Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, habari za wakati huu, bila shaka unaendelea kumtumainia Mungu ndio maana umetenga muda wako kusoma ujumbe huu. Ili ujue nini kinachozungumziwa siku ya leo, cha kuweza kukusaidia katika safari yako ya wokovu.

Tumekuwa na ukawaida SANA wa kuona maombi ni kitu cha kawaida, ambapo tunaamua tuombe au tusiombe, hasahasa tunakuwa na ukawaida pale tunapokuwa kwenye hali nzuri za maisha. Pale unapokuwa na ndoa yenye furaha, watoto wenye afya njema, ada ya shule/chuo inapatikana vizuri, hali ya kazi na biashara zinaenda vizuri.

Nyakati kama hizi kila mmoja wetu huwa na amani na furaha ya moyo wake, wengi katika kipindi hichi huwa wanaona haina haja ya kujitesatesa kuacha kula. Sio ajabu mtu huyu aliye kwenye hali nzuri, akakuambia kufungafunga ni kwa ajili ya wenye shida zao.

Mwingine anaweza kukuambia wanaofunga ni wale wenye shida ya chakula, ni wale wasio na pesa za kula milo mitatu kwa siku, wanafanya kazi ya kufunga ili kuepuka gharama.

Tunakuwa tunakosea sana kufikiri kufunga ni kujiwekea bajet vizuri tusije tukazidiwa na matumizi, tunasahau kufunga ni kujinyenyekeza kwa Mungu atusaidie hitaji ambalo tunaona ni mzigo kwetu, na bila yeye kuhusika hatutaweza.

Mkristo asiyependa kufunga, yeye kazi yake ni kula tu, wokovu wake una shida sehemu. Ukimfuatilia mtu wa namna hii utaona vitu vya ajabu sana visivyompendeza Mungu, japo kufunga sio tiketi sana ya kuonyesha mtu ameokoka maana hata shetani ana watu wake anaowagiza wafunge. Ila kufunga kwetu tuliokoka inatupa nafasi kubwa sana Mungu kusikia maombi yetu kwa namna ya pekee sana.

Unaposikia agizo la kufunga na ukaelezwa sababu ya kufanya hivyo, usipuuze hata kidogo, Mungu hutazama ile nia ya ndani. Nia ile inaendana na matendo yetu, hatuwezi kumpenda Mungu kwa kutamka tu mdomoni pasipo kuyaishi maisha matakatifu.

Mara ngapi umechukua hatua ya maombi ya kufunga pale ulipoona pasipo msaada wa Mungu hutaweza peke yako. Ulifanya hivyo au uliona ukiacha kula utaharibu umbo lako namba nane, au uliona utapauka sana, au uliona utapoteza mvuto kwa watu.

Lakini tuona taifa la Yuda kiongozi wao akitoa agizo la watu wote kufunga kwa ajili ya kumweleza Mungu vita iliyo mbele yao. Hawakuishia kusema Mungu atatusaidia tu, bali walichukua hatua ya kumwendea Mungu kwa pamoja kwa kuacha chakula, kwa kila mmoja wao.

REJEA; Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute BWANA; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta BWANA. 2 NYA. 20:3‭-‬4 SUV.

Kiongozi wako alipotangaza maombi ya kufunga ulifunga? Au wewe ni mtu wa dharura kila unaposikia tangazo la maombi. Maombi ni silaha mhimu sana kwa mkristo, sisemi maombi ambayo hujafunga Mungu hayasikii la hasha! yanajibiwa ila yapo mambo hayawezekani mpaka kwa kufunga na kuomba.

Jenga utaratibu huu wa kutii maombi ya kufunga utaona matunda mazuri sana katika huduma yako, katika familia yako, katika masomo yako, katika biashara zako, katika ujana wako. Unaweza kuteswa sana na tamaa za mwili huku umeokoka, lakini ukiamua kuingia kwenye maombi ya kujinyima chakula, utashangaa unaondolewa hiyo hali mbaya kabisa.

Mungu akusaidie uelewe hili ninalokueleza hapa, kama ulikuwa unachukulia maombi ni kitu cha kawaida, kuanzia sasa yaone ni kitu cha msingi sana kwako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako,
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com