Haleluya,

Zipo tabia ambazo huwa tunaziendeleza na kujikuta tunaharibu mahusiano yetu ya ndoa, kwa sababu tu ya uzembe wetu wenyewe.

Unakutana na dada/kaka ameanza maisha ya ndoa lakini bado anafanya mambo kama vile anaishi na wazazi wake. Anaona hawezi kumshirikisha mwenzake mambo mengine isipokuwa yale tu anayoona kwake inafaa.

Badala ya kushauriana na mwenzi wake wa ndoa, anaona ni heri akapate ushauri kwa wazazi/ndugu zake. Mwenzake anakuwa tu mtu wa mwisho kabisa katika maamzi ya ndoa yake.

Sisemi ni vibaya kuwashirikisha mambo wazazi wako, ninachozungumza hapa yapo mambo mnapaswa kuyajenga wenyewe bila ndugu/wazazi wako kujua. Akili yako yote inapaswa kujua rafiki namba moja wa kumshirikisha jambo lako kabla hata ya wazazi wako, ni mke/mume wako.

Ni ajabu mzazi wako kuwa na mipango yenu ya maisha kwa mwaka mzima, alafu mke/mume wako uliyenaye ndani hajui chochote.

Wengine wanaanzisha miradi mikubwa mke/mume wake wala hajui chochote, wengine wanakuwa na nyumba za kupangisha wageni ila mume/mke wake hajui chochote. Ila wazazi wake wanajua kila kitu, isipokuwa mke/mume wake.

Huo sio mwili mmoja, walio mwili mmoja wanapaswa kushirikiana mambo yao pamoja. Yapo mambo huwezi kumshirikisha mzazi wako, ila mke/mume wako utaweza kumshirikisha bila hofu yeyote.

Lakini wapo watu bado wanakumbuka wazazi wao kuliko mke/mume wake aliyenaye karibu. Unapochanganya mambo haya, kwanza unafanya mke/mume wako adharauliwe na wazazi/ndugu zako.

Unakuta dada/mama ameolewa lakini anajibia vitu vya ndani anapeleka kwao bila taarifa yeyote ya mume wake, akijua anamkomoa mume wake kumbe anajikomoa mwenyewe. Hapo akija kujua mume wake lazima pawepo mtafaruku mgumu sana ndani ya nyumba.

Hebu tuone maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hili la kuwasahau wazazi wako pale unapoingia ndani ya ndoa.

Rejea: Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako. ZAB. 45:10 SUV.

Umeona hapo, tunaaswa hivyo tuwasahau wale wa nyumbani mwetu. Hii inamaanisha kwamba unapaswa kujua sasa unaye mwenzako ambaye mnapaswa kwenda pamoja. Sio baadhi ya mambo unamshirikisha na mengine unaacha, unakimbilia kuwashirikisha ndugu zako au wazazi wako.

Uelewa hapa, sio uwasahau na kuacha kushirikiana nao vitu kama mwanafamilia, haimanishi hivyo. Utashirikiana mkiwa na mwenzako au mkiwa mmekubaliana wote.

Mama/dada usifanye makosa haya, heshima ya wazazi wako itabaki pale pale. Ila kwa mume wako itabaki vilevile pia, na anapaswa kujua mengi zaidi unayoyahitaji kutoka kwake na akakusaidia vizuri tu na mengine mkasaidiana.

Mungu akubariki mno.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu.
Tovuti: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.