Mch Samson;

Shalom mtu wa Mungu!

Wewe unajua kuanza kwangu Chapeo ya Wokovu hata hapa Mungu aliponifikisha, na mbele ninaendelea kwa msaada wa Mungu.

Bado najiona sitoshei katika kujifunza Neno la Mungu, lakini Mungu ananishangaza sana na siwezi kuendelea kunyamaza.

Mwaka jana July, nilipewa jukumu na Mchungaji wangu kuwa nafanya maandalio ya masomo kupitia kile kitabu cha Shule ya uanafunzi ambacho makanisa yetu ya TAG hukitumia kila Jumapili (kitabu cha Sunday School)

Lengo la maandalizi hayo ni kuweka mwongozo kwa walimu watakaposimama katika ufundishaji wao.

Mwanzo niliingiwa na kawoga kidogo kwa sababu ya ukubwa wa kanisa ninaloabudu.

Ukubwa kwa maana ya wingi wa watumishi walipo kanisani, elimu ya juu sana kitaaluma waliyo nayo wengi, nguvu ya uchumi nk.

Nikasema mimi ni nani miongoni mwa washirika karibu elfu mbili hivi tunaoabudu katika kanisa hili la mahali pamoja.

Utumishi huo nimeufanya katika mazingira magumu, na wewe Sam unajua kwa sababu kuna mambo kadha huwa nakushirikisha.

Baada ya kutumika hivyo kwa mwaka mzima, nilimwomba Mch wangu nipumzike kidogo kwa sababu mazingira yangu si rafiki sana (unajua Samson).

Lakini juzi nilipigwa shock nilipopigiwa simu na ofisi ya Mch kuwa hiyo huduma niendelee nayo bila kujali mazingira hayo.

Nimepokea kwa moyo wa kunyenyekea sana nikijua si mimi bali ni kwa Roho wa Mungu.

Mch Sam, mimi ninamshukuru sana Mungu kwa maono aliyokupa uyasimamie kupitia Chapeo ya Wokovu.

Kama kuna watu fulani ambao wamekutana na Mungu aliye hai kupitia Chapeo ya Wokovu, basi mmoja wao ni mimi.

Namshukuru na kumtukuza Mungu, nawe ukapokee sikuzote thawabu ya utumishi huu toka kwa Bwana.

Yawezekana kabisa unapanda kwa machozi, lakini shuhuda kama hizi zikupe kigelegele cha shangwe.

Ndimi mtumwa wa Kristo Yesu Bwana wangu.