Tunapompokea Yesu anatubadilisha mambo mengi sana, namna isiyofaa mbele zake inaondoka ndani mwa mtu hasa pale anapojazwa na Roho Mtakatifu. Unakuta mnakuwa kitu kimoja na watu ambao hamkuzaliwa tumbo moja na wala sio wa kabila moja.

Pamoja na hayo yapo mambo katika tamaduni zetu huwa hayaachwi moja kwa moja, ndio maana utaambiwa mambo fulani yameondolewa kwa sababu tumeokoka ila mengine utayakuta yapo kwa mtu au kabila lao.

Wapo pamoja na kuokoka, kutokana na kutokuwa na mafundisho ya kutosha utakuta wanaishi katika mambo ambayo hata mbele za Mungu hayampendezi kabisa. Ama wazazi wanaweza kuwa hawajaokoka ila kijana wao akawa ameokoka.

Unapokuwa umeokoka alafu wazazi wako hawajaokoka uwe na uhakika usipokuwa makini utafanya yale yaliyo machukizo mbele za Mungu, na baadaye yakakuletea shida kwenye ndoa yako.

Kwanini ni muhimu kujua mila na desturi kwa unayetaka kumuoa/kuolewa naye?

Kama wewe ni kijana wa kiume unapaswa kulifahamu hili kwa binti, lipo kabila linaamini mwnanaume anayempenda mke wake lazima atampiga. Wewe huamini katika hilo na unajua kumpiga mke wako ni dhambi, kama hutojua hili mapema na ukaongea na mwenzako kujua mtazamo wake juu ya hilo ukoje ujue utaingia kwenye ugomvi  na mke wako.

Ukiwa wewe ni binti unapaswa kujua upande wa mume wako mtarajiwa mila na desturi zao zipoje, yapo makabila yanaamini mwanamke mwenye heshima anapaswa kumpigia magoti mume wake anapokuwa anamwandalia chakula au anapomsalimia.

Alafu ukaingia ukiwa hujui hilo na kwenu hakuna hayo mambo ya kupiga magoti, ujue utaingia kwenye mgogoro ambao utaona unaonewa na hujazoea hayo mambo ya kupiga piga magoti.

Vizuri kufahamu mapema, unaweza kuonekana kwa wakwe zako huna heshima au adabu kwa kutopiga kwako magoti wakati unawasalimia au unawaandalia chakula. Ukaingia kwenye mgogoro ambao utaona unaonewa na kubadilika haraka ikawa ni ngumu kwako kama hutolipokea haraka moyoni mwako.

Vizuri kujua mila na desturi kwa mwenzako uliye na malengo naye ya kuingia kwenye maisha ya ndoa, zipo tabia za kawaida kwa wahusika ila kwako inaweza ikawa adhabu  kwa sababu hujazoea hayo maisha.

Kabila zingine kitoweo chao ni nyama ya Panya, au mbwa, na mwenzako anapenda sana hicho kitoweo na anatamani mke wake awe anampikia hicho chakula. Alafu wewe ukawa unashangaa hayo na kuona haifai na huwezi kupika, kitakachofuata hapo ni ugomvi.

Yapo makabila mengine ni makarimu, yanapenda kuwakarimu wageni wanapowatembelea nyumbani kwa kuwapikia chakula chao cha heshima. Alafu yapo makabila hayana hiyo tabia na wanaona kula kula kwa watu sio tabia njema, usipolijua hilo utagombana na mwezi wako na kumwona ana roho mbaya.

Yapo mambo mengi sana ambayo kabila na kabila hayaingiliani kabisa kwenye tabia na muundo wa maisha wanayoishi nayo, lazima ujue hilo mapema, hata kama mmekutana mjini ujue utaenda kwao. Ukienda kwao usije ukakerwa na kujisikia vibaya kutokana na desturi zao.

Jiandae mapema, fahamu desturi zao zikoje, jiulize upo tayari kuendana nazo au haupo tayari kabisa, ukiwa haupo tayari fanya maamuzi ya busara mapema. Ukiwa haupo tayari jiupushe naye kuliko kupeleka ugomvi usio na maana kwenye familia yako.

Usiseme umeokoka utawaombea hadi wabadilike na kuendana na desturi zenu, nikiulize ikiwa hayo maombi yatajibiwa miaka 10 mbele ukiwa kwenye ndoa yako! utakuwa tayari kusubiri huo muda? maana huwezi kumpangia Mungu muda wa kujibu maombi yako.

Ninaamini umepata jambo ulilojifunza kupitia makala hii, na ninaamini Roho Mtakatifu atakufundisha zaidi kadri unavyozidi kutafakari haya au wakati unasoma haya. Yale umejifunza usiyapuuze bali yafanyie kazi mapema kabla ya kuingia kwenye hatua kubwa zaidi.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
+255759808081