaya. Sio kwamba utasubiri mpaka siku ya mwisho ndio uje upate madhara yake, madhara yake utaanza kuyaona hapa hapa Duniani.

Mungu atusaidie sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081