Kwanini uwe na mashaka mtu wa Mungu, mashaka ya nini kwa washirika wako, kuwazuia kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu. Wewe unamhubiri Yesu Kristo si ndio? Yote unayohubiri yapo ndani ya Biblia si ndio?

Sasa kwanini unapoona mtu anakimbilia mafundisho ya Neno la Mungu, wewe unamzuia? Sio kana kwamba anakimbilia mahali ambapo anapotoshwa, sio kana kwamba mahali anaenda wanahubiri injili ya vitambaa, au ya mafuta ya upako.

Wanahubiri injili isiyoghushiwa, injili ambayo hata wewe ukiisikia lazima ubadili mwelekeo wa maisha yako, kama hukuwa vizuri. Na kama ulikuwa vizuri unaondoka na maarifa mazuri zaidi ya kukujenga.

        Ndugu ukiona unazuiwa sana kwenda kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu, usifikiri labda mchungaji wako, nabii wako, mtume wako, mwalimu wako. Ameona huko sio sehemu sahihi, hapana, anajua ukienda huko utamgundua kuwa sio mtumishi wa Mungu sahihi.

Mtu yeyote aliye kinyume na Neno la Mungu, hawezi kuruhusu washirika wake au watoto wake wakasikie ile injili sahihi ya Neno la Mungu. Atawajaza maneno potovu watoto wake au washirika wake kuhakikisha wanaendelea kubaki udanganyifu.

Mtumishi sahihi hawezi kuwa na mashaka labda ataibiwa washirika na mtu anayehubiri injili sahihi ya Neno la Mungu, anajua washirika wake wameenda kujifunza Neno la Mungu kwa mtumishi sahihi.

Kama mtumishi wako anakuzuia kabisa usitafute mafundisho mengine zaidi yake, usifikiri anakupenda sana na hapendi kukuona ukipotea kwenye njia sahihi. Wengine wanakuzuia ili usije ukatoka usingizini, anajua kabisa ukizinduka usingizini utamkimbia.

Japo wapo watumishi wa kweli wa Mungu, wanaweza kukuzuia usiende mahali ambapo sio sahihi, sasa hapa lazima uwe na Neno la Mungu la kutosha, hapa lazima uwe umejazwa Roho Mtakatifu. Itakusaidia kuepuka mtengo wa shetani, aliouweka ili akunase.

Shetani hapendi kukuona ukipata maarifa sahihi ya Neno la Mungu, atahakikisha anakunyima hiyo nafasi ili aendelee kukutumia. Sio kukutumia tu hapa Duniani, lengo lake usipate nafasi ya kwenda kuishi maisha ya umilele mbinguni.

Mtu yeyote aliye kinyume na Neno la Mungu, lazima apinge watumishi wa Mungu wa ukweli, lazima awe mpinzani mkubwa. Sio kwamba anafanya hivyo kama mtu asiyejitambua anafanya nini, anajua kabisa kazi aliyonayo.

Hili tunajifunza kupitia Neno la Mungu, mtu mmoja alikuwa mchawi sana, mchawi huyu alikuwa karibu sana na Liwali, Liwali huyu alivyoona watumishi wa Mungu. Ambao walikuwa ni Barnaba na Paulo(Sauli), Liwali huyu aliwaita kwake ili apate kulisikia Neno la Mungu.

Lakini mtu huyu mchawi alivyoona Liwali anataka kusikia Neno la Mungu kutoka kwa watumishi wa Mungu, yule mtu mchawi alitafuta kila njia kumzuia yule Liwali asiamini ile imani iliyokuwa inahubiriwa na Barnaba na Paulo.

Rejea: Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho. MDO 13:6‭-‬9 SUV.

Hiyo ndio mbinu ya manabii wa uongo, kazi yao kubwa ni kukunyima nafasi ya kusikiliza Neno la Mungu, watahakikisha wanaufunga ufahamu wako usiweze kusikia mafundisho ya Neno la Mungu.

Ukiwa kama mtumishi wa Mungu uliyesimama vizuri na Mungu, usipokuwa na nguvu ya Roho Mtakatifu unaweza kushindwa nguvu na hawa manabii wa uongo, hawa walimu wa uongo, na hawa wachungaji wa uongo, ambao wanatumia nguvu za giza kama huyu mtu mchawi tuliyemsoma habari zake hapa.

Rejea: Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. MDO 13:9‭-‬11 SUV.

Hiyo ndiyo dawa ya kupambana na wana wa ibilisi ambao ni manabii wa uongo, walimu wa uongo, wachungaji wa uongo, na mitume wa uongo. Kilichomsaidia Paulo, ni kujaa nguvu za Roho Mtakatifu, ambaye hata wewe unaweza kujazwa naye Roho Mtakatifu.

Usifanye huduma kienyeji bila kuwa na Roho Mtakatifu, uwe mwimbaji, uwe mwalimu mzuri wa Neno la Mungu, hakikisha unajazwa na Roho Mtakatifu. Maana akina Elima wapo wengi sana kwa Dunia ya sasa, pale utapokutana nao hakikisha umejiweka vizuri na Mungu.

Karibu sana katika group la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081 wenye Neno CHAPEO YA WOKOVU utaunganishwa.

Soma Neno ukue kiroho.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com