Mungu huwa anatutoa mbali sana, nasema mbali kwa sababu kuna mazingira mtu anakuwa nayo. Mazingira ambayo ukiyatazama unaona  kweli huyu mtu kuna mahali anapita.

Sio kupita tu, kuna mazingira mtu anakuwepo na ukimtazama kwa akili za kibinadamu huwezi amini kama ataweza kubadilika.

Wapo watu leo ukipata nafasi ya kuangalia picha zao za miaka 10 au mitano iliyopita, huwezi amini kama ni wenyewe.

Vile alikuwa amechoka, vile alikuwa mwembamba haswa,  sio mwembamba kwa sababu ya kupenda awe hivyo.

Mtu huyo huyo Mungu anamjalia anakuwa mnene, hata mwenekano wake unabadilika kabisa.

Baada ya kunenepa na kupendeza, anamsahau na Mungu. Anakuwa hana muda na mambo ya Mungu.

Anakuwa hana muda wa KUFUNGA NA KUOMBA, hana kabisa habari hiyo.

Watu kama hawa Mungu alishawatambua siku nyingi tangu agano la kale.

Rejea: Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke; Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda; Ndipo akamwacha Mungu aliyemfanya, Akamdharau Mwamba wa wokovu wake. KUM. 32:15 SUV.

Utakuwa sio mgeni na hili, kuhusu wale watu ambao walikuwa na miili midogo. Baada ya kunenepa na kumpendeza wakamsahau Mungu.

Kumdharau Mungu ni kuanza kupuuza mambo yake, kudharau neno lake, hushtuki tena na mambo yahusuyo Mungu.

Ndugu yangu, utakapofanikiwa kiafya, kiuchumi, kimasomo, usije ukamdharau Bwana Mungu wako.

Mungu awabariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com