Wengi huwa tunakimbilia kuwa watumishi, kuwa wachungaji, kuwa wainjilisti, kuwa mitume, kuwa manabii na kuwa walimu. Bila kuwa na wito wa hizi huduma ndani yetu, tukifikiri kuitwa mtumishi wa Mungu ni dili fulani hivi.

Muda mwingine sio kama mtu anakuwa na hiyo huduma ndani yake ila kutokana na ameona wengine wanavyopata heshima. Anaona na yeye bora awe hivyo ili aweze kupata hiyo heshima wanayopata wengine.

Ukiwa kama kiongozi, hasa kiongozi wa kiroho, unaweza kufika mahali Mungu akakutwisha mizigo ya wale unaowaongoza. Ukiwa kama kiongozi unakuwa umebeba dhamana kubwa ya wale unaowaongoza, mambo mengi mazito yanaanzia kwako kabla ya kuwafikia wale unaowaongoza.

Wanapoenda kinyume na maagizo ya Mungu, hata kama wewe hujatenda hayo, mzigo mkubwa unakuwa kwako. Unaweza kuingia gharama kubwa kwa ajili ya wale unaowaongoza, kwa sababu ya maovu yao.

Unaweza kuingia kwenye maombi magumu kuepusha hasira ya Mungu isiweze kuwaangukia wale unaowaongoza. Huwezi kusema watajua wenyewe, Mungu anakutazama wewe kiongozi wao.

Hebu fikiri ulijiingiza kwenye uongozi kwa ajili ya maslahi yako binafsi, hukuwa na wito wowote ndani yako. Ule wito wa kuwatumikia wengine hukuwa ndani yako, uliingia kwenye huduma kwa kuvutwa na vitu vya kimwili.

Unakutana na suala la kubeba mizigo ya wale unaowaongoza, uongozi unaweza kugeuka mchungu. Unaweza kufika mahali ukasema uchungaji basi tena, ualimu basi tena, uinjilisti basi tena, utume basi tena, na unabii basi tena.

Changanya huna muda wa kutulia usome Neno la Mungu, maana yake huna chakula chochote cha kiroho ndani yako. Hapa unaweza kuikimbia huduma, hapa unaweza kuukimbia uongozi uliokuwa nao.

Ukiwa kama mchungaji, au mwinjilisti, au mwalimu, au mtume, au nabii, mizigo mingi ya unaowaongoza unakuwa unaibeba wewe. Hapa lazima uwe na stamina za kutosha, sio stamina za ugali, ni stamina za kiroho, zilizoshiba Neno la Mungu na maombi.

Hili tunajifunza kwa nabii Ezekiel, alibebeshwa uovu wa nyumba ya Israel na nyumba ya Yuda. Huu mzigo hukuwa mzigo rahisi kuubeba, ulikuwa sio mzigo wa kawaida, lakini alipaswa kufanya hivyo.

Rejea: Tena lala chini kwa ubavu wako wa kushoto, ukaweke huo uovu wa nyumba ya Israeli juu yake; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala juu yake, kwa kadiri hiyo utauchukua uovu wao. Maana nimekuagizia miaka ya uovu wao iwe kwako hesabu ya siku, yaani, siku mia tatu na tisini; ndivyo utakavyouchukua uovu wa nyumba ya Israeli. Tena utakapozitimiza hizo, utalala kwa ubavu wako wa kuume, nawe utauchukua uovu wa nyumba ya Yuda; siku arobaini, siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagizia. EZE. 4:4‭-‬6 SUV.

Mwanzo nilitangulia kusema hivi, nafasi ya uongozi, hasa uongozi wa kiroho sio dili, usikimbilie uchungaji wa kanisa kwa maslahi yako binafsi. Kama ndani yako huna huduma ya kichungaji, utaukimbia huo uchungaji mchana kweupe.

Kupitia hiyo mistari michache niliyokupitisha hapo juu, unaweza kuona huduma sio jambo la kuchukuliwa kawaida. Watumishi wa Mungu wamebeba dhamana nzito sana juu ya wale wanaowaongoza, wanapaswa kuisema kweli ya Mungu bila kupindisha maneno, na wanapaswa kutubu uovu badala ya wengine.

Katika huduma zao za utumishi, yapo mambo magumu wanakutana nayo ni Mungu tu anakuwa anawatetea. Muhimu sana kuombea watumishi wa Mungu, wamebeba dhamana nzito sana ya maisha ya watu wengine.

Uongozi sio fasheni, ukijua hili hutokimbilia ovyo kuwa kiongozi bila kupiga hesabu vizuri. Haijalishi uongozi wa kawaida, nikiwa na maana uongozi usio wa kiroho, unaweza ukawa kazini kwako au shuleni/chuoni huwa kuna uongozi wa wanafunzi. Lakini fahamu uongozi sio jambo jepesi.

Ukiwa kama mtumishi wa Mungu uliyekabidhiwa dhamana ya kuwaongoza wengine, Mungu akutie nguvu, nakuombea kwa Mungu akupe nguvu na ujasiri wa kuweza kusimama katika nafasi yako pasipo kuyumbishwa na chochote.

Mungu akubariki sana

Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.