Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, wakati mwingine tena tumepata nafasi ya kushirikishana yale tuliyojifunza, ambatana pamoja nami.

Vizuri ukiamua kumfuata Mungu umfuate kweli, kwa kuishi maisha yampendezayo yeye, na kumtumikia katika roho na kweli. Hii inakupa nafasi nzuri mbele za Mungu ya kuweza kutumiwa na yeye, kuliko kuonekana upo na Mungu kumbe sivyo ilivyo.

Mungu wakati mwingine akitaka kutubariki, anashindwa kutokana na vizuizi vya maovu yetu tunayoyatenda katika maisha yetu.

Lakini tunajifunza kwa mtu aliyemcha Mungu katika roho na kweli, Mungu akambariki na akampa kibali cha kuletewa zawadi kutoka sehemu mbalimbali. Akawa na mali nyingi ambazo zilitokana na makundi mbalimbali ya watu.

REJEA; Naye BWANA alikuwa pamoja na Yehoshafati, kwa kuwa alikwenda katika njia za kwanza za Daudi babaye, asiyatafute mabaali; Kwa hiyo BWANA akauthibitisha ufalme mkononi mwake; Yehoshafati akaletewa zawadi na Yuda wote; basi akawa na mali na heshima tele. Na baadhi ya Wafilisti walimletea Yehoshafati zawadi, na fedha ya kodi; Waarabu nao wakamletea makundi, kondoo waume saba elfu na mia saba, na mabeberu saba elfu na mia saba. 2 NYA. 17:3‭, ‬5‭-‬5‭, ‬11 SUV.

Huna haja ya kujuta kumtumikia Mungu katika huduma yako, ikiwa mahusiano yako na Mungu yapo vizuri. Kabisa hatuna haja ya kuona hasara ya kuokoka, ikiwa Yesu Kristo yu ndani yetu. Tufahamu ya kwamba akili zetu na uwezo wetu wa kufanya kazi unaletwa na juhudi za kuutafuta uso wa Mungu.

Hakuna mtu aliyelazimishwa kumletea Yehoshafati zawadi, hakuna mtu aliyezamishwa kumeletea fedha, hakuna mtu aliyelazimishwa kumheshimu. Walifanya hivyo kwa sababu Mungu alimpa kibali machoni pa watu, kwa sababu ya kumtumikia Mungu kwa uaminifu.

Mungu anajua mahitaji yako, ukimtumikia kwa uaminifu, atakuinua kutoka chini mpaka juu, kutoka kudharauliwa mpaka kuheshimiwa. Ni wewe kuamua uishije maisha ya kumpendeza yeye, Mungu wetu hataki uabudu miungu mingine, Mungu wetu hataki ujichanganye na dhambi.

Utashangaa Mungu akiinua huduma yako ya uimbaji kifedha ili upate kuwafikia wengi zaidi, utashangaa Mungu akikuinulia watu wa kukubeba katika huduma yako ya kuihubiri injili. Hutolazimisha mtu, bali Mungu mwenyewe atawaongoza watu wake kuleta kile anachowasukuma wakifanye kwako.

Haikuwa rahisi wafilisti kumletea Yehoshafati zawadi, haikuwa rahisi waarabu kumletea Yehoshafati makundi ya kondoo. Nasema hivi, sio jambo la kawaida mpaka wasiomjua Kristo kujitolea kutoa mali zao kwa ajili ya kazi Bwana.

Unaweza usielewe sana ila shika sana maandiko yanavyosema, maandiko yapo sahihi, naamini kama upo makini na Mungu. Utakuwa umeona vitu fulani katika maisha yako, Mungu akikuinua kwa viwango ambavyo hata wewe mwenyewe ukikaa na kutafakari unakiri kweli Mungu ni mkuu.

Hakuna hasara ya kumtumikia Mungu kama utakuwa unamwelewa vizuri unayemtumikia, maana wanaweza kuja watu ambao hukutegemea wakiwa na mali zao. Wakisema tumeleta kwako mtumishi wa Mungu, usiposikiliza sauti ya Roho Mtakatifu, unaweza kuwafukuza kwako.

Mungu wetu ni wa vyote, mali na fedha vyote ni vyake, ukimtumikia katika Roho na kweli, hatokuacha kamwe, iwe kwenye biashara yako, kazi yako, masomo yako, familia yako, Mungu atakubariki kwa uaminifu wako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com