Kila mmoja anaweza kuweka alama kwa watu, alama ambayo haitafutika kwenye mioyo ya watu. Yale mambo yanayoonekana madogo madogo, yale mambo yanayopuuzwa na watu, mtu anaweza kuyafanya na yakamletea kumbukumbu njema kwenye mioyo ya watu.

Ni ngumu kumfurahisha kila mtu, maana tunaweza kutenda mema kwa wengine, wengine wakatuona kwa namna mbaya. Namna ambayo ukiisikia inakuvunja moyo wa kuendelea kuwatendea wengine mema, lakini usipojali sana maneno ya watu. Unaweza kufanya vizuri kabisa.

Kujitoa kwa ajili ya wengine, kuwatendea wengine mema, ni hazina kubwa sana tunajiwekea mbinguni na hapa Duniani. Unaweza kumtendea mtu jema, ukawa umesahau kabisa kwenye fahamu zako ila kwa mtendewa uliyemtendea jema akawa anakumbuka.

Utasema mbona mimi nimewatendea sana watu mazuri ila wakati wa shida yangu hakuna aliyejitokeza hata mmoja, upo sawa kabisa, maana hao ni wanadamu ila kumbuka vizuri wakati ile shida yako Yesu Kristo alikuinulia watu wengine kabisa ambao hukuwategemea.

Mema yako unayowatendea watu, hayo yanakuwa kumbukumbu yako kwa Mungu wako, hata kama mwanadamu mwenzako atakusahau uwe na uhakika Yesu Kristo hawezi kukusahau kamwe.

Kwahiyo usiache kutenda mema, kwa sababu kuna watu uliwatendea mema wao wakakulipa mabaya. Wema wako ni akiba, akiba hiyo itatumika wakati ambao umeishiwa kabisa na unauhitaji mkubwa.

Kujitoa kwako kuwatendea wengine mema, inaweza isiwe pesa ila muda wako unaoutoa kwa ajili ya wengine. Mungu anakuona, ipo siku kupitia hayo unayowatendea wengine yatakuokoa kwenye shida yako. Nakueleza kitu nilichokiona kwenye maisha yangu.

Kutoa pesa zako kwa ajili ya kusimamisha majengo ya kanisa, hiyo sio hasira, ni hazina yako umejiwekea, utavuna kwa wakati ambao hukudhania kabisa. Wakati ambao hukujua kama ulilolitenda linaweza kutumika kusukuma muujiza wako utendeke/utokee haraka.

Kukarimu kwako watumishi wa Mungu, kuhakikisha wanakuwa salama wakati wa huduma, elewa hufanyi kazi ya bure, ipo siku utavuna matunda ya ukarimu wako. Hata kama umeanza siku nyingi kuwakarimu watumishi wa Mungu, na huoni matunda yeyote, na wakati mwingine umetupiwa maneno mabaya na washirika wenzako. Amini ipo siku utavuna matunda ya ukarimu wako, unachokifanya hupotezi kitu, bali unapanda kitu kwa Bwana.

Unaweza kuwa umejitoa sana kwa mambo ya kanisa, hadi umefika mahali unajisikia kuchoka, unasikia kabisa kukata tamaa. Huna kabisa ule msukumo wa kuendelea kujitoa, nakutia moyo usichoke, kazi yako sio bure, utavuna usipozimia moyo.

Sikuelezi habari ambazo hazipo, haya ninayokueleza hapa yapo kibiblia, wapo watu waliotoa maisha yao kwa ajili ya watu wengine. Tumeona Mungu aliwatetea na kuwabariki, mfano mzuri ni Dorkasi, Mungu alimrejesha uhai wake tena.

Na kilichomfanya Mungu amrejeshee uhai Dorkasi, ni sadaka zake, wale wamama wajane waliokuwa wanashonewa nguo. Walisema haiwezakani mtu huyu mwema kutuacha, wakati Dorkasi hawezi kusema kitu, wakati amenyamazishwa na mauti, wapo watu walisimama badala yake kusema, na mwisho tunaona alifufuliwa.

Rejea: Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. MDO 9:36‭-‬40 SUV.

Matendo yako mema unayowatendea wengine usijione unapoteza muda wako, ipo kumbukumbu yake, hata kama huambiwa unafanya vizuri. Endelea kumtumikia Mungu kwa sadaka yako ya vitu, ya muda wako, ya fedha zako, ya mali zako, utaona ikikuzalia matunda mema.

Hili hatujifunzi kwa Dorkasi tu, hili tunajifunza tena kwa akida mmoja, huyu akida alikuwa mtu mwema aliyelifaa taifa lake, alijitoa akajenga sinagogi. Siku mtumwa wake anaumwa sana, tena alikuwa anaumwa mtumwa anayependwa sana na jemedari/akida huyu. Aliposikia habari za Yesu Kristo, alituma watu kumwita aje amponye mtumwa wake.

Cha kushangaza hao watu walipofika kwa Yesu Kristo, walianza kumwanga sifa za akida yule, vile anastahili kutendewa lile analolihitaji kutoka kwa Yesu Kristo. Na Yesu Kristo aliwasikiliza watu wale na kufuatana nao hadi kwa akida.

Rejea: Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana. Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake. Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi. LK. 7:2‭-‬5 SUV.

Je, wewe msomaji wangu, watu wataweza kusimama kuusema wema wako? Huo wema wenyewe unao uliowatendea wengine? Kama ulikuwa unaona huna haja ya kujitoa kwa ajili ya wengine, kuanzia leo anza kubadili mtazamo wako hasi.

Wema unalipa, na kujitoa kunalipa, tumeona kwa Tabitha/Dorkasi, tumeona kwa akida/jemadari, jinsi watu walivyonena wema wao waziwazi. Na vile wema ulivyowasaidia, wakati ambao watu wengine walisimama kuwasemea juu ya shida yao.

Yesu Kristo ndio kila kwetu sawa ila tunapaswa kuweka alama njema kwa watu wake, hili ni muhimu sana, fanya sehemu yako, usitafute mambo makubwa sana. Hayo hayo madogo unayoyaona kwako, yana mchango mkubwa sana, cha msingi yafanyike kwa moyo wa upendo. Na kwa utukufu wa Mungu.

Dorkasi alililiwa na wajane mbele ya Petro, Petro alionyeshwa kazi aliyokuwa anawatendea wale wamama wajane. Najua unaelewa vilio vya akina mama waliojaa uchungu mwingi ndani yao, tena uchungu wa kuondokewa na mpendwa wao, hakika kilikuwa kilio kikuu sana.

Hebu fikiri kwa muda, tenga muda wako ujiulize hili, yupo mtu anaweza kusimama na wewe kuhakikisha umetoka kwenye shida yako. Mtu huyo akisukumwa na wema wako uliowahi kuutenda huko nyuma, kama hakuna una nafasi ya kurekebisha hilo. Na kama lipo, mshukuru Mungu na endelea kutenda mema.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
WhatsApp: +255759808081
www.chapeotz.com